Ni miaka 14 sasa tangu Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alipoaga dunia Oktoba 14, 1999 katika HospitalI ya St. Thomas jijini London. Ilikuwa siku ya majonzi makubwa kwa Watanzania kumpoteza mtu aliyetumainiwa na wengi kama nguzo na dira ya maono kwa Taifa la Tanzania.

Ilikuwa siku ngumu na yenye uchungu mwingi kumpoteza mtu  aliyesimamia na kuenzi misingi ya haki, umoja, utu, usawa na kujitegemea. Hakika pengo lake  halitazibika. Popote unaponisikia pumzika kwa amani Baba wa Taifa.

Miaka 14 baada ya kifo cha Mwalimu Nyerere naiona laana kwa Taifa hili la Tanzania, itakayozidi kuparaganisha Taifa hili kama watu hawataamua  kuacha woga na kufanya mabadiliko ya kweli.

Mwalimu Nyerere alipata kusema, “Wananchi wanataka  mabadiliko, wasipoyapata ndani ya CCM, watayatafuta nje ya CCM.”

Leo hii binafsi sioni misingi aliyoiasisi Mwalimu Nyerere ikisimamiwa na kufuatwa na hata kuleta mabadiliko ya kweli kwa Watanzania. Siuoni umoja wa

dhati wala juhudi za dhati za kujali kulitoa Taifa hili kwenye  utegemezi kama jinsi Mwalimu alivyofanya juhudi hizo kupitia Azimio la Arusha.

Sioni kiongozi wa chama alichoasisi Mwalimu akikemea na kupinga rushwa kwa dhati na watu walioko chini yake wakamsikia na kumuamini na

kufuata maagizo yake. Nasikitika simuoni hata mmoja, wote wameisahau misingi na ni kama vile wanalamba kisogo alichokiasisi Mwalimu.

Leo hii wengi wanaona kinyaa hata kulitaja Azimio la Arusha achilia mbali kufuata japo machache kati ya mengi ya msingi kwenye Azimio  hilo! Wapo viongozi hawataki hata baadhi ya hotuba za Mwalimu zisikike kwa  wananchi maana  wanaona kama alizitoa kwa kuwalenga wao binafsi, kutokana na matendo na mienendo yao mibaya.

Miaka 14 ya kumbukumbu ya kifo cha Mwalimu ituzindue fikra zetu tujue kuwa Taifa hili lilijengwa kwenye misingi na jasho na damu za Watanzania wenzetu japo kuna wakubwa wameparaganyua misingi  hiyo.

Miaka 14 itoshe kuwakemea na kuwakataa viongozi waliojilimbikizia mali na kupenda kujaza matumbo yao, viongozi waliogeuka mchwa wanaotafuna rasilimali za Taifa tulizopewa bure na Mwenyezi Mungu.

Viongozi hao wamesahau misingi aliyoiasisi Mwalimu, ni wabinafsi na wamejilimbikizia mali kila kona ya nchi hii, ingawa wengi wao walikuwa waumini wazuri wa fikra za kisiasa, mitazamo na maono ya Mwalimu, lakini punde baada ya kuona ameaga dunia wakayatoa makucha  yao na sasa wanapigana vikumbo kuivunja  misingi iliyojengwa na Mwalimu.

Mmoja akipitisha meli yenye shehena ya pembe za tembo,  mwingine anajimegea vitalu vya uwindaji, mwingine akijichotea fedha kwa kampuni feki za mifukoni, mwingine anakabidhi migodi ya madini inahujumiwa na wajanja wachache!

Hao tuwakatae na kuwakemea kwa sauti za ukali kisha tuwachukulie hatua maana utadhani waliombea Mwalimu aage dunia ili wafanye watakavyo.

Inasikitisha watu waliosomeshwa bure na Mwalimu leo wamekosa ubunifu wa kutumia rasilimali zilizopo kuendelea kusomesha bure na kusimamia elimu

bora kwa watoto wa maskini wa Kitanzania.

Leo elimu yetu imekosa dira na uelekeo madhubuti na juhudi za dhati kuikwamua na kuiinua  angalau ifanane na elimu ile ya enzi za Mwalimu, hazionekani maana watunga sera na wanaopaswa kuzisimamia hawaziamini hata sera wanazozisimamia kuwa zitakuwa na ufanisi kwenye shule zetu za ukata. Wao wanapeleka watoto wao kusoma nje ya nchi na kwenye shule bora za kimataifa, wanaacha wengi wasio na uwezo wafaulu wakiwa hawajui kusoma na kuandika. Hii ni laana!

Leo hii Mwalimu anatimiza miaka 14 akiwa ameacha chama chenye kundi lisiloitakia mema Tanzania. Kwa busara zake na kuona mbali kwake, Mwalimu alikubali mfumo wa vyama vingi japo karibu asilimia kubwa waliukataa, yeye alijua una manufaa kwa nchi. Leo hii kakikundi ka watu wachache wanaotaka kulinda maslahi yao binafsi, wanachakachua mchakato wa Katiba mpya ili ulinde maslahi yao na chama chao badala ya maslahi ya Taifa. Wamesahau kuwa Mwalimu alisisitiza siasa safi na uongozi bora.

Leo baadhi ya wanachama wa chama alichoasisi Mwalimu wanafanya siasa za kilaghai, ubabe na chuki kwa vyama pinzani.  Inasikitisha kuwa aliowaacha Mwalimu wengi wao hawana mishipa ya ujasiri kulisemea hilo, wako kimya.

Enzi za uhai wake, Mwalimu alipata kuwaeleza wajumbe wa CCM juu ya viongozi bora. Leo miaka 14 baada ya kifo chake unaweza kusema alikuwa anawapa majibu kuwa CCM imefika mwisho wa kutoa kiongozi bora, aliwaasa wana-CCM na Watanzania kumuogopa mtu anayekimbilia Ikulu kama ukoma.

Leo hii tunaona mbio zinazoambatana na mafurushi ya fedha kwa watu wanaotajwa kuiwania Ikulu. Hao ndiyo tumeaswa na Mwalimu tuwaogope kama ukoma.

Kwenye kitabu chake cha ‘Uongozi Wetu na Hatima ya Tanzania’, Mwalimu anasema, “Lakini hatulazimiki kuendelea na uongozi mbovu wa chama na Serikali. Wala tukiendelea na hali hii, bila kubadili uongozi wa chama na Serikali sina hakika kama tutafika huko salama… majuto ni mjukuu huja baadaye.”

Nihitimishe kwa moja ya kauli kwenye hotuba ya Mwalimu mwaka 1995 alipohutubia wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM pale Dodoma, alisema,

 

“…Watanzania wanahitaji mabadiliko, wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.” Nakulilia Mwalimu, wao wanakulamba kisogo.

0713 246 764


1179 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!