Wiki iliyopita nilihitimisha makala hii kwa aya iliyosema; Pamoja na Rais Kenyatta kushinikizwa amkamate (Raila Odinga) kwa uhaini, alimtafuta kwa faragha na kuunda naye ushirika ambao unaonekana kuileta pamoja Kenya, ilikuwa inaelekea kutumbukia tena katika machafuko.  Maafikiano haya yamezaa ‘utakatifu’ ambao Wakenya wameubatiza jina la kimombo, handshake. Endelea…

Kabla sijaendelea na makala hii ya Odinga, msomaji niruhusu angalau kwa aya mbili tu nizungumzie tukio la kutekwa kwa Mohamed Dewji (Mo). Leo katika habari kuu ya gazeti hili tumeandika kuwa Mo ameokolewa na teknolojia. Kwamba ana kifaa maalumu mwilini mwake kinachoitwa ‘microchip’ ambacho kimekuwa kikirekodi taarifa zote tangu amekamatwa hadi anaachiwa.

Kifaa hiki inaelezwa kuwa aliwekewa nchini Uingereza miaka 10 iliyopita. Hakika tukio hili limelifedhehesha taifa letu. Nampongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro, kwa jinsi alivyosambaza askari wake kumsaka Mo, ila kutojibu maswali ya wanahabari siku ya Jumamosi iliyopita kumeacha maswali mengi.

Ukiacha namba za gari kutofanana, gari la awali alilolionyesha lilikuwa na tairi nyuma ya mlango, ila gari la pili tairi lipo chini. Naamini bado tunastahili kufanya uchunguzi wa kina kubaini ni kina nani hao waliokuwa wamemteka Mo. Tusiliache hili likapita kimya, maana “mzaha mzaha hutumbua usaha.”

Nikirejea kwa Odinga, nasema awali katika Serikali ya mzee Mwai Kibaki waligawana nyadhifa za juu serikalini na Odinga akaukwaa uwaziri wa barabara, uliomkutanisha na waziri kama huyo kwa upande wa Tanzania wakati huo, ambaye sasa ni Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli. Walijenga uswahiba mkubwa uliodumu hadi leo.

Katika kipindi hicho kina Odinga waliweka makubaliano ya mdomo( gentleman agreement) kwamba katika muhula wake wa kwanza, lazima Kibaki afanikishe pamoja na mambo mengie, kuandikwa kwa katiba mpya itakayounda wadhifa wa waziri mkuu mtendaji na rais asiye na meno (ceremonial president).

Katika makubaliano ambayo baadaye Kibaki aliyashtukia na kuyapiga chini, ilikuwa imekubaliwa kwamba mzee Kibaki atawale muhula mmoja tu na kumkabidhi kijiti makamu wake wakati huo, Kijana Michael Wamalwa.

Baada ya Kibaki kuushtukia mtego huo, Odinga aliwashawishi baadhi ya mawaziri wenzake wakafanya uasi ndani ya serikali yao, wakishinikiza kuundwa katiba mpya.

Akishirikiana kwa karibu sana na aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Kalonzo Musyoka, walianzisha mapambano yaliyozaa upigaji wa kura ya maoni kuamua kama iandikwe katiba mpya au ile iliyokuwepo ikarabatiwe kidogo tu.

Odinga akakaa na kambi yake iliyotumia kaulimbiu ya ‘Chungwa’ kudai katiba mpya na upande wa pili ikawepo kambi ya Kibaki iliyotumia kaulimbiu ya ‘Ndizi’ kutetea katiba iliyokuwepo. Kundi la Odinga liliibuka kidedea dhidi ya bosi wao na ikatungwa katiba mpya mwaka 2010.

Kwa gadhabu, Kibaki akawafuta kazi Odinga na kundi lake, na hapo ndipo akawa amekoleza moto. Harakati za ukombozi nchini humo zikaanza rasmi. Kina Odinga ambao walipiga kampeni ya nguvu ya ‘Kibaki Tosha’, ndiyo iliyoiangusha KANU, wakaibuka na vuguvugu jipya ambalo lilijulikana kama Orange Democratic Movement (ODM).

ODM ilizoa mawaziri wengi wa Kibaki na kuanza mapambano dhidi yake, walibadilisha kaulimbiu yao ya ‘Kibaki Tosha’ mwaka 2002 na kuja na mpya ya ‘Kibaki Toka’ mwaka 2007.

Ili kumng’oa Kibaki, ODM ilitengeneza chombo cha juu cha maamuzi cha Pentagon, kikiwa kimewekwa sawia kulingana na jiografia na siasa za ukabila za nchi hiyo, ambacho kilizoa kura nyingi.

Odinga mwenyewe na Najib Balala (Waziri wa sasa wa Utalii), waliwakilisha masilahi ya Mkoa wa Pwani, huku Kalonzo na Charity Ngilu wakiwakilisha masilahi ya Ukambani. Ruto (kabla hawajafarakana), aliyekuwa ameuacha ukatibu mkuu wa KANU, aliuwakilisha vema Mkoa wa Bonde la Ufa katika chombo hicho na kuzoa kura nyingi za kabila la Kalenjini.

Makamu wa Rais mstaafu, Musalia Wycliffe Mudavadi, aliwakilisha Mkoa wa Magharibi na viunga vyake.

By Jamhuri