Rais Dk. John Magufuli, amekutana na kuwaambia wachezaji wa timu ya taifa ya soka (Taifa Stars) kwamba hafurahishwi na matokeo ya timu hiyo, hasa katika kampeni ya kufuzu kucheza fainali za mashindano ya Bara la Afrika (AFCON) mwaka 2019 nchini Cameroon.

Rais Magufuli alikutana na wachezaji wa timu ya taifa Ikulu, jijini Dar es Salaam baada ya ushindi wa Taifa Stars dhidi ya Cape Verde katika mchuano muhimu wa hatua ya makundi ili kufuzu kucheza fainali hizo. Mchezo huo ulichezwa wiki iliyopita.

“Napenda sana michezo, lakini mimi si shabiki wa timu yoyote hapa Tanzania…sipendi kushindwa, na ni aibu sana watu milioni 55 kushindwa kupata Kombe la Afrika,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli amewaambia wachezaji wa Taifa Stars kuwa wameanza kurejesha matumaini baada ya ushindi wa nyumbani na kuahidi kuwapa Shilingi milioni 50 ili kufanikisha maandalizi ya kambi ya timu ya taifa.

“Mlipofungwa mabao 3-0 nilikata tamaa, na mlipofunga mabao mawili sikufurahi, kwa sababu bado mnadaiwa bao moja…bado hamjashinda, bado,” amesema Rais Magufuli.

Rais Magufuli baada ya kuwakabidhi viongozi wa Taifa Stars kiasi cha fedha alichokuwa ameahidi, alitumia muda huo kuwatahadharisha kutozitumia fedha hizo kinyume cha malengo yaliyokusudiwa.

Fedha zilizotolewa na Rais Magufuli zimepeleka ujumbe kwa viongozi wa Shirikisho la Soka nchini (TFF) pamoja na vyama vya michezo kuwa serikali imetia rasmi mguu katika vyama hivyo kwenye juhudi za mapambano dhidi ya ufisadi kwenye vyama vya michezo.

Katika mazungumzo yake na wachezaji pamoja na viongozi wa TFF, rais aliwaambia viongozi hao kuwa ametoa fedha hizo kwa ajili ya kusaidia maandalizi ya Taifa Stars kwenye mechi ijayo ya kufuzu kucheza Fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika dhidi ya Lesotho.

Rais Magufuli amesema hataki kusikia fedha hizo zinatafunwa na watu ambao hawaingii uwanjani, badala yake zitumike kwa maandalizi na akawaonya viongozi wanaopenda kutumia mwanya wa timu kutafuna fedha.

“Wakati ninaingia madarakani nilikuta kuna viongozi kwenye sekta ya michezo wamekuwa majizi, wengine ni katika ngazi ya klabu, nikasema hawa washughulikiwe. Sitaki kuzungumza sana hili kwa sababu wengine tayari wapo mahakamani wameshtakiwa,” amesema.

Amewaambia wachezaji na viongozi kwamba miaka ya hivi karibuni viongozi wengi wa michezo wamekuwa majizi, ndiyo sababu hata Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) likaikatia Tanzania mgawo wa fedha za msaada ambazo hutolewa kwa nchi mbalimbali kusaidia maendeleo ya soka kiasi cha dola za Marekani milioni tatu, ambazo ni zaidi ya Sh bilioni 6.5.

Taifa Stars ilipata ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Cape Verde wiki iliyopita na kujiweka katika nafasi nzuri ya kufuzu kucheza fainali hizo.

Tanzania ni ya pili katika kundi ‘L’, ikiwa na alama tano baada ya kushinda mechi moja na kutoka sare michezo miwili. Kundi hili linaongozwa na Uganda ambayo ina alama 10.

Kufuzu kucheza fainali hizo, Taifa Stars inahitaji kushinda mechi ijayo dhidi ya Lesotho jijini Maseru, ikisubiri mechi ya mwisho mwezi Machi, 2019.

Mara ya mwisho Tanzania kufuzu kucheza fainali hizo (AFCON) ni mwaka 1980 nchini Nigeria.

Please follow and like us:
Pin Share