Kenya's President Uhuru Kenyatta (L) greets opposition leader Raila Odinga of the National Super Alliance (NASA) coalition after addressing a news conference at the Harambee house office in Nairobi, Kenya March 9, 2018. REUTERS/Thomas Mukoya/File Photo

MOROGORO

Na Mwandishi Wetu

“Ni nani atakayetuondolea lile jiwe?” Swali gumu walilojiuliza wanawake watatu wa kwenye Biblia ile siku ya kwanza ya juma walipokwenda kaburini wakiwa na nia ya kumpaka mafuta Yesu (mwili wa Yesu uliokuwa umezikwa kaburini) kukamilisha taratibu za maziko ya Kiyahudi.

Swali kama hili linatukabili Watanzania wa leo, tukijiuliza ‘ni nani atakayetuondolea hili jiwe la uhasama kati ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chaderma) na Chama Cha Mapinduzi (CCM)?’

Uhasama kisiasa ni uchu, uadui, mtazamo au ni hatua mbaya kinyume cha hali fulani njema, ambayo huchochea vurugu/tofauti miongoni mwa jamii na kusababisha machafuko huku watu wenye hekima wakishindwa kuyazuia kwa kutowajibika.

Pamoja na nia njema ya wanawake wale wa kwenye Biblia, mbele yao kulikuwapo vikwazo lukuki vya kuwakatisha tamaa; cha kwanza kilikuwa jiwe lililowekwa mlangoni mwa kaburi.

Maandiko (Marko 16:4) yanasema jiwe hilo lilikuwa kubwa na wao walijua isingekuwa rahisi kwao kuliondoa waweze kuingia ndani ya kaburi.

Kikwazo kingine kilikuwa ni askari wa Kirumi waliokuwa wakilinda kaburi hilo. Hawa walisifika kwa uhodari, ukakamavu na ushujaa wao. 

Wakiwa kwenye lindo hawalali, wala hawanunuliki kirahisi. 

Kikwazo cha tatu, kaburi lenyewe lilikuwa limepigwa muhuri (lakiri) wa gavana (seal) kuzuia watu kulifungua!

Pamoja na hayo, akina mama wale waliamua kwenda kaburini kujaribu kutimiza nia au wajibu wao. Mungu mkubwa, walipofika kaburini, walikuta jiwe limeviringishwa mbali, askari wamekimbia, na Yesu amefufuka!

Kama ilivyokuwa kwa Warumi kuweka jiwe kwenye kaburi la Yesu, wakoloni (wa ndani na nje ya Afrika) kwa manufaa yao, wametuwekea ‘jiwe’ la tamaa mbaya ya uhasama wa kisiasa.

Kwa ukubwa wa jiwe hilo, uhasama umesababisha umwagaji damu nyakati za uchaguzi. Sasa tuna jiwe la watoto yatima, wajane na wagane wanaochuruzika machozi kila siku.

Ndugu hawa wa waathirika wa masuala ya kisiasa yumkini hawajui na hawana hatia yoyote! Wamejikuta katika hali ngumu kimaisha, wakiishi katika unyonge na umaskini mkubwa.

Hivi, tutapataje kupona mbele za Mungu kwa machozi ya watu hawa? Tutasingizia mabadiliko ya tabia nchi, kumbe ni adhabu ya mawazo, maneno na matendo yetu maovu.

Jiwe la tamaa mbaya ya mali na uhasama wa kisiasa limesababisha kuwepo vijana na wazee wanaokufa kwa dawa za kulevya na magonjwa mbalimbali yakiwamo ya zinaa.

Lipo pia jiwe la talaka linalosambaratisha ndoa na kuongeza watoto wa mitaani unapotekelezwa uhasama wa kisiasa ulioagizwa na wakoloni.

Ni nani atakayetuondolea ‘jiwe la dhuluma’ za haki za wanyonge kwa kisingizio cha kutafuta mali, au kuleta maendeleo? Nani atakayetuondolea jiwe hili la mauaji ya watu wasiokuwa na hatia kwa sababu za kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni zikirembeshwa na tamaa ya madaraka na ubinafsi?

Kwa asili nzi ni mdudu mchafu, lakini kuna mambo tunaweza kujifunza kwake. Ukiwa umetulia utamuona anachezesha miguu ya mbele, ya nyuma na mbawa zake.

Vitendo vyake hivi ni sawa na kusema: “Ukijua ya mbele, mimi nayajua ya nyuma. Ukijua ya kushoto, mimi najua ya kulia.”

Usipomfukuza haraka, atakuachia vimelea vya magonjwa kwenye chakula na kukusababishia gharama kubwa za matibabu! 

Hili ni fumbo. Tukiendekeza uhasama wa kisiasa kwa tamaa ya madaraka; mipango, maendeleo ya kisiasa, kiuchumi, kiutamaduni, kijamii iliyokuwa iende mbele inarudi nyuma.

Muda uliokuwa utumike vizuri kuyapeleka mambo kulia kwenye tija, utatumika kutuelekeza upande usio na tija (kushoto).

Ni nani, kama si Mungu, atakayethubutu hata kulikaribia jiwe hilo kama lina muhuri wa gavana au mtu mwingine mwenye mamlaka? 

Kwa mtazamo wa kibinadamu unaweza kudhani hakuna. Yaani haiwezekani. Kwamba ‘jiwe ni kubwa mno’.

Lakini maandiko yanasema lisilowezekana kwa binadamu kwa Mungu linawezekana.

Kumbe tuna uwezo wa kuondoa kila aina ya jiwe linalotusumbua, hata kama linaonekana kuwa kubwa kiasi gani, tukiwa na dhamira ya dhati na ya pamoja.

Hatua za awali tunazochukua ni muhimu sana katika mafanikio yetu kimwili, kiroho na kiakili.

Kumbuka wale akina mama waliamua kwenda kaburini wakijua fika ukubwa wa matatizo yaliyopo mbele yao. 

Kwa kuwa walikuwa na nia moja, wakachukua hatua wakiamini Mungu atawawezesha. Hata sisi tunapaswa kuchukua hatua sahihi zitakazotusaidia kuboresha hali tuliyonayo pasipo kumkosea Mungu, au kutuingiza katika majuto.

Ni vema kumuomba Mwenyezi Mungu atupe hekima na uwezo wa kuyashughulikia yanayotukera, zaidi sana tuwaombee wenye mamlaka ili Mungu aseme nao na kuwaponda mioyo yao wajue wajibu walionao kwa Mungu na kwa binadamu.

“6. Kwa upendo na uaminifu uovu huondolewa; kwa kumcha Bwana mtu hujiepusha na ubaya. 7. Njia za mtu zinapompendeza Bwana, huwafanya hata adui zake waishi naye kwa amani.” (Methali 16:6-7).

Mbaazi ikikosa maua, husingizia jua! Watanzania na wenye hekima tukihasimiana au kuona magumu, badala ya kuchukua hatua kwenda kama wale wanawake wa Biblia, tumekuwa na tabia na visingizio vya mambo ya kubumba tukiwasingizia wageni na majirani kila mara, hata kama nyakati fulani yapo.

Kuna mtu mmoja (jina linahifadhiwa) amewahi kusema: “Uhasama uliopo kati ya CCM na CHADEMA unaweza kutumiwa na watu wa nje kutugombanisha.”

Hii ni kweli, lakini pia unaweza kutumiwa na watu wa ndani kutugombanisha! Kwa mfano; si sahihi kwa wenye hekima kukaa kimya ili watoto wapigane hadi apatikane mshindi kwa kuwa mmoja atakuwa ameumia.

Maandiko matakatifu yanasema: “Lakini hao walio nje Mungu atawahukumu. Ninyi mwondoeni yule mbaya miongoni mwenu.” 1 Kor 5:13.

Aliyetaka kuzuia ukombozi wa Israeli lilikuwa jiwe kubwa. Je, mimi na wewe ni jiwe kubwa la ustawi wa haki, amani na ustawi wa nchi yetu? Ifahamike ndimi zenye kauli mbili ni jiwe kubwa nchini mwetu!

Nani anayefaidika na uhasama huu?

Ukitaka kujibu swali hili lazima ukumbuke msemo; ‘wanapogombana fahari wawili ziumiazo ni nyasi’, na nyasi kwa maana ya makala hii ni wananchi na maendeleo yao katika sekta mbalimbali.

Katika hili ndiyo maana kuna wakati shetani naye huenda kulalamika kwa Mungu anapoona binadamu wanafanya mambo ambayo hata yeye  hawezi kufanya.

Hujitetea kwa Mungu akisema yeye hakuwatuma binadamu kufanya hayo, wamefanya kwa utashi wao.

Wenye hekima waliondoa jiwe kwenye kaburi la Yesu ili hofu na kilio cha wale akina mama viondoke. Walikuwa ni malaika na walinzi waliothibitisha umahiri na kilichosababisha amani ikapatikana kwa taifa zima.

Je, wako wapi wenye hekima wetu Tanzania? Wazee, viongozi wastaafu, viongozi wa dini, taasisi, asasi mbalimbali za haki? Mbona wameshindwa kuzuia yaliyotokea na yanayotokea yasitokee?

Katika kukomesha umwagaji damu zisizo na hatia wakati wa uhasama wa kisiasa kati ya Uhuru Kenyatta na Raila Odinga wa Kenya, wenye hekima nchini humo walisimama mstari wa mbele kushinikiza viongozi hao kukaa katika meza ya mazungumzo na kumaliza tofauti zao.

Akihutubia wabunge na maseneta, Kenyatta akawataka kuungana naye pamoja na Odinga kuhubiri maridhiano baada ya uchaguzi uliomwaga damu za watu.

Viongozi wa dini walikuwapo kuongoza kuondoa tofauti hizo! Je, hapa kwetu itawezekana?

Kenyatta alisema, mauaji na uharibifu wa mali uliojitokeza haustahili kujitokeza tena katika historia ya Kenya. Akaomba radhi kwa Wakenya iwapo matamshi aliyoyatoa wakati wa kampeni yaliligawa taifa, akisema  hatua yake ya kumaliza tofauti na Odinga ilikuwa ni kwa sababu ya umoja wa taifa hilo. 

Kwa mara ya kwanza siku hiyo wabunge na maseneta wa upinzani walihudhuria hotuba ya Rais Kenyatta.

Hakuna anayetamani ya Kenya yaje kutokea Tanzania, kwa kuwa wajukuu watakuja kuyapiga makaburi ya wenye hekima wakidai hawakuwajibika.

By Jamhuri