Hatari ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kuendelea kupoteza wanachama wazito katika kipindi cha kuelekea uchaguzi mkuu inazidi kukinyemelea chama hicho, uchunguzi wa gazeti la JAMHURI umebaini.

Habari kutoka ndani ya Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), zinaonyesha kuna wimbi kubwa la viongozi mahiri wa CCM, watajiunga na vyama vya upinzani ndani ya wiki hii.

Kaimu Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Salum Mwalimu, ameliambia JAMHURI kuwa mipango thabiti imewekwa na CHADEMA na washirika wengine wa Ukawa, kuwapokea viongozi wazito kutoka CCM.

Anasema vigogo hao watatambulishwa kwa mtindo wa kushtua kama ilivyotokea kwa Waziri Mkuu wa zamani, Frederick Sumaye aliyejiunga na Ukawa Jumamosi iliyopita.

Wanachama wanaowachukua huzungumza nao na kuwapa sera zao kabla ya kuwatangaza na hivyo sasa wapo kwenye mjadala mzito na viongozi hao, anasema.

“Usajili tunaofanya, hatufanyi usajili wa kufurahisha umma wa Watanzania. Tunachukua wanachama hawa, tunawapokea huku upinzani kwa sababu ya maandalizi ya kuchukua dola. Tumejiandaa.

“Ni ukweli kuwa kuna viongozi mahiri wa CCM, wanakuja hapa,” anasema Mwalimu.

Amesema kwamba viongozi wanakwenda Ukawa kwa sababu ya maandalizi ya kuunda Serikali kwani kuna kila dalili ya kushinda uchaguzi unaotarajiwa kufanyika Oktoba 25, mwaka huu.

Ingawa Mwalimu aligoma kutaja vigogo hao, Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba duru zinaonyesha ni mmoja kati ya wanaonyemelewa.

“Si unaona, CCM walipofahamu upepo wa Jaji Warioba wakaamua kumpandisha jukwaani harakaharaka amnadi Magufuli… Ninachojua huyu mzee ana makovu na uchungu mkubwa. Anafahamu sasa kuwa Rais Jakaya Kikwete anataka kumtumia.

“Pamoja na kwamba amepanda jukwaani, subiri uone mshituko wa mwaka atakaowapiga. Ukawa mwaka huu ni moto wa kuotea mbali,” kilisema chanzo chetu. Hata hivyo, mmoja wa wasaidizi wa Jaji Warioba alisema hajalisikia hilo na hadhani kama litatokea. Jaji Warioba hakupatikana kuzungumzia taarifa hizi zilizotoka kwa vyanzo zaidi ya vitano.

Ukiacha Jaji Warioba, duru za siasa zinaonyesha kuwa Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal naye yumo kwenye orodha inayosubiriwa UKAWA. Ingawa yeye amekwishakanusha taarifa hizi, wanasema huenda alifanya hivyo kwa kuwa zilivuja kabla ya muda mwafaka.

“Si hata Mhe Sumaye naye alikanusha kama Dk. Bilal taarifa hizi zilipovuja haraka? Wala Watanzania wasipate shida. Wakati ukifika hili kama Mungu amelipanga watashuhudia wenyewe. Mipango ipo ya kumnasa kigogo huyu na siwezi kusema zaidi,” kilisema chanzo chetu.

JAMHURI limezungumza na Mwandishi wa Makamu wa Rais, Boniface Makene aliyesema: “Kwa asili ya siasa za Zanzibar lazima ujue maana ya ASP na vyama vingine. Waliokuwa ASP ndio wako CCM na wala hawawaamini wa CUF na waliopo CUF, ni wale waliokuwa wa vyama vingine na wala hawawaamini wa CCM. Kwa kulifahamu hilo, Dk. Bilal hawezi kuhama,” alisema Makene.

Hata hivyo, Makene alikataa kuzungumzia suala la kwa nini Dk. Bilal alinyimwa nafasi ya kuzungumza katika mkutano wa CCM Dodoma uliofanya uteuzi Julai 12, na wiki iliyopita akanyimwa tena nafasi wakati Magufuli anazindua kampenzi zake.

Chanzo kilichofikisha taarifa hizi kwa JAMHURI kilisema: “Dk. Bilal amenyimwa kuzungumza Mkutano Mkuu Dodoma, na leo (Juampili) amenyimwa. Hilo linatutia simanzi sisi tulio karibu naye. Linatufanya tuamini kuwa kuna jambo na limeandaliwa makusudi.

“Leo (Jumapili iliyopita) ilikuwa nafasi ya Dk. Bilal kupata fursa ya kukanusha kuwa ahami CCM kwa kuthibitisha kuwa yupo. Kwa kumnyima nafasi, wamethibitisha yanayosemwa na inaelekea hata CCM haimwamini,” alisema mtoa habari wetu.

Kwa upande mwingine, watu waliopo karibu na Waziri Mkuu, Mizengo Pinda wanasema hadi sasa ana masikitiko ya mwaka. Wanasema Rais Kikwete alimwaminisha kuwa angempitisha kugombea urais na akamshauri achukue fomu huku akijua kuwa hamwambii ukweli.

“Hata leo (Jumapili iliyopita) ingawa alikuwa na shughuli nyingine hakuwapo kwenye uzinduzi wa kampeni, lakini inaaminiwa kuwa hata hasira zilichanganyika na kuzaa sura tuliyoiona. Aanapewa nafasi Warioba asiye na cheo chochote serikalini wanaachwa Makamu wa Rais na Waziri Mkuu wasizungumze? Kuna nini?” kilihoji chanzo chetu.

Kwa upande wake, Kaimu Katibu Mkuu Mwalimu alikiri kuwako kwa mazungumzo na baadhi ya viongozi, yanayoratibiwa kwa siri ingawa miongoni mwa viongozi wanaotajwa baadhi walijitokeza juzi kwenye kampeni za CCM hivyo kuzua maswali.

Lakini mtoa habari anayeratibu mazungumzo hayo, aliliambia JAMHURI kuwa, “CCM walimteka Mzee [Warioba] na walimtaka mara moja apande jukwaani, lakini nguvu yao ya kuzuia viongozi hao ni ndogo,” anasema.

Wakili wa kujitegemea, Mohammed Tibanyendera, ambaye Jumamosi (siku Sumaye alipojiunga Ukawa) alikuwa mshereheshaji anasema, “kwa namna hali ilivyo, Tanzania inakuja kuzaliwa upya.”

Tibanyendera ambaye ni Kada wa NCCR-Mageuzi aliongeza: “Ukawa inazidi kuwa imara na itakuwa imara zaidi.”

Jumamosi iliyopita Sumaye alitangaza kukihama CCM na kujiunga na Ukawa ikiwa ni siku chache tu, baaada ya kuibuka uvumi kuwa angehama.

Sumaye anakuwa Waziri Mkuu mstaafu wa pili kujiondoa CCM katika historia ya Tanzania, ambapo waziri mkuu wa kwanza kuhama CCM alikuwa Edward Lowassa aliyejiunga Chadema Julai 28, mwaka huu.

Sumaye ambaye hakutangaza chama ambacho atajiunga nacho, baadae ilithibitika kuwa anakwenda NCCR-Mageuzi.

Vyama vinavyounda Ukawa ni Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), Chama cha NCCR-Mageuzi na Chama cha National League for Democracy (NLD).

Sumaye anasema sababu kuu ya yeye  kujiunga na upinzani ni kulinda maslahi mapana ya nchi na Watanzania hasa suala la amani na maendeleo.

“Siingii kwa sababu ya maslahi yangu binafsi nipo tayari kuwasaidia ili muwe na nguvu, siingii kwa sababu Lowassa anatoka Kaskazini,” anasema.

Anasema kukithiri kwa rushwa ndani ya CCM na kuvurugwa kwa mchakato wa uchaguzi kumechangia wananchi kukata tamaa hali iliyochochea upinzani kuungwa mkono kila unapokuja uchaguzi mkuu.

“Kwa mwaka huu 2015, naona kuna kazi kubwa. Nasema tena itakuwa ni ngumu kuzuia wimbi la mabadiliko. Ukawa watashinda uchaguzi huu.

“Wapo wanaosema kiongozi hawezi kutoka Kaskazini, binafsi nazipiga vita sana siasa za ukanda na udini ni sumu kwangu  na niliwahi kuzikemea mara kadhaa baada ya baadhi ya watu fulani kusema kiongozi wa nchi hawezi kutoka eneo fulani.

“Sisemi watu walioko upinzani ni mbumbumbu, la hasha! Kuna wasomi wazuri lakini hawana ujuzi wa kuendesha nchi, hivyo nimeingia kusaidia ili mambo yaende kwa spidi.

“Sitoki kwamba labda nimekasirika kwa vile sikuteuliwa kugombea urais kupitia CCM, sitoki CCM labda nina tatizo na mgombea wake, Dk. John Magufuli, sitoki labda nina sababu na uongozi wa juu wa CCM na wala kukidhoofisha badala yake nakiimarisha…

“Sijiungi na upinzani labda kwa sababu ya maslahi yoyote ya cheo au fedha, sijahaidiwa cheo chochote wala kupewa fedha zozote, mimi sihongeki wala sinunuliwi,” anasema.

Anasema kwamba kwa upande wake, alijitosa kuwania urais ndani ya CCM kwa lengo la kuleta mabadiliko ambayo ameyayataja kuwa ni kurekebisha sura ya utawala – siasa iwe mbali na utumishi, lakini imeshindikana hivyo ana imani kwa Ukawa itawezekana.

Kujiunga kwa viongozi hao Ukawa kumesababisha mtikisiko ndani ya CCM ambako baadhi ya wasomi wameshutumu mwenendo wa viongozi wa chama tawala kuendelea kuwatukana kwa kuwaita wanaohama makapi na oil chafu.

Wasomi na wanasiasa, wamefuatilia uzinduzi wa kampeni za CCM na kuibuka na masikitiko makubwa kutokana na lugha ya matusi zilizotumiwa na viongozi wa chama hicho.

Kauli za kashfa na kubeza zinazotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, zimepata upinzani mkali.

Mmoja wa vigogo wa Serikali ambaye amethibitisha kwamba amelelewa kutoka Youth League hadi Jumuiya ya Umoja wa Vijana (UVCCM), amesema, “Kauli za Nape na Mkapa  zinaua chama.”

Kiongozi huyo alikwenda mbali zaidi akisema kwamba hata matusi aliyotoa Rais mstaafu wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa kwamba wanaodai kuleta ukombozi ni “wapumbavu” haijengi chama zaidi ya kukibomoa.

Kauli ambazo kigogo huyo alisema zinaua chama ni zilizotolewa na Nape kuwa CCM itashinda kwa “bao la mkono”; “wanaohama CCM ni makapi”; na “waliohama ni oil chafu”.

Mkapa ametakiwa kuomba radhi kwa kutumia lugha ya matusi kwenye kampeni kwani aliowatusi kuwa ni wapumbavu tafsiri yake ni kuwa hata Sumaye aliyekuwa Waziri Mkuu wake kwa miaka 10 amemweka katika kundi la wapumbavu. Sumaye amekuwa Waziri Mkuu tangu mwaka 1995 hadi 2005.

Mkapa alisema kwamba wanachama wanaodai kuwa wanakwenda kuleta ukombozi wa Tanzania nje ya CCM ni wapumbavu kwani nchi ilikwisha kukombolewa na vyama vya TANU na ASP vilivyozaa CCM mwaka 1977.

Mkapa alisema; “Kuna chama cha ukombozi kimoja katika nchi hii. CCM ni CCM iliyozaliwa na ASP na TANU, vyama vya ukombozi kwa Bara na Visiwani. Wazazi wakombozi wanazaa mtoto mkombozi…

“Nenda nchi za jirani na uliza watakwambia chama cha ukombozi ni CCM. Ndiyo maana nina kila sababu ya kuwaita wapumbavu na malofa.”

Rais Jakaya Kikwete alisema, “Nitakabidhi kijiti kwa John Pombe Magufuli kwa sababu tulipomchagua Magufuli hatukubahatisha… Nataka Rais anayependa nchi na anayependa wananchi wa nchi hii. Magufuli ana sifa hizo.”

Magufuli kwa upande wake alijikita katika kutangaza sera za chama chake kueleza iwapo atachaguliwa atalifanyia nini taifa. Alisema anajua kiu ya mabadiliko kwa Watanzania na Watanzania wanataka kitabu kipya.

“Nawahakikishia shida na matarajio yenu nayajua na ninayafahamu. Natambua nina uwezo wa kuyashughulikia. Nimetambua Watanzania mnataka amani, usalama, umoja wa kitaifa. Penye umoja na amani, mtaleta mabadiliko ya kweli,” alisema.

Amani, usalama na umoja wa kitaifa ni msingi wa maendeleo ya kweli, alisisitiza. Wizi, ubadhilifu, rushwa ameahidi kuvikomesha haraka, huku akiahidi kuanzisha Mahakama ya Rushwa. Ametoa mfano wa hospitali mgonjwa kuandikiwa cheti hospitalini na kuambiwa akanunue dawa kwenye duka jirani na akahoji hilo duka limepataje dawa na hospitali ikazikosa?

Amegusia elimu, mikopo ya wanafunzi, ajira kwa vijana, wakulima kupata miliki ya ardhi, pembejeo, mbegu za gharama nafuu, masoko ya uhakika na bei nzuri za mazao. Akasema wakulima kukopesha serikali hili halitatokea wakati wa serikali yake.

Umoja wa kitaifa, Muungano wa Tanzania, ulinzi na usalama wa nchi, kuhesimu mihili, kwamba Bunge litafanya kazi bila kuingiliwa na Mahakama hataiingilia. Ataimarisha utawala bora, uhuru wa kuabudu, uhuru wa vyombo vya habari, ataheshimu mawazo ya vyama vingine yenye lengo la kujenga nchi na atajenga viwanda vingi.

Baadhi ya watu waliozungumza na JAMHURI kwa sharti la kutotajwa walihoji Magufuli atapata wapi fedha za kujenga viwanda na miradi yote aliyoitaja kwani katika hotuba yake hakupambanua vyanzo vya mapato.

“Hofu yangu ni kuwa atazipata wapi hizo fedha za kujenga viwanda? Anapaswa kufafanua si kuja na hotuba za hadaa hapa. Watanzania hatutaki nyimbo tena tunataka vitendo,” alisema mtoa habari wetu na kuungwa mkono na wenzake watano aliokuwa nao.

Aliyekuwa Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Shinyanga, Khamis Mgeja amesema kilichofanywa na Rais Mkapa si uungwana hasa kwa viongozi ambao alipata kuwaamini na kuwapa madaraka mazito.

“Mkapa aombe radhi,” anasema Mgeja na kuungwa mkono na aliyepata kuwa Mbunge wa Arumeru Mashariki, Goodluck ole Medeye na Mwenyekiti wa zamani wa CCM Mkoa wa Dar es Salaam, John Guninita.

“Ukiona watu wanaanza kutukana ujue wameishiwa sera,” anasema Medeye wakati Guninita anasema, “Sikutegemea Mheshimiwa Mkapa angefanya hivyo, ndiyo maana wakati anaongoza nchi na chama nilikihama. Nina shaka na busara zake.”

Viongozi hao pamoja na Mwenyekiti wa CCM Singida, Mgana Msindai – aliyekuwa pia Mwenyekiti wa wenyeviti wote wa CCM walihama kutoka CCM na kujiunga Chadema kupinga mchakato wa uteuzi ndani ya chama hicho.

By Jamhuri