Mshambuliaji wa timu ya taifa ya Tanzania (Taifa Stars), Mbwana Ally Samatta, amekuwa lulu kwa klabu tatu za nchini Uingereza. Samatta yuko mguu sawa akisubiri Everton wazidi ‘kujikoki’.

Tetesi zinasema nyota huyo anasakwa na West Ham United – ‘Wagonga Nyundo wa London’ , Everton na Burnley. Samatta, 25, maarufu kama ‘Samagoal’ nyota yake imeng’aa sana akichezea Klabu ya KRC Genk, inayoshiriki ligi kuu nchini Ubelgiji.

Ameifungia klabu yake mabao 11 katika mechi 16 ambazo ameichezea msimu huu, nusu ya mabao hayo akiyafunga katika mashindano ya barani Ulaya. 

Taarifa za kumhusisha Samatta na Klabu ya Everton zimetoka kwenye mtandao wa hitc.com, moja ya mitandao maarufu kwa taarifa za wachezaji na kuhama kwao. Samatta amepata nafasi ya kucheza hatua ya makundi katika ligi ndogo ya klabu Ulaya, maarufu kama Europa League. 

 

Hii ni baada ya Klabu yake ya KRC Genk ya Ubelgiji kupata ushindi wa jumla wa 4-2 katika mechi ya kufuzu hatua ya makundi dhidi ya wapinzani wao Lokomotiva Zagreb ya Croatia.

Genk walipata ushindi wa 2-0 mechi iliyochezwa Alhamisi jioni. Klabu hizo mbili zilitoka sare 2-2 mechi ya mkondo wa kwanza.

Samatta aliifungia klabu yake bao la kwanza dakika ya pili huku Leon Bailey akifunga la pili muda mfupi baada ya mapumziko. Samatta pia alionyeshwa kadi ya njano dakika ya 69.

 

Samatta mwenye umri wa miaka 25, ambaye kwa sasa ni mshambuliaji tegemeo wa Klabu ya KRC Genk, anatajwa kuwa kijana mwenye ushawishi mkubwa nchini Tanzania kulingana na kura ya maoni iliyofanywa na chombo cha habari cha Avance Media.

Mwaka 2016 alishinda tuzo ya mchezaji bora wa Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF), miongoni mwa wachezaji wanaosakata kandanda barani Afrika, baada ya kuisaidia timu yake ya TP Mazembe kushinda Kombe la Klabu Bingwa Afrika.

 

Kwa nini anahusishwa na Everton?

Samatta, mwenye kimo cha futi 5 inchi 11, amefunga mabao sita katika ligi ndogo ya klabu barani Ulaya, Europa League, hivyo kuushangaza ulimwengu wa soka, kisha kuzivutia klabu za England.

Agosti 23, mwaka huu, Samatta alifunga ‘hat-trick’ dhidi ya Brøndby IF katika Europa League, kwenye mechi ambayo walishinda 5-2.

Everton wametatizika kumpata mshambuliaji wa kutegemewa tangu nyota wao, Romelu Lukaku, alipowaacha na kuhamia Manchester United kwa paundi milioni 75 mwaka 2017.

Everton wanakabiliwa na ukame wa mabao msimu huu na zaidi wamesaidiwa na mawinga au viungo wa kati badala ya washambuliaji wao ambao wanaonekana kuwa butu.

 

Samatta ndiye anayeonekana kuwa suluhisho kwenye idara ya ushambuliaji na Everton inamhitaji zaidi kwa sasa kutokana na ustadi wake wa kutikisa nyavu.

Pia klabu nyingine za Ligi Kuu ya England – West Ham United, Burnley na Brighton zinaelezwa kumfuatilia kwa karibu Mbwana Samatta.

Gazeti la Daily Mirror liliripoti kwamba West Ham wanamfuatilia mchezaji huyo ingawa walisema Everton wanaonekana kuwa na uzito zaidi wa kumtafuta, ikizingatiwa kwamba Niasse anatarajiwa kuuzwa Januari.

Everton tayari wana uhusiano na Afrika Mashariki kupitia mdhamini wao, SportPesa, na waliibuka kuwa klabu ya kwanza ya Ligi Kuu ya England kuchezea Afrika Mashariki walipocheza dhidi ya mabingwa wa Ligi Kuu ya Kenya, Gor Mahia, katika Kombe la SportPesa Super Cup mwaka jana.

 

Watakuwa pia klabu ya kwanza ya England kuwa mwenyeji wa klabu ya soka ya Afrika Mashariki watakapowakaribisha nyumbani Gor Mahia uwanjani Goodison Park mwezi ujao.

Samatta alijiunga na Genk akitokea TP Mazembe Januari 2016, ambapo alitia saini mkataba wa kumuweka katika klabu hiyo hadi msimu wa 2019/20.

Amesaliwa na miezi 20 kabla ya mkataba wake kumalizika.

 

Samatta alihamia Ubelgiji mwaka mmoja baada ya kutawazwa mchezaji bora wa mwaka Mwafrika aliyekuwa anacheza ligi za barani Afrika mwaka 2015.

Alishinda vikombe sita akiwa na TP Mazembe, ikiwa ni pamoja na kushinda Ligi ya Klabu Bingwa Afrika mwaka 2015 kabla ya kuondoka.

Tangu mwaka 2011, Samatta ameichezea timu ya taifa ya Tanzania mechi 46 na kuifungia mabao 16.

Samatta alikuwa miongoni mwa wachezaji wa Klabu ya Simba kabla ya kujiunga na TP Mazembe mwaka 2011.

Please follow and like us:
Pin Share