*Moto waanzia Pugu, Mlimani, sasa kuenea nchi nzima
*Unalenga kuwafunza watoto faida za kutumia benki

Benki ya NMB mara zote imekuwa mbele katika kubuni na kutekeleza miradi mbalimbali, yenye lengo la kuwainua Watanzania kimaisha.

Ni kwa sababu hiyo, haikushangaza kuona kwamba inakuwa ya hapa nchini kuzindua mpango wenye lengo la kuinua uelewa wa masuala ya kifedha kwa Watanzania, hasa wanafunzi. Kwa kimombo unajulikana kama NMB Financial Fitness.

Mpango huo utakaoenea nchi nzima, ulizinduliwa Mei 17, mwaka huu na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa aliyewakilishwa na Kaimu Kamishna wa Elimu, Martstella Wassena.

Kwa kuwa ni wa kihistoria na kipekee hapa nchini, NMB wakaona ni busara pia uzinduzi ufanyike katika shule ya sekondari iliyobeba historia ya kipekee. Hii si nyingine, bali ni Shule ya Sekondari Pugu.

Katika hotuba yake, Dk. Kawambwa alisema, “Shule hii ina historia kubwa hapa nchini Tanzania. Wengi tunaelewa kwamba viongozi wengi wa kitaifa na mashirika mbalimbali walipata elimu katika shule hii. Historia kubwa ya shule hii inatokana na ukweli kwamba Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, alifundisha katika shule hii, na kwa hiyo harakati za ukombozi wa nchi yetu zilianzia hapa.

“Mimi pia leo nimefurahi kupata fursa hii ya kuwa sehemu ya historia, kwa kusimama hapa kuwa mgeni rasmi wa tukio hilo lililoanzia hapa na kuenea nchi nzima.”

Dk. Kawambwa akasema msingi mkuu wa maendeleo ni uwezo na uelewa wa masuala ya kifedha, hasa kujiwekea akiba.

“Utunzaji na matumizi mazuri ya fedha si jambo ambalo mtu anazaliwa nalo, bali anafundishwa, hivyo basi mkakati wa kutoa elimu kuhusu masuala ya kifedha si tu unawajengea uwezo, bali pia utawawezesha kufanya uamuzi sahihi katika kutumia fedha,” alisema Dk. Kawambwa.

Amesema changamoto ya mikopo ya elimu ya juu ni kubwa kuliko uwezo wa Serikali, jambo linalofanya baadhi ya wanafunzi kukosa mikopo licha ya kuwa na vigezo.

Amesema maombi 113,356 yaliwasilishwa kwa mwaka 2011/2012. Kati ya hayo, waombaji wapya wa mwaka wa kwanza 38,541 walipata udahili kwa kuwa na vigezo, lakini wanafunzi 26,272 ndiyo waliopewa.

Amesema Serikali ilitenga Sh bilioni 317.8 kwa mikopo, lakini hadi Machi 15, mwaka huu kati ya walioomba, wanafunzi 94,092 wamekopeshwa na zaidi ya 19,264 wamekosa kwa sababu ya ufinyu wa bajeti.

Mwenyekiti wa Bodi ya NMB, Misheck Ngatunga, akizungumza katika hafla hiyo ya kihistoria, alisema benki hiyo iliainisha maeneo makuu matatu kwa ajili ya kuyaendeleza. Maeneo hayo ni elimu, afya na michezo.

“Kupitia sera hii, NMB imetenga asilimia moja ya pato lake baada ya kodi, kwa ajili ya kutekeleza miradi mbalimbali ya misaada kwa jamii kwa kila mkoa nchini Tanzania,” anasema.

Ngatunga anasema elimu ya fedha bado ni ya kiwango cha chini nchini Tanzania.

“Kutokana na ukweli huu uamuzi mkubwa unaofanywa kuhusiana na masuala ya kifedha, unakuwa hauna tija kutokana na wananchi kuwa na uelewa mdogo wa masuala ya fedha.

“Utafiti uliofanywa na Financial Sector Deepening Trust (FSDT) unaonyesha kuwa asilimia 10 tu ya Watanzania ndiyo wanaotumia huduma za kibenki, na moja ya sababu kubwa zinazoelezwa kuwa chanzo cha uwiano huu mdogo ni uelewa mdogo wa masuala ya kifedha.

“Kutokana na changamoto hii, NMB iliamua kufanya elimu kwa masuala ya kifedha kuwa sehemu mojawapo ya mikakati ya kusaidia jamii. Kwa kuanzia, tumeamua kujikita kutoa elimu kwa shule za msingi na sekondari. Hii inatokana na ukweli kuwa vijana ndiyo taifa letu la kesho. Hivyo NMB imeamua kulenga wanafunzi wa shule za msingi na sekondari katika awamu hii ya kwanza ya utekelezaji,” anasema.

Uzinduzi huo, kwa mujibu wa Ngatunga, unaambatana na uzinduzi wa jarida dogo lenye masomo ya masuala ya fedha ili kuwawezesha wanafunzi kujisomea na kuelewa shughuli za benki, kuweka pesa salama, matumizi mazuri ya fedha, mipango ya kutunza fedha, kukopa na kuweka akiba, na uwekezaji.

“Tunatarajia kusambaza vijarida 50,000 nchi nzima. Tunaamini kwamba elimu watakayoipata itasaidia familia zao, marafiki zao na jamii inayowazunguka,” anasema Ngatunga.

Mtendaji Mkuu wa NMB, Mark Wiessing, anasema katika kuhakikisha mpango huo unafanikiwa, matawi yote 142 ya NMB nchini kote yatatembelea shule tatu kwa ajili ya kuhamasisha. Benki hii ina mashine (ATM) 450 na wafanyakazi zaidi ya 2,600.

Wiessing anasema kati ya asilimia 30 hadi 40 ya Watanzania wote wenye akaunti, ni wateja wa NMB. Anasema idadi ndogo ya Watanzania wanaotumia huduma za kibenki inatokana na uelewa mdogo wa elimu ya masuala ya kifedha.

Ni kwa sababu hiyo, anasema kumekuwa na matatizo ya baadhi ya watu kupeana kadi na namba za siri za ATM.

“Mpango wetu umelenga kuwawezesha wasichana na wavulana kujua fedha ni nini, kutunza fedha kuna faida gani, kukopa (na kulipa), nini maana ya kuwekeza katika biashara au kujenga nyumba, na namna ya kutumia benki kwa ajili ya manufaa kimaisha.

“Tunataka watoto wawe na uwezo wa kufungua akaunti, wajue nini maana ya kadi ya ATM, kujua matumizi ya simu katika malipo mbalimbali, namna ya kutoa fedha katika ATM ya NMB bila kuwa na akaunti au kadi, umuhimu wa kutunza namba ya siri na kadhalika,” anasema.

Anasema ni kwa kutambua umuhimu huo, NMB itahakikisha kila tawi lake litatembelea shule mbili hadi tatu, mameneja watatembelea shule na shule zitatembelea matawi kujua masuala ya benki na fedha, NMB itasambaza vijarida zaidi ya 50,000 nchini kote na kila wiki kutatolewa katuni katika vyombo vya habari hapa nchini zikiwalenga kuwafundisha watoto.

Wiessing alitoa wito kwa jamii kujitokeza kusaidia elimu, akisema katika mataifa mengi bajeti ya shule za serikali inatokana na michango ya taasisi, wazazi na wasamaria wema.

Kwa kusherehekea uzinduzi wa NMB Financial Fitness katika Sekondari ya Pugu, Wiessing, kwa niaba ya benki hiyo, aliipatia msaada wa Sh milioni 20 kwa ajili ya masuala mbalimbali ya maendeleo shuleni hapo.

2829 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!