Na Moshy Kiyungi

 

Mwanamuziki, Noel Ngiama Makanda ‘Werrason’, aliamua kuikacha bendi yake ya Wenge Musica BCBG, akaamua kuunda kikosi chake cha Wenge Musica Maison Mere.

Amejizolea sifa lukuki kufuatia ubunifu alionao na tabia yake ya ukuzaji wa vipaji pamoja na kasuka kikosi cha vijana chipukizi.

Werrason alizaliwa Desemba 25, 1965 katika mji wa Kikwit,  Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Alitanguliwa kwa kuzaliwa na nduguze wengine akiwemo wa kwanza, Mbese Jonas, anayeishi nchini Canada;  wa pili ni Mchungaji Patrice Ngoy Musoko, aliyepo jijini Kinshasa.

Mdogo wake wa mwisho ni Guy Nkoyi, anayeishi Paris, Ufaransa.

Alianza kujifunza muziki akiwa na umri wa miaka 12, akiwa mmoja wa wanakwaya wa kanisa (CBZO) mjini Kikwit.

Nguli huyo anacho kipaji kingine cha uchezaji wa karate. Amewahi kuwa mshindi kwenye shindano la karate, ndipo alipachikwa jina la Tarzan, jina Tarzan likabadilishwa likawa ‘Le roi de la Foret’ au kwa lugha ya Kiswahili – Mfalme wa Msitu.

Werrason ni mmoja kati ya watu wachache ambao huchukuliwa  kama waasisi wa kundi la Celio Star mwaka 1979.

Kundi hilo ambalo baadaye mwaka 1981 lilibadilishwa jina na kuitwa Wenge Musica, likiwa na makao yake katika Manispaa ya Bandalungwa, a.k.a Bandal, jijini Kinshasa, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

 Baadhi ya waasisi wa kundi hilo la Celio Star ni Aime Bwanga, Didier Masela,  Papy Sanji, Machiro Kifaya, Kidja Brow na Jean Belis Luvutula.  Werrason aliwahi kueleza kwamba kabla ya kuwa mwimbaji mahiri, alikuwa mpiga ngoma.

Werrason alichangia kwa kiasi kikubwa ilipotolewa albamu yao ya kwanza ya kundi lao ya Wenge Musica ‘Bouger Bouger’ ya  mwaka 1998.

Albamu hiyo ilisaidia kundi lao kufahamika zaidi.

Safu ya waimbaji alikuwepo JB Mpiana, Ngiama Werrason, Ricoco Bulambemba, Blaise Bula, Adolph Dominguez, Alain  na Mpela.    

Werrason ndiye aliyeshikilia wadhifa wa ukurugenzi, aliyehusika na masuala ya fedha kwenye kundi hilo la Wenge Musica.

Pamoja na sifa lukuki iliyokuwa imetwaliwa na vijana hao wa Wenge Musica Original, mwaka 1997 liligawanyika. Werrason akaunda kundi lake la Wenge Musica Maison Mere.

Aliimarisha kundi hilo kwa kuwachukua wanamuziki mahiri kina Didier Masela, Adolph Dominguez na Ferre Gola.

Werrason ana sifa moja kuu ya ukuzaji wa vipaji. Alisuka kikosi cha vijana chipukizi, wakiongozwa na kijana machachari  Ferre Gola, aliyewaunganisha vijana wengine katika kikosi hicho cha Wenge Maison Mere; Adjani Adjedje, Didier Lacoste, JDT Mulopwe, Serge Mabiala, Baby Ndombe, Bill Clinton na Celeo Scram.

Mwaka 1998, Werrason na kundi lake walitoa albamu yao ya kwanza iliyoitwa ‘Force Intervention Dapide’, ikiwa na wimbo ulioshika chati wa ‘Chantal Switzerland’.

Wimbo huo uliteuliwa kama wimbo bora wa mwaka na waandishi wa habari jijini Kinshasa. Mwaka 1999, Wenge Maison Mere wakatoka na albamu ya ‘Solola Bien’, iliyopewa tuzo ya ‘Gold disc’ mwaka 2002 kwenye onyesho la Zenith de Paris.

Ngiama Kanda Werrason akawa mwanamuziki wa pili wa Kiafrika kutumbuiza kwenye Ukumbi maarufu wa Bercy, uliopo katika Jiji la Paris Septemba 16, 2000 akitanguliwa na Koffi Olomide.

Werrason akaingia kwenye historia ya Jiji la Paris, akawa mwanamuziki wa kwanza wa Kiafrika kutumbuiza kwa siku mbili zilizofuatana kwenye Ukumbi wa Zenith jijini Paris.

Ilikuwa Aprili 26 na 27, 2002 ambako alipachikwa jina la ‘L’ Homme’ au ‘Deux Babords’, ikimaanisha mtu aliyejaza Ukumbi wa Zenith kwa siku mbili mfululizo wakati huo wa dansi.

Baadhi ya nyimbo zake zilizotia fora wakati huo ni pamoja na; ‘Surprise Kapangala’, ‘Telephone’, ‘Siya’, ‘Likambo’, ‘Dine Nzau’ na ‘Ekota’.

0713331200. 

Please follow and like us:
Pin Share