TABORA

Na Tiganya Vincent

Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Balozi Dk. Batilda Buriani, amezitaka taasisi za utafiti wa wadudu kuchunguza matumizi ya salfa (sulfur) wakati wa kunyunyuzia mikorosho kama haina athari kwenye ufugaji nyuki.

Amesema ni muhimu ili makundi ya nyuki yasije yakapotea kutokana na matumizi ya viuatilifu, ikiwamo salfa, ambavyo vinaweza kusababisha vifo kwa nyuki wakati wanakwenda kwenye maua kutafuta chavua.

Balozi Dk. Batilda ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akihutubia kikao cha robo ya kwanza cha Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Uyui.

Amesema asali ni nembo ya kielelezo kikubwa cha Mkoa wa Tabora, kwa hiyo shughuli yoyote ya kuathiri makundi ya nyuki si vema ikafanyika.

Balozi Dk. Batilda ameongeza kuwa nyuki wanazo faida nyingi, ikiwamo uchavushaji wa mimea ya mazao mbalimbali na uzalishaji wa asali na mazao mbalimbali ya nyuki.

Balozi Dk. Batilda amesema vitendo vya kuhatarisha maisha yao vinahatarisha pia maisha ya wakazi wa Tabora kwa kupoteza utajiri wa asili wa asali na kudhoofisha uzalishaji wa mazao mashambani. 

Amesema kimsingi hapingi ulimaji wa korosho katika mkoa huo bali kinachotakiwa kuangaliwa kwa upana ni faida na hasara zitakazopatikana kutokana na matumizi ya viuatilifu kwenye korosho dhidi ya uzalishaji wa asali. 

Balozi Dk. Batilda amesema ni vema watafiti wa wadudu na wale wa kilimo wakashirikiana ili kuja na msimamo wa aina moja katika suala la kilimo cha korosho mkoani Tabora.

Amesema mkoa huo umo katika mkakati mkubwa wa kuongeza matumizi ya mazingira kisasa ili kuongeza uzalishaji wa mazao ya nyuki, vitendo vya kuhatarisha maisha ya nyuki vitawarudisha nyuma. 

Aidha, Balozi Dk. Batilda amesisitiza kuwa yapo mazao mengi ya kudumu nje ya korosho kama michikichi ambayo yakilimwa mkoani humo hayana athari kwa nyuki.

By Jamhuri