RC K’njaro amilikisha marehemu kiwanja

galleryNdugu zangu wanahabari,

Januari 30 mwaka huu, niliwaiteni na kuwaeleza kwa kirefu kuhusu mgogoro wa kiwanja kilichokuwa na hati namba 10660 ambacho ndipo zilipo Ofisi za Kata ya Mawenzi ambacho zamani kilikuwa kikimilikiwa na The Registered Trustees of Mawenzi Sports Club kabla ya kutwaliwa na Serikali mwaka 2002.
Lakini kama mtakavyokumbuka, niliwaeleza namna Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, ilivyoshiriki na kuwezesha taasisi hiyo kumilikishwa tena kiwanja hicho hata baada ya Serikali kukitwaa kiwanja hicho kutokana na Government Notice namba 55 ya 2002.


Mimi nikiwa Mbunge wa Moshi Mjini, kwa kushirikiana na Madiwani wa Halmashauri yetu wanaotokana na Chadema, tumeendelea kupambana na njama za kupora mali ya umma na suala hili sasa linachunguzwa na Polisi kubaini kuwapo viashiria vya makosa ya kugushi nyaraka.
Katika kufuatilia jambo hili, Madiwani wakiongozwa na Meya wa Manispaa ya Moshi, waliandika barua katika mamlaka mbalimbali za uchunguzi nchini. Mimi binafsi nimekwenda kuonana na wakuu wa taasisi hizo kuwaeleza kuwapo kwa kile ninachoamini kuwapo kwa mchezo mchafu.
Tumepitia jalada la kumbukumbu za wadhamini wa taasisi ya Mawenzi Sports Club lililopo Registration Insolvency and Trusteeship Agency (Rita) na kubaini mambo mazito ambayo yamenifanya leo niwaiteni kuwapa mrejesho wa yale tuliyoyagundua katika jalada hili.


Tumebaini kuwa tarehe 05.01.2008, wadhamini wa taasisi hiyo waliotajwa kuwa ni Devchand Nathu Shah na Mohamedali Shariff wanaonekana kwenye kumbukumbu (minutes) za kikao hicho kuwa walihudhuria kikao hicho na kuhamisha udhamini wao kwa Amratlal N. Pattn na Hitesh H. Solani wa S.L.P 392 hapa Moshi.
Lakini tumeibani kuwa Devchand Nathu Shah alifariki dunia mwaka 1979 wakati Mohamedali Shariff alifariki mwaka 1998. Tunajiuliza ilikuwaje wadhamini hao waliofariki mwaka 1979 na 1998 wakae tena kikao Januari 2008 wakati walishafariki dunia?
Kumbukumbu za Return of Trustees za miaka iliyofuata baada ya kufariki (2000-2008), zinaonekana kuwasilishwa RITA mwaka 2012 zikiwa na sahihi ya wadhamini hao ambayo tayari walikuwa wameshafariki tangu miaka ya 1979 na 1998.


Ni kutokana na kuwapo kwa dalili za udanganyifu huo, tuliwasiliana na vyombo vya kiuchunguzi na RITA na kuonyesha udanganyifu huo na tunashukuru Mkurugenzi wa RITA, Bw. Gilbert Bubelwa amewaandikia barua wadhamini hao wapya na kuwasimamisha kutekeleza majukumu yao.
Katika barua yake ya Aprili 10,2015 Bubelwa amenukuu kifungu namba 17(1) cha Sheria ya Wadhamini sura 318 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2002 kinachotaka ili udhamini wa wadhamini ukubaliwe ni lazima kuwepo kikao halali na kuwepo na uangalizi wa mamlaka za Serikali.
Ukisoma masharti ya vifungu vya sheria hiyo na udanganyifu tunaoamini umefanyika katika kutunga kikao na kuwahusisha watu ambao ni marehemu, ni dhahiri hata miamala (transaction) zote zilizofanywa na wadhamini hao ni batili mbele ya uso wa sheria.


Tunafahamu, ni kutokana na mabadiliko hayo ya wadhamini, nyaraka za wadhamini hao ndizo zilizotumika katika mchakato mzima wa kupatiwa hati mpya Mawenzi Sports Club ya kumiliki kiwanja hicho ambacho kilitwaliwa na Serikali kama nilivyotangulia kusema.
Kubainika kwa udanganyifu huo, kunafanya tuhoji umakini wa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Mheshimiwa Leonidas Gama na wote waliomshauri hadi akafikia hatua ya kuandika dokezo tarehe 26.11.2014 akimwagiza Katibu Tawala wake (RAS) abariki mchakato mzima wa uporaji huo.
Ni rai yetu kwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete, kumwajibisha Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Leonidas Gama kwa kushindwa kutumia vyombo vyake kulinda mali ya umma isiweze kuporwa na kikundi cha watu wachache kwa kutumia mgongo wa uamuzi wa Ofisi ya RC Gama.
Tunamuomba Mheshimiwa Rais, atumie mamlaka yake kubatilisha hati mpya ya umiliki wa kiwanja hicho, ambayo wamepewa Mawenzi Sports Club baada ya kubainika kuwapo kwa udanganyifu wa kikao cha wadhamini na pia kugushi returns zilizowasilishwa RITA.


Mbali na hilo, lakini tunaiomba taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), kuanzisha uchunguzi rasmi wa watendaji wote wa Serikali waliotumia vibaya madaraka yao na kupotosha ukweli juu ya uhalali wa Mawenzi Sports Club kupewa hati mpya ya kumiliki kiwanja hicho.
Tunapoimba Takukuru kuchunguza jambo hili, hatumaanishi kwamba tumekosa imani na uchunguzi unaondelea kufanywa na Jeshi na Polisi, la hasha! Bali tunafanya hivyo kutokana na msingi kuwa Jeshi la Polisi litajikita zaidi katika uchunguzi wa makosa ya kugushi wakati tunaona katika mchakato mzima vipo viashiria vya rushwa kwa baadhi ya watendaji.


Ni matumaini yetu kuwa vyombo hivi vitafanya kazi kwa weledi na uadilifu mkubwa ili kurejesha imani ya wananchi wa Moshi na Watanzania na pia kuonyesha kuwa nchi hii inaendeshwa kwa misingi ya utawala wa Sheria ili wale wanaoboronga, basi wawajibishwe ikithibitika hivyo.
Pamoja na taarifa, nitawapa nyaraka mbalimbali kuhusiana na sakata hili.
Imetolewa leo mjini Moshi tarehe 18.04.2015

Philemon Ndesamburo ni Mbunge wa Moshi Mjini (CHADEMA). Taarifa hii aliitoa kwa waandishi wa habari wiki iliyopita mjini Moshi. Tumeichapisha kama ilivyo kwa kuzingatia msimamo wetu wa utawala bora na uwajibikaji.
Mhariri