PAROKO wa Parokia ya Urumi, iliyoko Wilaya ya Kalambo mkoani Rukwa, Padri Peter Twamba, amewajia juu waamini wa Kanisa la Waadivetisti Wasabato, waliotuhumiwa kukashifu imani ya Kanisa Katoliki (RC).

Tukio hilo lilitokea kanisani hapo, Jumapili ya 23 ya mwaka ‘A’ (kijani) ya Septemba 7, mwaka huu saa 3 asubuhi mara baada ya misa ya asubuhi kanisani hapo.

Mmoja wa waamini aliyekuwako ndani ya kanisa hilo, alilithibitishia gazeti hili juu ya tukio hilo akisema: “Eeeh,bwana mambo yalikuwa ni kama sinema hivi.”

Akisimulia mkasa huo, muumini huyo alisema, “Mambo yalikuwa …hivi: Wasabato hao wako maeneo ya Urumi huku Kalambo wakitangaza madhehebu yao kwa wakazi wa eneo hilo ambao wengi ni waamini wa Kanisa Katoliki.”

Amesema kwamba wakiwa huko kwa takribani wiki nzima ya kuanzia Septemba Mosi, walikuwa wakibeza imani ya Kanisa Katoliki kwamba waamini wake wanaamini sanamu, huku wakibeza kofia ya Papa Francis wakiihusisha na shetani, sanjari na kumkashifu Bikira Maria.

Taarifa zinasema kwamba kazi ya Wasabato imekuwa ikifanyika kila jioni ya wiki hiyo wakitumia vipaza sauti na vifaa vingine vya kurushia matangazo.

Kuendelea kwao kukashifu imani ya Kanisa Katoliki, kuliwaudhi baadhi ya waamini ambao walishtushwa zaidi baada ya kuwaona baadhi wakijumuika katika ibada ya misa takatifu ya Jumapili.

Taarifa za chini chini zilienea ndani ya kanisa hilo hadi kumfikia Paroko aliyekuwa anaendesha misa hiyo. Mara baada ya misa hiyo, Paroko alizungumzia juu ya mihadhara hiyo na kuwapa moyo waamini kwamba wasipotoshwe.

Akaendelea kusema nasikia baadhi wako hapa ndani ambao na wamekuja kutaka kuendelea kutoa semina kwa Wakatoliki, mara baada ya misa wakilenga kuwaambia wasiende tena katika Kanisa Katoliki.

Wakati waamini wote wakiwa wameketi, Paroko Twamba akawataka Wasabato hao kusimama. Wakasimama na kusema wana neno la kuokoa, wanataka kulisema kwa waamini hao mbele ya Paroko.

Basi, Paroko huyo akawaita mbele ya kanisa hilo na kuhoji kulikoni wanatangaza madhehebu yao kwa kukashifu Kanisa Katoliki?

Wasabato hao walikaa kimya, ndipo Paroko huyo alipowachapa kila mmoja vibao viwili na wakati wakijiuliza na kutaka kukimbia, kiongozi wa kanisa akaamuru milango idhibitiwe.

Wasabato hao walidhibitiwa kisawasawa, kabla ya Paroko huyo kuagiza bakora, ambako aliamuru Wasabato hao kulala chini. Wakalala na kila mmoja akalambwa bakora tatu.

Baada ya bakora hizo, Paroko aliwachukua Wasabato hao hadi Kituo cha Polisi cha Mwimbi, akiwatuhumu kuvamia Kanisa Katoliki kabla ya viongozi wao wa Kisabato kwenda na kuomba radhi na ya kuyamaliza. Watuhumiwa hao wakaachiwa huru.

Kamanda wa Polisi Mkoa (RPC) Rukwa, hakupatikana kuzungumzia tukio hilo, ambalo lilimalizwa hapo polisi kabla ya kesi hiyo kuendelea mbele.

 

*****

 

Picha Na 1. Mkuu wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es Salaam (CBE), Prof. Emanuel Mjema, akitoa ufafanuzi kwa waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho miaka 50 ya chuo hicho yanayoendelea jijini Dar es Salaam. (Picha na Mpigapicha Wetu).

 

****

 

Maadili yaboresha ufaulu CBE

 

Na Aron Msigwa (MAELEZO)

 

Hatua iliyochukuliwa na uongozi wa Chuo cha Elimu ya Biashara Dar es Salaam (CBE) kusimamia maadili kwa wanafunzi, imezaa matunda baada kuongezeka kwa ufaulu wa masomo kwa wasomi chuoni hapo.

Hayo yalibainishwa wiki iliyopita jijini na Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Emanuel Mjema, alipozungumza na waandishi wa habari kuhusu maadhimisho ya kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwa chuo hicho.

Amesema suala la usimamizi wa maadili kwa wanafunzi na jamii nzima inayoingia chuoni hapo, limepewa kipaumbele kikubwa na uongozi wake tofauti na miaka iliyopita, hali inayokifanya chuo hicho kuwa mfano wa kuigwa na vyuo pamoja na taasisi nyingine za elimu ya juu hapa nchini.

“Chuo chetu sasa ni mfano wa kuigwa na vyuo vingine hapa nchini kwa sababu tumeweza kusimamia suala la maadili, hasa uzingatiaji wa mavazi yenye staha kwa wanafunzi, hali iliyoongeza heshima kwa chuo chetu,” alisema Prof. Mjema.

Mbali ya suala la usimamizi wa mavazi kwa wanafunzi, Prof. Mjema amesema chuo hicho kimeendelea kuhakikisha ulinzi na usalama kwa wanafunzi na jamii nzima inayoingia na kutoka katika mazingira ya chuo hicho, kuimarisha ukaguzi katika maeneo yote muhimu ya kuingilia wanafunzi na kuwatambua wanafunzi wote kwa kutumia vitambulisho vyao.

Amefafanua kuwa chuo hicho sasa kinafurahia matunda ya mafanikio ya kutimiza miaka 50 tangu kuanzishwa kwake, yakiwamo mabadiliko na maboresho makubwa katika sekta ya elimu hasa ongezeko la udahili wa wanafunzi, ongezeko la fani za masomo na kampasi za chuo hicho katika mikoa mingine nchini ikiwamo Dodoma, Mwanza, Mbeya na Zanzibar.

Prof. Mjema amefafanua kuwa CBE sasa inatimiza miaka 50 kikiwa chuo pekee Afrika Mashariki na katika nchi za Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) kinachotoa wanafunzi wa shahada ya vipimo.

“Chuo hiki pekee ndicho kinachotoa mafunzo kwa ngazi ya shahada ya vipimo, ni chuo kinachotegemewa sana katika ukanda huu wa nchi za Afrika Mashariki na SADC,” alisisitiza.

Ameeleza kuwa tangu kuanzishwa kwake Januari 1965 na aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, chuo hicho kimepata mafanikio makubwa kwa kuongeza idadi ya wanafunzi wanaodahiliwa kila mwaka kutoka wanafunzi 25 mwaka 1965 hadi 14,000 mwaka 2014.

Mafanikio mengine ni kuongezeka kwa kozi za masomo na ngazi za mafunzo hadi kufikia shahada, kuongezeka kwa wakufunzi wenye shahada za uzamivu (PhD) chuoni hapo,  pamoja na chuo kuanzisha ushirikiano wa elimu na vyuo vikuu vingine nje ya nchi kikiwamo Chuo Kikuu cha Eastern Finland katika utoaji wa mafunzo ya shahada za uzamivu kwa kutumia TEKNOHAMA kwa nchi za SADC.

Ameongeza kuwa katika  kipindi cha miaka 50 ya chuo hicho, idadi ya kampasi imeongezeka kutoka moja ya jijini Dar es Salaam na kufikia nne katika mikoa ya Mbeya, Mwanza, Dodoma na upande wa Zanzibar huku idadi ya wahitimu wa chuo hicho ikiongezeka kwa kipindi chote ikiwa zaidi ya wanafunzi laki moja.

Aidha, katika kuhakikisha chuo hicho kinaendelea kuimarisha ubora wa elimu inayotolewa kwa wanafunzi katika maadhimisho hayo, chuo kinaandaa matukio mbalimbali ya ukusanyaji wa fedha kupitia chakula cha hisani, matembezi, midahalo ya wasomi na mikutano ya wanafunzi wahitimu wa chuo hicho Zanzibar, Dodoma, Mwanza, Mbeya na Dar es Salaam kwa ajili ya ujenzi wa maabara, vyumba vya mihadhara ya wanafunzi na  madarasa.

Pia chuo hicho kinaandaa mafunzo ya ujasiriamali yatakayotolewa kwa jamii ikiwa ni sehemu ya kurudisha huduma kwa jamii kwa kuwajengea uwezo wajasiriamali, na kuwajengea uelewa wanafunzi ili waweze kuwa na uchaguzi sahihi wa hatima yao ya baadaye wanapohitimu mafunzo.

By Jamhuri