Tanzania haiwezi kuendelea kisiasa, kiuchumi na kiutamaduni, kama haitabadili mfumo wa elimu na kuwekeza zaidi katika sekta hizo.

Tanzania iliyopata Uhuru wake mwaka 1961, imekuwa ikikabiliana na mambo makuu matatu kwa ajili ya maendeleo yake ambayo ni ujinga, maradhi na umaskini.


Mambo hayo yaliyoitwa kuwa ni maadui wakubwa wa maendeleo ya nchi, yameathiri uchumi wa nchi kabla na baaada ya Uhuru na kusababisha matatizo ya kutokuwa na wataalam wa kutosha katika fani mbalimbali, kutokuwa na miundombinu bora na uzalishaji mdogo.


Mipango mbalimbali ya maendeleo ya muda mfupi na muda mrefu, imekuwa ikibuniwa katika kukabiliana na umaskini na kukuza uchumi. Juhudi za kukuza uchumi na kuondokana na umaskini zinaendelea.

 

Katika kipindi cha miaka 50 ya Uhuru wa Tanganyika, kuna mipango na dira mbalimbali imeandaliwa ili kuhakikisha nchi inapata maendeleo kwa lengo la kupunguza umaskini na kukuza uchumi.


Baadhi ya dira hizo ni pamoja na Azimio la Arusha la mwaka 1967, lililofafanua falsafa ya ukombozi wa kiuchumi na kijamii chini ya misingi ya Ujamaa na Kujitegemea kama lengo la muda mrefu kwa Watanzania.


Februari 1967 Dira ya Maendeleo ya Taifa sawia na sera za mageuzi ya kijamii na kiuchumi, zikawa zikiongozwa kwa misingi ya Azimio la Arusha. Dira ya pili ni Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025 iliyoanza kutekelezwa mwaka 1995 – inayoongoza harakati za maendeleo ya uchumi na jamii kufikia 2025.


Mkakati wa kitaifa wa kuondoa umaskini (National Poverty Eradication Strategy (NPES) uliokuwa na lengo la kupunguza umaskini ifikapo mwaka 2010, ulitoa dira kuhusu umaskini na uboreshaji wa maisha ya jamii. Madhumuni yake yalikuwa ni kutoa mwongozo kwa wadau wote katika kutambua, kutekeleza na kutathmini hali ya umaskini.

 

Malengo ya mkakati huo yalikuwa kuangalia ukuaji wa uchumi, kipato, elimu ya msingi, upatikanaji wa maji, magonjwa, afya na vifo, ajira, makazi na miundombinu, kuratibu sera na programu kwa muda mfupi na mrefu.

 

Mkakati mwingine ni ule wa misaada Tanzania – Tanzania Assistance Strategy (TAS). Huo ulikuwa ni mkakati wa muda mfupi wa kitaifa wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, uliojumuisha mikakati ya Serikali na ya kimataifa katika kupunguza umaskini na kukuza uchumi.

 

Pia kulikuwa na Mkakati wa Kupunguza Umaskini (Poverty Reduction Strategy Paper-PRSP 2000-2003) ulioandaliwa na wadau. Mkakati huo ulilenga zaidi katika kuondoa umaskini ingawa katika utekelezaji wake ulikumbwa na changamoto za udogo wa bajeti.

 

Katika jitihada za kukuza uchumi na kuondoa umaskini na kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa 2025, Serikali iliandaa na inaendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Uchumi na Kuondoa Umaskini Tanzania (MKUKUTA).


Mkukuta ni mwendelezo wa mikakati ya kuondoa umaskini na kukuza uchumi. Awamu ya kwanza ya Mkukuta iliandaliwa mwaka 2004 na kupitishwa na Bunge, Februari 2005 na utekelezaji wake ulianza rasmi katika mwaka wa fedha 2005/2006, ukiwa wa miaka mitano 2005-2010.


Mkukuta wa kwanza ulitekelezwa kupitia nguzo kuu tatu ambazo ni; Ukuaji wa uchumi na kupunguza umasikini wa kipato, maisha bora na ustawi wa jamii na utawala bora na uwajibikaji. Lakini pamoja na mipango hiyo, bado Tanzania haina uchumi imara mbali na kuwa na rasilimali nyingi.


Tafiti nyingi zilizofanywa hapa nchini, ukiwamo ule uliofanywa na Taasisi ya Utafiti wa Uchumi (REPOA), zimebaini kuwa bado kuna ongezeko kubwa la umaskini unaochangiwa na kutotekelezwa kwa sera za mipango ya maendeleo.


Akizungumza na JAMHURI hivi karibuni, Mbunge wa Afrika Mashariki, Nderakindo Kessy, amesema kwamba yote hayo yatawezekana iwapo mfumo wa elimu utabadilika na serikali kuwekeza zaidi katika elimu. Amesema elimu ndiyo njia sahihi itakayoiwezesha Tanzania kuendelea kiuchumi.


“Kwanza kabla ya kuendelea mbele, lazima tujue elimu ni nini na msomi ni nani – awe wa darasa la saba, kidato cha nne, cha sita, au Chuo Kikuu. Wanafalsafa na wanazuoni wa sehemu mbalimbali ulimwenguni, kwa muda mwingi hata kabla ya kuzaliwa Kristo, wamejaribu kutoa na kufafanua maana ya elimu katika muktadha tofauti tofauti.


“Pamoja na wingi wa ufafanuzi huo wa wanafalsafa na wanazuoni, bado kuna maeneo wanakutana na kukubaliana. Karibu wote wanaiona elimu kama mchakato; pili wanaiona elimu kama mabadiliko au ujenzi wa binadamu na tatu wanaiona elimu kama maisha ya mtu katika jamii.


“Elimu ni mchakato ambapo mtu hupata maarifa na ujuzi wa kujitambua na kujiweka sawa katika kupambana na mazingira na mabadiliko ya mara kwa mara ya kijamii, kisiasa na kiuchumi. Aidha, ni njia ya mtu kuweza kuutambua uwezo wake kamili,” amesema.

 

Anasema wanazuoni wengine wanaieleza elimu kuwa ni mchakato wa kufundisha au kukuza maarifa, stadi na maadili ya wanaojifunza. Pia elimu ni mfumo wa kujifunza na kufundisha unaozaa maarifa rasmi, maarifa matumizi, yaani ujuzi na stadi za maisha, pia maarifa ya upeo wa upembuzi na ubunifu, ambayo mtu hupata uwezo wa kufanya jambo jipya katika jamii.


Anasema Mwalimu Julius Nyerere alifafanua elimu kama mchakato unaomwandaa mtu aweze kukabili mazingira anayoishi; hivyo kuwa mzalishaji na si mnyonyaji (anayejitegemea).

 

Anasema Mwalimu Nyerere aliifanya elimu kuwa dira ya nchi kujitegema, hivyo elimu inapaswa kuwa mwanga wa ustawi wa jamii nzima, ichochee ushirikiano, haki na usawa katika jamii. Pia ilenge kwenye uhalisia wa maisha ya Tanzania.

 

Kessy amesema kuwa elimu itolewayo kwa sasa, haimsaidii mhitimu kujitumikisha bali kutumikishwa, kwa maana hiyo inamtafsiri kwamba ni mtu aliyeingia darasani na kupewa cheti tu bila kujua nini kilichompeleka darasani.

 

Unapotaja neno elimu kwa dunia ya sasa, unazungumzia maendeleo yatakayoleta mabadiliko katika jamii kwa wakati na kupata mahitaji muhimu. Lakini hilo halipo kwa sasa na ndiyo sababu ya kudorora kwa uchumi wa Tanzania.

 

“Mhitimu anatakiwa kuwa mbunifu kwa kutumia rasilimali zinazomzunguka katika kufanya kazi yake, ili kuleta maendeleo katika jamiii inayomzunguka, lakini hapa kwetu hakuna kitu kama hicho.

 

“Pili wasomi wetu wengi hapa nchini hawafanyi na si hawafanyi kwa sababu ya uvivu, bali hawajui kwa kuwa hawakufundishwa shuleni kwa vile hawajui kuchambua mambo  na kuyatekeleza, kutathmini na kuwa wabunifu wa mambo kutokana na mazingira aliyokuwa nayo,” amesema.


Amesema tafiti nyingi zinazofanywa na wasomi wengi hufanywa kwa kunakili, kwa kuziingiza katika makaratasi bila kutumia akili zao, na unapokuja katika uhalisia tafiti hizo zinashindwa kutekelezeka kulingana na mazingira.

 

“Siko huko lakini naambiwa kuwa asilimia 60 ya wasomi kutoka katika vyuo mbalimbali wanaofanya tafiti zao, ‘wanakopi na kupesti’. Mwaka jana nilikutana na vijana wa Chadema (Chama cha Demokrasia na Maendeleo) mjini Moshi, tukaongelea kuhusu pato la Taifa (GDP), nikagundua kuwa wengi hawajui kuhusu hili. Tukabishana pale lakini hawakunielewa kuwa wataalamu wanachukua fomula ya nchi zilizoendelea ndiyo wanapiga ili kupata pato letu.


“Lakini anachongalia ni maghorofa ya hapa mjini, lakini nyumba ya yule anayejenga kwa matope kijijini na kuezeka kwa nyasi au bati, wataalamu wetu hapa hawamhesabu, huyu anafaa kuingizwa katika GDP. Wanaangalia mjini zaidi. Hii ni kwa nchi zilizoendelea tu. Haya ni kutokana na kukopi na kupesti,” amesema.


Amesema kuna makosa makubwa katika kuangalia pato la taifa kwa kunakili kutoka nje. Huwezi kupata hesabu kamili. Wataalamu wanaopiga hesabu hizo huchukua hesabu zao kulingana na nchi zilizoendelea bila kuangalia uhalisia wa nchi ya kama Tanzania, hali inayofanya isiwe sahihi.


Nderakindo ambaye ni Mtaalamu wa Hisabati katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), anasema wakati wa Mwalimu Nyerere mahitaji muhimu yalikuwa yanapatikana kwa asilimia 60 kutokana mchango wa  wasomi. Lakini kwa sasa upatikanaji wa mahitaji muhimu umeshuka hadi kufikia asilimia 35, kutokana na wasomi kushindwa kutumia nafasi zao katika kutoa mchango wao katika maendeleo ya kiuchumi.

 

Amesema suluhisho la matatizo hayo ni kubadilisha mfumo wa elimu, kuongeza bajeti katika Wizara ya Elimu, watendaji wawe na taaluma sahihi ya elimu, katiba ya nchi ijayo ioneshe wazi wajibu wa Serikali katika kutoa elimu kwa kiwango fulani. Hii itasaidia wahitimu kujituma kuliko kutumikishwa.


Amemalizia kwa kusema Katiba mpya iainishe adhabu kwa watu watakaofanya utafiti kwa kunakili hata kwa ukurasa mmoja kutoka katika tafiti zilizopita.


 

1237 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!