Makala iliyopita ya “JWTZ nginjangija Goma hadi Kigali’, imenifumbua macho. Nimepata simu nyingi na ujumbe wa maandishi usio idadi. Wapo waliotumia lugha kali, lakini wengi walikuwa waungwana. Hiyo ndiyo raha ya mijadala. Kuna wakati tunaweza kukubaliana kwenye baadhi ya mambo, na wakati mwingine tusikubaliane kwa hoja fulani fulani. Muhimu ni kujenga moyo wa uvumilivu na staha.

Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, katika maandishi yake ya Mei, 1962 kupitia kijitabu chake cha “Tujisahihishe’, anasema, “Hatuna budi, hasa katika majadiliano na mazungumzo yanayohusu jumuiya, tujifunze kusikiliza hoja zenyewe zinazotolewa na wenzetu, na kuijibu zile hoja kwa kuzikubali au kuzikataa, bila kujali kama aliyezitoa ni rafiki au si rafiki. Pia wanaopingwa hawana budi wakubali kuwa kinachopingwa ni zile hoja zao, siyo wao wenyewe. Bila mazoea haya, mazungumzo hayana maana; yanakuwa ni kupoteza wakati maana huwa tumekwisha kuzihukumu hoja za mtu hata kabla hajazitamka! Kadhalika, hoja zetu zikijibiwa kwa kupingwa halafu tukawakasirikia waliozipinga tunafanya mazungumzo yasiwe na maana, kwa sababu tunapenda hoja zetu zikubaliwe tu hata kama si hoja safi.”

 

Baba wa Taifa anaongeza kusema, “Wakati mwingine mtu tunayempinga huwa ana makosa kweli, lakini hoja tunaotoa ni za kinafsi na hazihusiani kabisa na hoja zake. Nikisema mbili na tatu ni sita, nakosa. Lakini ni bora kunionyesha kwamba pengine nafikiri tunazidisha kumbe tunajumlisha. Ni kweli mbili mara tatu ni sita, lakini mbili na tatu ni tano, siyo sita. Lakini ukijaribu kuwashawishi wenzetu wakatae mawazo yangu na kukubali yako kwa kusema kuwa meno yangu ni machafu, au natoa kamasi daima, utakuwa unatumia hoja ambazo hazina maana. Huu ni mfano wa upuuzi, lakini mara nyingi hoja tunazotumia kuwashawishi watu wakatae mawazo ya wale tusiowapenda, au kukubali mawazo yetu huwa hazihusiani kabisa na mambo tunayoyajadili.” Mwisho wa kunukuu.

Naam, wapo waliothubutu kunikosoa kwa kuihama mada. Nashukuru kwamba wametilia shaka mambo yangu kadhaa, lakini si uzalendo kwa taifa langu. Msingi wowote wa nchi imara ni umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wake. Nchi haiwezi kuwa nchi kama watu wake ni wababaishaji na walio tayari kuitoa nchi yao kwa watu wasio wa taifa hilo. Watanzania tulisifika sana kwa kuwa na umoja na mshikamano miongoni mwetu, kiasi kwamba tuliamini adui anaweza kuingia kirahisi Tanzania, lakini kamwe hatotoka salama.

 

Majibu niliyoyapata kutoka kwa baadhi ya wasomaji, hasa kuhusu suala la wahamiaji haramu hapa nchini, yananishawishi niamini kuwa tunahitaji nguvu za ziada kurejea kwenye ujenzi wa taifa letu.

 

Wapo wanaosema uzalendo hauwezi kujengwa kwa sababu viongozi wenyewe si wazalendo. Kuamini hivyo ni kosa. Ni kosa kwa sababu sisi wananchi wenyewe ndiyo tunaopaswa kutekeleza wajibu wetu halali wa kuwalazimisha viongozi kuwa wazalendo. Kama tunajua kiongozi fulani ni muuza ardhi yetu kwa wageni, kwanini tumvumilie? Ana nguvu gani za kivita za kutushinda jeshi la wazalendo wa nchi hii? Hakika hana jeshi la kutushinda.

 

Tunashukuru kuwa Rwanda wameanza kupunguza chokochoko zao kwa Tanzania. Marais wetu-Jakaya Kikwete na Paul Kagame, wamekutana na kutokana na nyuso ambazo ukizitazama kwa umakini, utaona zilikuwa nyuso za kupendezesha picha! Mioyoni mwao huenda kukawa bado na makunyanzi ya fadhaa.

 

Rais Kagame si wa kumwamini sana. Msomaji mmoja ameniletea ujumbe huu wa maandishi, “Mwandishi, siachi kukuita mzalendo wa kweli juu ya ajenda ya Rwanda kwa Tanzania. Kwanza tuna eneo ambalo Watutsi hao wanamiliki milima kama sehemu ya Kitutsi katika Mkoa wa Rukwa kando ya Ziwa Tanganyika na katika Mkoa wa Kigoma wamejiita Wahambwe.  Sehemu za Nguruka kando ya Mto Malagarasi napo wamejitanua kama himaya ya Kitutsi. Hao wote walihamia miaka ya 1950 wakitokea huko Rwanda. Fanyeni tafiti majibu mtayapata.”

 

Mwananchi huyo ameongeza kwenye ujumbe wa pili kwa kusema, “Kwa Rukwa eneo hilo linaitgwa Mwese milimani kando ya kando mwa Ziwa Tanganyika. Kwa Kigoma kupitia Tarafa ya Buhingu au Mgambo.” Mwisho wa ujumbe huo wa maandishi.

 

Historia ya Afrika iko wazi. Wakoloni walitugawa Waafrika bila kufuata makabila, ndiyo maana Wakurya na Waluo wapo Kenya na Tanzania. Wamakonde wapo Tanzania na Msumbiji. Warundi ndiyo Waha hao hao. Wahangaza na ndugu zetu wa Uganda ni kitu kimoja.

 

Pamoja na ukweli huo, bado viongozi wa Afrika walikubaliana kuheshimu mipaka iliyowekwa na wakoloni. Walifanya hivyo ili kuondoa adha na migongano isiyokuwa ya lazima. Uamuzi huo haukuathiri msimamo wa baadhi ya mataifa, Tanzania ikiwamo, ya kuamini kuwa “Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja”.

 

Maneno hayo ya mwisho ndiyo pengine yanayotumiwa na Wanyarwanda na wahamiaji wengine haramu kuingia nchini bila kufuata taratibu. Ni ukweli ulio wazi kuwa wahamiaji haramu kutoka Burundi, Rwanda au Kenya wana tabia tofauti na Watanzania. Sisi tumelelewa katika umoja, upendo na mshikamano. Tumefundishwa kuwapokea na kuwasaidia wageni bila kujali hali zetu za kiuchumi. Ukarimu wetu umetumiwa kuwa chachu ya kunyanyaswa kwetu katika ardhi yetu.

 

Katika makala iliyopita nilisema kuwa hata kama ni kweli “Binadamu wote ni ndugu zangu na Afrika ni moja”, hiyo haina maana kwamba sasa kila anayetaka kuja kutuonea, basi aingie tu bila kuulizwa au kuhojiwa. Marekani wanaotamba kwa kujiona mababa wa demokrasia na haki za binadamu, kamwe hawajafungua mipaka yao na kuwaacha tu wageni wanaotaka kuingia, kufanya hivyo bila kufuata utaratibu. Wahamiaji haramu kutoka Mexico wapo wengi nchini Marekani. Wapo kwa kificho, na si kwa kutamba mitaani na kufanya lolote watakalo.

 

Uamuzi wa Rais Kikwete kuwataka wahamiaji haramu kurejea kwao kwa hiari ulikuwa na utaendelea kubaki kuwa ni uamuzi wa busara. Tena basi, akawataka wale wasio na vibali au wanaotaka kuhalalisha ukaazi wao, wafanye hivyo kisheria. Sote kila siku tunalia kutokana na matukio ya ujambazi na mauaji. Haya yamechangiwa mno na ujio wa wahamiaji haramu. Mtu ambaye hana rekodi yake, ni rahisi kufanya jambo lolote baya na kutoweka.

 

Kauli ya Rais Kikwete imepokewa kwa kejeli na dharau kutoka kwa vibaraka fulani fulani. Ingawa sina desturi ya kuwatetea viongozi wa Serikali, kwa hili nitabaki kuwa miongoni mwa watetezi wa Rais wetu. Mara kadhaa nimesema hata kama humu ndani ya taifa letu hatumpendi Rais Kikwete, linapokuja suala la nchi na nchi lazima tuungane tuwe upande wa kiongozi wetu mkuu. Wale Republican wa Marekani linapokuja suala la maslahi ya nchi yao, wanaungana na Democratic. Nasi tuige tabia hiyo nzuri.

 

Wapo wanaohoji, iweje wahamiaji haramu wawe ni kutoka Rwanda, Burundi, DRC, Uganda au Kenya pekee? Mbona Wachina wengi hawashughulikiwi? Swali zuri lakini pia ni dhaifu.

 

Hapa ndipo ninaposema kuwa dhima ya kuwa na viongozi wazalendo inaanzia kwa wananchi wenyewe. Kama Rais Kikwete kawagusa Wanyarwanda, na tayari wananchi kadhaa wamejitokeza kumpinga, hali itakuwaje wakiguswa Wachina, Wahindi au Wazungu? Taarifa za wahamiaji haramu wa aina hiyo tunazo sisi wenyewe wananchi. Tunayajua mabohari wanamolala. Tunajua wanakokwenda kuburudika. Viongozi wetu wa Uhamiaji wanawajua. Polisi wanawafahamu sana. Lakini nani anawajibika kuwashughulikia kisheria?

 

Sijakutana na polisi Mtanzania mzungu au mwenye rangi tofauti na hii ya wengi wetu. Sisi wenyewe tumejenga nadharia potofu kuwa hakuna mzungu mwizi au tapeli! Nashukuru wananchi wa Mbezi Beach hivi karibuni walimkamata Mzungu mwizi kwenye mashine ya ATM. Hapo ndipo wengi wetu tulitambua kuwa kumbe hawa jamaa nao wamo vibaka! Mwingine mwenye asili ya Kiasia kakamatwa kwa tuhuma za ujambazi!

 

Barabarani trafiki wetu wengi hawasimamishi wazungu. Pengine ni kwa kutomudu lugha ya mawasiliano, lakini pili ni ile dhana duni ya kwamba mzungu ni mtu makini-hafanyi makosa! Tumejiaminisha hilo kiasi kwamba wengi wetu kwenye nyumba zetu tumepamba picha za watoto wa kizungu; hali inayowafanya watoto wetu wakue wakiamini kuwa mzungu ni bora zaidi, maana asingekuwa bora, basi yeye mtoto mweusi naye angeiona picha yake ukutani!

 

Ninachojaribu kukieleza hapa ni kwamba sheria zetu zifanye kazi kote kote bila kuuliza mbona fulani hafanywi vile au hivi. Hii ni kama hoja dhaifu ya Waafrika kadhaa wanaohoji iweje Mahakama ya ICC iwe ni kwa Waafrika tu. Je, kama Waafrika wanafanya uhalifu, kwa hiyo waachwe kwa sababu hata wazungu nao wanafanya?

 

Watanzania wa kweli tunapaswa kulipenda taifa letu. Tunapaswa kulilinda kwa hali na mali. Tuifanye kazi hii, si kwa manufaa yetu ya leo, bali kwa hao Watanzania wa baadaye ambao ni wajukuu, vitukuu na vilembwe vyetu.

 

Tunapaswa kuzitambua hila za majirani zetu na kukaa mkao wa hadhari. Tunapaswa kuilinda ardhi yetu dhidi ya watu wote wenye njama za kutupoka. Tupambane nao bila kujali kama ni wageni au ni wazawa.

 

Tuwe tayari kupambana na wote wanaoeneza kauli chafu za kutugawa kwa kisingizio kwamba Tanzania ya sasa si moja. Maadui zetu wameanza kutumia sinema ya kweli ya ngumi za bungeni kuthibitisha kuwa Watanzania si wamoja tena.

 

Mimi nasema hao wanajidanganya. Ngumi bungeni si jambo la kustaajabisha. Ukisoma vema historia ya Sergeant at Arms kuwapo bungeni, utajua ni kwa sababu gani. Wabunge wanagombana, lakini ambacho sijawahi kuona ni kwa askari kumpiga mbunge ndani ya ukumbi wa Bunge!

Wala sijawahi kusoma wala kusikia wabunge wa chama kinachotawala wakiacha kujadili muswada ulio mbele, badala yake wanatumia dakika zote kutukana. Hii inaweza kuwa mbinu ya Serikali ya kuwa-provoke wapinzani ili wagombane na Spika, hatimaye miswada ipitishwe kiulaini. Ugomvi ndani ya Bunge ni ukomavu wa demokrasia. Hiki ni kipindi cha mpito, na wala hakujafanya umoja na mshikamano wetu viyumbe.

 

Hao waliopigana bungeni walitaka Katiba nzuri! Hayo ni mapambano halali. Kama wangekuwa wakigombea posho, hapo tusingewaelewa. Bado nasisitiza umuhimu na wajibu wetu wa kuendelea kutomwamini sana Rais Kagame na wafuasi wake. Ndani ya Tanzania ana wafuasi, hata kama si wengi, lakini wana ushawishi na mbinu za kujitetea. Tukae mkao wa tayari tayari. Asante sana.

1426 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!