Klabu ya ‘Kibibi Kizee cha Turin’ Juventus imo kwenye hatua za mwisho kumrudisha kiungo wake wa zamani, Paul Pogba.

Mchezaji huyo kwa sasa anacheza katika Klabu ya Manchester United. Mipango ya mabingwa hao wa Italia inaanza Januari mwakani.

Pogba amekuwa kwenye mkakati wa kuondoka Manchester United kutokana na mtifuano uliopo kati yake na Kocha wake, Jose Mourinho.

Kwa sasa uongozi wa Manchester United umemzuia Pogba kuzungumzia matatizo ya Mourinho na uwezekano wake wa kuondoka Old Trafford.

Iwapo uongozi wa Manchester utamwachia Pogba aondoke, hiyo itakuwa na maana kwamba Kocha Mourinho na Ofisa Mtendaji Mkuu, Ed Woodward, wameshindwa kumshawishi kiungo huyo kubaki katika Ligi Kuu ya Uingereza.

Ni jukumu lao kufanya kila linalowezekana kusalia naye, ingawa hatua hiyo inaweza kumaanisha kwamba wadhifa wa Mourinho hauna nguvu tena baada ya kuzuiwa kununua wachezaji wapya aliowataka msimu uliopita.

Iwapo Juventus hawatamchukua mapema kiungo huyo, Barcelona inaweza kubahatika kumpata kutokana nayo kuonyesha nia ya kuhitaji huduma yake.

Inaelezwa kuwa Pogba anaweza kuwa haelewani na mtu aliyechukua jukumu la kulipa dau lililovunja rekodi ya pauni milioni 89 kumsaini kutoka Juventus. Huu ni wakati muhimu kwa Manchester United kujitafakari.

Septemba mwaka huu Kocha Mourinho alieleza kuwa hana tatizo na kiungo wa kati wa Man United, Pogba, licha ya kumwambia mchezaji huyo kwamba hawezi tena kuwa nahodha wa klabu hiyo.

Mourinho alimwambia Pogba kwamba si nahodha wa klabu hiyo kutokana na wasiwasi kuhusu tabia yake. Alisema alichukua uamuzi wa kumwondolea kitambaa cha unahodha kwani yeye ndiye mwenye mamlaka ya kufanya uamuzi huo.

Alinukuliwa na chombo kimoja cha habari akisema: “Hakuna tofauti zozote kati yetu, ni uamuzi tu ambao si lazima nieleze.”

Pogba aliambiwa kuhusu uamuzi huo kabla ya mechi ya Kombe la Carabao dhidi ya Derby.

Mourinho amejaribu kuonyesha uzito wake baada ya kosa la Pogba kuisaidia timu ya Wolves kufunga bao la kusawazisha katika Uwanja wa Old Trafford mbali na mchezaji huyo kukosoa mbinu zinazotumika.

Pogba amekuwa akiyapuuza matamshi ya Mourinho. Katika ripoti yake dhidi ya Derby iliyoshinda kwa njia ya penalti, Mourinho alisema kuwa hafurahishwi na baadhi ya wachezaji wake.

“Mechi dhidi ya Wolves ilikuwa funzo zuri, funzo ambalo ninarejelea kila wiki, funzo ambalo baadhi ya wachezaji hawajifunzi. Kila timu inayocheza dhidi ya United hucheza kufa – kupona, na tunahitaji kuimarika ili kukabiliana nazo, asilimia 95 haitoshi iwapo wengine wanatoa asilimia 101.

Mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa, Pogba, ambaye alitajwa katika kikosi dhidi ya Derby, alitazama mchezo kutoka eneo la mashabiki huku Ashley Young akiwa nahodha wa kikosi hicho.

Antonio Valencia ndiye nahodha wa klabu hiyo.

Kabla ya mechi hiyo Mourinho alinukuliwa akisema: “Wamepumzishwa. Nilimpumzisha Luke Shaw, Paul, Victor Lindelof, Antonio Valencia na David de Gea, lazima nicheze na kikosi kizuri.”

Kufuatia sare ya 1-1, Pogba alisema kwamba alitamani timu hiyo kushambulia mara kwa mara kwani walikuwa wakicheza katika Uwanja wa nyumbani wa Old Trafford. “Tuko nyumbani na tunafaa kucheza vizuri zaidi. Tuko hapa kushambulia, tunapocheza hivyo ni rahisi kwetu sisi.”

Pogba alijiunga tena na Manchester United kutoka Juventus kwa dau lililovunja rekodi mwaka 2016, alikuwa akiachwa nje msimu uliopita na kusema kwamba hafurahii kuendelea kubaki Old Trafford.

By Jamhuri