Ndugu Rais, kama kuna wakati uligusa mioyo ya Watanzania na hasa masikini, ni pale uliposema, “Walidhani nitakuwa pamoja nao!” Kama hii ilikuwa ni ahadi, basi ni ahadi iliyotoka juu!
Nina hakika hii haimo katika ilani ya chama chako. Kwa ahadi hii uliwafanya Watanzania na hasa masikini wa nchi hii, walione tumaini lililopotea, likirejea! Yuko wapi mhubiri mwema, awahubirie wanawema habari hii njema? Kwani mimi ni nani baba, hata nikuambie ole wako usipoitimiza? Lakini mimi ni mtumishi wako japo sistahili! Nawiwa kukumbusha kuwa ulipoitoa kauli hii ya matumaini, Mungu wa Eliya, Mungu wa Ibrahimu alikusikia! Waambie uliowapa mamlaka kuwa huyafanyi haya kwa kutafuta sifa, bali unasukumwa na uchungu kwa masikini wa nchi hii! Kwako, nchi hii na vyote viijazavyo ni mali ya Watanzania wote kwa usawa wao.

Wanaodhani kuwa wana mamlaka ya kuvifanya vingine vionekane ni vyenu peke yenu, wanafanya ujinga unaoharibu kazi njema uifanyayo! Ndugu Rais, sijui Waziri wa Habari, Michezo na Utamaduni ni wa dini gani, lakini atambue kuwa mbele ya Mwenyezi Mungu, mwizi hana kinga! Bwana Yesu aliuliza, “Kama nimesema uongo toa ushuhuda. Lakini kama nimesema kweli kwanini unanipiga?”

Wananchi wana haki ya kujua Mawio walikosa nini? Utolewe ushuhuda kama upo. Vinginevyo tukiruhusu wababaishaji waendelee kupuyanga, wataua chombo kimoja baada ya kingine mtawalia! Watanzania siyo mabwege. Bado wanakumbuka walivyohenyeshwa na wale manabii wa uongo walioizunguka nchi nzima kwa miaka, wakipandikiza chuki katika nchi. Wanaosema leo kuwa zile fedha nyingi walizokuwa wanachezea hovyo ni matokeo ya dhambi ya makinikia, wanakosea wapi?
Anayemkingia kifua, ni mwizi mwenzake. Ulionao wengi ni wanafiki tu! Wako upande tofauti na kule ulikosimama. Baba, tambua hii vita unapigana peke yako!
Ndugu Rais, zile siku zipatazo thelathini za mwanzo kabisa, ulipofanya kazi peke yako ukisaidiwa na Waziri Mkuu wetu makini, Kassim Majaliwa, na Makamu wa Rais, Mama Samia Suluhu Hassan, uliwapa watu wako matumaini makubwa sana. Mlifanya kazi iliyo njema sana. Hakuna mwanzo unaokosa makosa, lakini busara ni kuyakiri na kujisahihisha! Ulipounda baraza jipya la mawaziri ukweli ulipoteza matumaini ya baadhi ya wananchi. Ukaleta Baraza jipya, lakini baadhi ya mawaziri walikuwa ni wa zamani ambao muda wao wa kutumika ulikuwa umepita.

Hawa uliwachagua mwenyewe au mazingira yaliyokuwapo yalikulazimisha uwe nao hata wale uliosema walidhani utakuwa nao?
Ukawarudisha wachovu wengi na hata wale waliolazimishwa na wananchi kupitia Bunge lao, kujiuzulu. Masikini walipolazimika kuwakubali wale waliowaambia kuwa wasitarajie mabadiliko katika msitu ule ule wenye nyani wale wale, lilikuwa kosa la nani? Ukweli hata ukisemwa na kichaa, unabaki kuwa ukweli. Kuukataa ni kujipumbaza mwenyewe.

Ndugu Rais, wananchi walipoambiwa hakuna tena ‘Bunge live’ hawakuamini masikio yao. Waziri mwenye dhamana alilisimamia mpaka ikawa kweli. Yalipomkuta ya kumkuta akakumbuka maneno ya wahenga kuwa mchimba kaburi huingia mwenyewe nukta kwa mkato! Watanzania wakapigwa marufuku kutembea kwa kufuatana na pia kuhubiriwa hadharani.
Nakumbuka vema baba, haukuwa wewe, bali jamaa mmoja sijui alilelewa wapi. Akasema, “Kuanzia sasa Watanzania marufuku kukutana hata vyumbani mwao”. Sijui huyu naye alikula maharage ya wapi! Lakini katika nchi zote duniani viongozi walevi wa madaraka, hawakosekani! Watawala wote waliofanikiwa ni wale waliomudu kuwadhibiti viongozi walevi waliowapa madaraka!
Hili la ESCROW limetingisha nguzo nyingine tofauti na makinikia.

Lakini wengi walioko katika dhambi ya makinikia ndiyo hao hao walioko katika dhambi ya ESCROW! Hatujui kama ni kutokana na ushauri au ni uamuzi binafsi. Likitekelezwa ipasavyo, lina nguvu kubwa ya kulirudisha tumaini lililopotea! Siamini katika washauri wabovu, bali katika rais anayewategemea washauri wanafiki. Kuche, kuchwe linajulikana sasa katika Mawio!
Ndugu Rais, kwa maana hiyo wote waliowahi kusimama hadharani na kusema fedha zilizoibwa ESCROW si za umma, sasa imethibitika pasipo kuacha shaka kuwa ni wezi, tena mafisadi wakubwa. Manyang’au hawa lazima wachenjuliwe maana sasa ni sawa na makinikia. Kila aliyetetea wizi huu ni mwizi wetu.

Zilitolewa kauli mbalimbali nyingine zikitoka kwa wanaojiita
waheshimiwa kumbe ni wezi tu. Washirika wao wakasema eti hata kama zile fedha zilikuwa zinahifadhiwa katika Banki Kuu ya Serikali fedha hizo hazikuwa mali ya Serikali. Watu walioaminiwa wakapewa mamlaka makubwa na wananchi, kumbe ‘majizi’ tu. Wezi walisimama hadharani bila kuona aibu wakasema fedha za ESCROW si za umma.

Wewe unaipora nchi halafu unasema hujui kwanini nchi hii ni masikini! Uko sawa sawa kweli? Hapa lazima haki itendeke. Anayemtetea mwizi ajumuishwe na mwizi mwenzake! Ni wakati sasa tuwakumbushe wananchi baadhi ya kauli zilizotolewa na wawakilishi wao walipokuwa wanatetea wizi huu bungeni. Alisikika mbunge mmoja kutoka visiwani akasema, “Nimesikiliza ripoti ya PAC na Serikali, lakini jambo hili lipo wazi kwamba fedha hizi hazikuwa za umma, zilikuwa za IPTL zimelipwa na Tanesco.”
Huyu waliomchagua wajue kuwa walimchagua mwizi! Mwenzake wa viti vya kusaidiwa akasema, “Hapa hatoki mtu. Si nani wala nani. ESCROW ni njama za wapinzani kutukoroga sisi wanachama chetu. Zile fedha si za umma. Tanesco ina madeni mengi, inadaiwa Sh bilioni 700. Waziri ameongea vizuri kwa hiyo tusipotezeane muda hapa.” Viti maalumu hata kwa wezi? Aliowatetea kuwa hawatoki leo ajiulize wako wapi?

Na mwizi mwingine akasema, “Tusiwavunje moyo wizara, wamefanya kazi kubwa. Tukiwa na utaratibu wa kufukuzana itaendelea hivyo hivyo, tumwogope Mungu, lakini nafsi zetu zitatusuta kwa sababu ya matendo yetu.
Hivi sasa kumezuka mtindo wa kusingizia mtu huyu kala, huyu kapewa mtu akipewa asimame hapa aseme amepewa, lakini tusiwasingizie. Hawa ndiyo wabunge wasiofaa waliotetea kile ambacho baba leo anatuonesha kuwa ni wizi!
Ndugu Rais, tambua kuwa unapigana vita hii peke yako, lakini wananchi watasimama na wewe! Ukiifikisha mwisho kwa haki, bila kumwonea mtu wala kumwogopa mtu, wananchi watalihifadhi jina lako katika vibao vilivyomo ndani ya mioyo yao!
Jina lako litarembeshwa kwa dhahabu ing’arayo na kutundikwa juu katika barabara kuu ili lisomeke hata na watu wa mataifa!

By Jamhuri