*Naendelea kusimama kama Galileo Galilei

Mjadala unaoendelea sasa miongoni mwa Watanzania wengi, ni huu unaohusu Rasimu ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, iliyozinduliwa wiki iliyopita.

Yamezungumzwa na yataendelea kuzungumzwa mengi, yote yakiwa na lengo la kuboresha rasimu hiyo ili hatimaye hiyo ndoto ya kuwa na Katiba bora yenye maslahi kwa Watanzania wote, iweze kutimia.

 

Naomba niweke wazi kwamba mimi ni miongoni mwa waumini wakuu wa Muungano wa Tanganyika na Zanzibar. Kwa maana hiyo, mimi ni mmoja wa Watanzania wanaoumizwa na kauli za kuubeza Muungano na zenye mwelekeo wa kuuvunja.

 

Katika kipindi cha Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) wiki iliyopita, msomi mmoja wa Kenya (jina nimelisahau), kwenye majadiliano aliwaeleza Watanzania mambo ya maana sana. Alitutaka tufanya yote, lakini Muungano huu wa Tanganyika na Zanzibar uendelee kudumu. Hiyo ndiyo sala ya Waafrika wengi wapenda umoja na mshikamano wa Bara la Afrika.

 

Kama nilivyosema, tangu rasimu ilipozinduliwa, kumekuwapo mijadala mikali karibu kila mahali katika Taifa letu. Wengi wameipongeza. Lakini ni ukweli ulio wazi kwamba sehemu iliyowagusa wengi ni ya aina ya Muungano. Rasimu imependekeza muundo wa Serikali tatu -Tanzania Bara, Zanzibar na ya Shirikisho. Mjadala unaoendelea upande wa Tanzania Bara kwenye suala hili si mkali kama ilivyo kwa upande wa Zanzibar. Kwa upande huo wa wenzetu, kinachoonekana wazi ni kutoutaka Muungano, ingawa kwenye maelezo yao ni kwamba wanautaka.

 

Mimi si mtaalamu wa historia, lakini nadiriki kusema kwa uelewa wangu sijapata kuujua ‘Muungano’ wa nchi mbili ambazo kila moja ina uwakilishi kamili wa ‘ki-nchi’ katika vyombo mbalimbali vya kimataifa kama vile kwenye Umoja wa Mataifa (UN). Wazanzibari kadhaa wanataka muungano wa aina hiyo!

 

Wananchi wa Tanzania Bara, pengine kwa kuchoshwa na maneno ya Wazanzibari, nao wameamua kuidai Tanganyika yao. Kwa kadiri ya mjadala ulivyo, na kwa kubarikiwa kwa Serikali Tatu kwenye rasimu ya Katiba, siioni Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Naziona Tanganyika na Zanzibar, na pengine miaka si mingi, Zanzibar nayo itakuwa na Unguja na Pemba.  Tanganyika nayo sidhani kama itakuwa salama kwani tayari kumeanza kuwapo madai mazito ya Makonde Land! Kila ninapojaribu kuyatafakari haya, napata shaka juu ya hatima ya Taifa hili ambalo kwa miongo mitano limekuwa la kupigiwa mfano katika Afrika.

 

Tunaweza kuwapuuza, kuwakejeli na hata kuwatukana waasisi wa Muungano wetu (kama inavyotokea sasa kwenye mitando ya kijamii), lakini ukweli ni kwamba maneno ya manabii yana kawaida ya kutimia. Manabii tunaowasoma kwenye vitabu vitakatifu walikuwa wanadamu. Kama hivyo ndivyo, sioni ni kwanini maneno kama ya Mwalimu Nyerere kuhusu Muungano, yasiwe ya kinabii.

 

Nakumbuka mwanzoni mwa miaka ya 1990, Baba wa Taifa alizungumzia sana ubovu wa uongozi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM). Akawa tayari kutamka wazi kwamba kama kungekuwapo chama kingine makini chenye sifa za kuliongoza Taifa, asingehangaika kuikosoa CCM.

 

Lakini akaonya kwa kusema kwamba mwanaume akiamua kumwacha tu mkewe kwa sababu anazozijua –  hata kama hazina uzito; na akaoa mke mwingine; lakini baada ya muda akagundua kuwa huyu aliyemuoa ni balaa zaidi, itakuwa vigumu sana kumrudia yule wa awali.

 

Naam, maneno haya nikiyalinganisha na huku twendako kwenye Serikali Tatu, nayaona yakielekea kutimia. Leo tunaweza kuuona Muungano wa Serikali mbili ni mbaya – isipokuwa unaofaa ni wa Serikali Tatu – lakini sidhani kama tukishaonja shubiri yake, tutakuwa tayari kurejea kwenye Serikali mbili au moja! Sidhani. Kitakachotokea ni kifo cha kitu kinachoitwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na mparaganyiko wa hawa wawili waliojitenga. Huu ndiyo ukweli wenyewe.

 

Mwalimu Nyerere katika kitabu chake cha unabii cha ‘Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania’, anasema maneno haya, “Kwa ghiliba za viongozi na hasira za mkizi wamefanywa waonekane kuwa sasa wao wote, pamoja na viongozi wetu, wamekuwa ni mbuya na makomredi wa kushuku Muungano. Badala ya kuwasaidia wananchi wenzao kwa kuishughulikia Selikali yenyewe na ubovu wake, wanataka kuongeza Serikali ya Tatu! …Nadhani akilini mwao Muungano na Ramani ya Zanzibar; na maadamu ‘tumechoka na Wazanzibari’, basi na waondoke warudi walikotoka, wakifungasha na Muungano wao na Rais wao! Kwa hiyo, kama majuha au mazuge tunaendelea kuimba wimbo wa Serikaili tatu, na nchi inazidi kuserereka kuelekea gema la hifaki.”

 

Kwa kweli kinachofanywa na viongozi wetu, kiasi cha kuaminiwa na wananchi wanaoshinikiza Serikali tatu, ni uvivu na uzembe wa kutatua kero za Muungano.

 

Mwalimu anaendelea kusema, “Tulitazamia kuwa Serikali ya Muungano itapinga hoja ya Utanganyika, na kuwaarifu wabunge kwamba Kamati hiyo itapokamilisha kazi yake Serikali itafikisha mapendekezo yake bungeni. Badala ya kufanya hivyo, Serikali ya Muungano ikaamua kuwa mfumo wa Serikali Mbili haufai, kinachofaa ni mfumo wa Serikali Tatu. Hivi sasa sera ya Serikali ya Muungano ni muundo wa Serikali Tatu.

 

Itawezekanaje Serikali hiyo hiyo ikae chini na Serikali ya Zanzibar kuzungumzia umuhimu wa kutii, au jinsi ya kurekebisha muundo wa Serikali Mbili? Kwao Katiba hiyo inachongojea ni kufutwa tu. Mapendekezo ya Kamati ya Ndugu Shellukindo na wenzake hayana maana tena kwa Serikali hii. Serikali ya sasa inachosubiri na inachokishughulikia ni Shirikisho la Serikali Tatu – kwa kweli kufa na kuzikwa kwa Tanzania. Hawana uhalali, wala uwezo, wala nia ya kuzungumza Muungano wa Serikali Mbili. Kwa kweli jambo moja ambalo waheshimiwa hawa wamefaulu ni kufanya watu waache kabisa kuzungumza Katiba ya sasa na mambo mengine yale muhimu, na wabaki kumkimbiza sungura wa Serikali ya Tanganyika ndani ya Muungano”.

 

Maadamu matatizo halisi ya Muungano hayazungumzwi wala hayashughulikiwi, watu wenye nia mbaya, wa Bara na Visiwani, wanaopenda kuitumia hali hiyo kuivunja nchi yetu wanaendelea kufanya hivyo. Na wale, wa huku na huku, wanachocheana kama mifukuto ya shetani. Na hiyo inawafanya hata watu wasio na nia mbaya, ila ni wajinga tu, waamini kuwa inafaa wote tushiriki na tujiandae kuivunja Tanzania tusije tukashtukia kuwa Tanzania imevunjika na tumeachwa katika mataa! Anayedhani kuwa viongozi wetu ni wajinga yafaa akachunguzwe akili zake! Wanajua wafanyalo.

 

Nimesema awali kwamba ‘Wazanzibari’ na ‘Watanganyika’ ni marafiki wakuu. Matendo ya ‘Wazanzibari’ ni kisingizio kizuri cha matendo ya ‘Watanganyika’: na matendo ya ‘Utanganyika’ ni kichocheo cha ukabila wa upande wa pili. Wenyewe wanauita ‘Utaifa’, na ni sawa maana ni wa kupinga Utanzania.

 

Serikali yenye msimamo wa Utanganyika haiwezi kukaa na Serikali ya Zanzibar kuzungumza katiba hii ya Serikali Mbili. Hilo linaweza kufanywa na Serikali mpya ya Jamhuri ya Muungano: Serikali inayokubali na kuheshimu Katiba tuliyo nayo. Serikali ya sasa haina uhalali wala uwezo wala nia ya kuizungumza, ukiacha mazungumzo ya kuitia maji ili kuwafurahisha ‘Wazanzibari’, au kuifuta ili tulete Shilikisho la Serikali Tatu na hivyo kuwafurahisha ‘Watanganyika’.

 

Tufanye nini? Maadam ‘Watanganyika’ wengi wameitaka Tanganyika yao, halina budi litokee. Hata hivyo, hiyo haina maana kwamba sote tunakubaliana na jambo hili.

 

Kila mwenye akili ya kawaida kabisa anayewasikiliza watu wa Bara na pia akawasikiliza kwa makini wale wa Visiwani, wakiongozwa na wapinga Muungano, haoni kama kuna kitu tena kitakachoitwa Tanzania.

 

Vyovyote iwavyo, Muungano wa Tanganyika na Zanzibar ni muhimu kwa pande zote mbili. Zanzibar ni muhimu kwa Tanganyika kwa sababu nyingi, zikiwamo za ulinzi na usalama.

 

Zanzibar inaihitaji zaidi Tanzania Bara pengine kuliko Bara inavyoihitaji. Ulevi wa wanasiasa wanaotaka kuuvunjulia mbali Muungano, utawagharimu wananchi wasiokuwa na uwezo wa kupinga wanachohimizwa kukitenda.

 

Mwanasayansi mahiri, Galileo Galilei, kazi zake nyingi ziliufanya utawala wa Papa umweke kizuizini maana alionekana kupingana na ‘uumbaji wa ‘Mungu’. Akiwa amegundua mambo mengi na kuyathibitisha kisayansi, akatakiwa na Kanisa ayakane. Akakataa kuyakana. Hatimaye akafungiwa kizuizini ndani ya nyumba kwa miaka minane kabla ya kufariki dunia mwaka 1642 akiwa kipofu kwa sababu ya kukosa mwanga.

 

Mwaka 1758 Kanisa likaanza kuondoa baadhi ya vikwazo kwa kazi za utafiti wake. Matokeo yake, mapapa wengi waliofuata baada ya karne ya 20 walizikubali na kuzitambua kazi zake, zikiwamo zile za kuwapo kwa sayari zaidi ya dunia, dunia kulizunguka jua na kadhalika. Sasa anatambulika kwa kimombo kama “The Father of Modern Science.”

 

Vivyo hivyo, itatuchukua miaka kadhaa (si 400 kama ya Kanisa kumtambua Galileo), kabla kizazi cha Tanzania kukiri kilichosemwa na Mwalimu.

 

Ninachosema hapa ni kwamba ingawa tunampuuza Baba wa Taifa leo kwa kejeli na kudhani mtazamo wake umepitwa na wakati, kadiri miaka itakavyokwenda ndivyo ukweli wa yale aliyoyasema utakavyozidi kujidhihirisha kama ilivyokuwa kwa Kanisa na Galilei.

 

Nami kwa hili la muundo wa Muungano wetu na hatima ya Tanzania, nabaki kuwa na msimamo wa Galilei hata kama tunatofautiana na wengi. Maandiko hayafutiki.

1143 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!