IGP Mwema ampa hifadhi ‘muuaji’ wa Barlow

*Apewa ulinzi wa polisi wenye silaha

*Anapewa huduma zote za kibinadamu

*Mbunge, Naibu Waziri wahusishwa ujangili

Kijana Mohamed Malele aliyejisalimisha kwenye vyombo vya ulinzi na usalama akijitambulisha kuwa mshirika wa mtandao uliohusika kumuua Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Liberatus Barlow, amepewa ulinzi maalumu.

Ulinzi huo umetolewa na Mkuu wa Jeshi la Polisi hapa nchini, Inspekta Jenerali (IGP) Said Mwema.

 

Chanzo cha habari kimeiambia JAMHURI kwamba Malele anahifadhiwa katika nyumba maalumu jijini Dar es Salaam, akilindwa na polisi wenye silaha na kupewa huduma zote za kibinadamu. Kutokana na sababu za kiusalama, gazeti hili linaendelea kuhifadhi jina la mtaa alikohifadhiwa.

 

Malele ana siri nzito juu ya mtandao mpana wa mauaji ndani ya Jeshi la Polisi, unaohusisha watumishi wengine kutoka vyombo vya ulinzi na usalama, wafanyabiashara na wanasiasa.

 

Habari za karibuni kabisa zinasema kwenye orodha ya aliowataja kwenye mtandao wa uhalifu, wamo wabunge na naibu waziri. JAMHURI inaendelea kuyahifadhi majina yao kwa kuwa haijafanikiwa kuzungumza nao.

 

Mtandao huo unatajwa na Malele ambaye ni mkazi wa Kijiji cha Igoma, Kwimba mkoani Mwanza, kwamba ndiyo uliohusika na mauaji ya Kamanda Barlow usiku wa kuamkia Oktoba 13, mwaka jana katika eneo la Kitangiri jijini Mwanza, alipokuwa akimrejesha nyumbani Mwalimu anayetajwa kwa jina la Doroth Moses, aliyekuwa naye katika kikao cha harusi.

 

Malele alikamatwa Ijumaa ya Mei 10, mwaka huu, katika lango la Bunge mjini Dodoma wakati akijaribu kuwatafuta wabunge kadhaa.

 

Malele anatajwa kuwa mtu muhimu ambaye taarifa zake zinawasaidia viongozi wa juu wa vyombo vya ulinzi na usalama, na Serikali kwa jumla, kuutambua na kuufumua mtandao wa uhalifu ndani ya Jeshi la Polisi.

 

Namna alivyokamatwa

Malele anasema kwamba kikundi cha maofisa wa ngazi za juu wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kinachojihusisha na matukio ya ujangili, kilimtaka ashiriki kwenda kumuua Kamanda Barlow.

 

 

Anasema, pamoja na ukweli kwamba ameshiriki matukio mengi ya mauaji, hakutaka kabisa kwenda kumuua Barlow kwa kuwa anamfahamu vema, na kwamba alishafanya kazi nyumbani kwake.

 

“Nilikataa kwenda kumuua Kamanda Barlow, roho iliniuma sana walipotaka nishiriki mauaji hayo, kwa kweli nilihuzunika sana,” anasema.

 

Uamuzi wake wa kukataa kwenda kushiriki kwenye mauaji hayo, uliwatia hofu washiriki hao wa uhalifu, hatua iliyowafanya wamkamate Malele na kumpeleka katika Gereza la Butimba, akiwa amebambikiwa kesi ya ujambazi wa kutumia silaha.

 

Anasema akiwa gerezani, kikosi cha uhalifu ndani ya Polisi, kilikwenda kumuua Barlow, na kwamba siku chache baadaye, akiwa gerezani, alipata taarifa za mauaji hayo.

 

“Niliposikia Kamanda Barlow kauawa sikushangaa kwa sababu niliwajua wauaji, lakini cha kusikitisha ni pale niliposikia eti kuna Mwalimu amekamatwa akihusishwa na mauaji hayo,” anasema.

 

Malele anamtaja mmoja wa maofisa walioshiriki kumshinikiza ashiriki mauaji hayo, na ambaye anasema inawezekana alishiriki moja kwa moja kumuua Barlow kuwa ni Kamanda Muna.

 

Taarifa za uchunguzi zinaonesha kuwa Malele baada ya kuwapo gerezani kwa miezi kadhaa, Mkuu wa Gereza aliamua kumwachia kwani hakuona sababu ya kuendelea kumhifadhi mtu ambaye hana chembe ya mashitaka.

 

Inaelezwa kwamba mtandao wa uhalifu uliposikia taarifa za kuachiwa kwa Malele, ulijiandaa kumuua mara baada ya kurejea uraiani. Hatua hiyo ilimfanya kijana huyo agome kwa muda kutoka gerezani akitambua kuwa angeuawa.

 

“Nilimweleza Mkuu wa Gereza mambo yote, naamini kwa maelezo yale aliwasiliana na wahusika, sina uhakika, lakini nilidhani hivyo. Kwa sababu hiyo nikaogopa kuwa nikitoka lazima nitauawa. Baadaye nikapata wazo nikitoka gerezani niende wapi,” anasema kwenye maelezo yake.

 

Malele akimbilia katika Kikosi cha JWTZ

Baada ya kuachiwa kutoka Gereza la Butimba, Malele alikwenda moja kwa moja kujisalimisha katika Kikosi cha Anga cha Jeshi la Ulinzi la  Wananchi wa Tanzania (JWTZ) kilichopo eneo la Uwanja wa Ndege wa Mwanza.

 

Uchunguzi wa JAMHURI unaonesha kuwa alipojisalimisha, aliwaeleza wanajeshi hao ‘mkanda mzima’ wa mauaji na vitendo vya ujambazi alivyokuwa akivifanya na hatari iliyokuwa ikimkabili endapo kikosi cha uhalifu kingejua yupo uraiani.

 

Inaelezwa kwamba wanajeshi waliomsaidia walijaribu kuwasiliana na wabunge kadhaa wakiwa na matarajio ya kuwapata ili waweze kumsaidia. Hata hivyo, kuna maelezo kwamba wabunge wengi hawakupokea simu, na hata wengine walipopokea, hawakuonesha nia ya kukutana na kijana huyo ili kumsaidia.

 

Uchunguzi unaonesha kuwa mbunge mmoja aliweza kuzungumza na kijana huyo na kumtaka afike mjini Dodoma ili aweze kusaidiwa. Kuna habari kwamba wanajeshi, kwa huruma na kwa kuzingatia uzito wa maelezo ya kijana huyo, walimsaidia nauli ya basi na Sh 10,000 kwa ajili ya chakula njiani.

 

Anaswa akiwatafuta wabunge

Malele alipofika Dodoma jioni, alipumzika na kwenda katika Ukumbi wa Bunge asubuhi. Kitendo chake cha kutojua kusoma na kuandika kilimfanya awe na karatasi yenye majina na namba za simu za Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu, na Mbunge wa Musoma Mjini, Vincent Nyerere.

 

Maofisa Usalama wa Taifa na Polisi waliokuwa katika lango alilofika walipomuuliza anataka kumwona nani, aliwapa majina hayo na namba za simu. Walipombana zaidi kujua shida yake nini, inasemekana Malele alianza kuwaeleza historia yake na namna alivyofika hapo bungeni.

 

Polisi waliposikia taarifa hizo, inaelezwa kwamba ziliwashitua, na wakaamua kuwasiliana na viongozi wakuu wa Polisi Mkoa wa Dodoma, ambao waliamuru awekwe rumande. Polisi hao waliwasiliana na wenzao wa Mwanza, na ndipo ikatolewa amri kuwa arejeshwe Mwanza kwa maelezo kwamba “ni mtuhumiwa hatari wa ujambazi”.

 

Hata hivyo, taarifa zilimfikia mmoja wa mawaziri, na yeye akawasiliana na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, David Misime, na kumtaka asimrejeshe Mwanza kijana huyo.

 

Uchunguzi wa JAMHURI unaonesha kuwa baadaye taarifa zilimfikia Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dkt. Emmanuel Nchimbi, na ndipo ukaandaliwa utaratibu wa kumhoji. Kwenye mahojiano hayo walihusishwa pia maofisa wa Usalama wa Taifa.

 

Imeelezwa kwamba kabla ya kuhojiwa, alijengwa kisaikolojia kwa kumhakikishia kwamba asingedhurika wala kupigwa. Alipewa chakula na akawa huru kuzungumza.

 

Habari za uhakika zinasema kwamba Malele alitoa maelezo marefu ya namna alivyoshiriki matukio mbalimbali ya ujambazi katika miji ya Mwanza, Geita, Shinyanga na maeneo mengi ya Kanda ya Ziwa.

 

Aliweka wazi kwamba yapo matukio mengi ambayo alitumika kama chambo. Miongoni mwa matukio anayoyaeleza kuwa yanamuumiza sana moyoni ni la yeye kutumiwa kumwita mama aliyekuwa kanisani, na kisha kuondoka naye na kwenda kumuua.

 

“Kwenye mauaji hayo nilimfuata mama kanisani, alipotoka tukamteka na kwenda kumuua. Shida yetu ilikuwa viungo – tulikata maziwa na viungo vya sehemu za siri – hivi vinatumiwa na wafanyabiashara,” amenukuliwa akisema.

 

Matukio ya ujambazi yalivyofanikishwa

Malele anasema ameshiriki matukio mengi – makubwa na madogo – ya ujambazi katika maeneo ya Ukerewe, Kahama, Shinyanga, Mwanza, Geita na kwingineko.

 

Kwenye mauaji ya Barlow, anasema chanzo hasa kilikuwa kwamba Kamanda huyo aliwahi kuwadhulumu wenzake, na kwamba walipomfuata mara kadhaa awape mgawo, aliwaahidi kufanya hivyo baada ya kupata “kazi nyingine kubwa”.

 

Anasema kikosi cha uhalifu kinawashirikisha Polisi, maofisa kadhaa wa Usalama wa Taifa, wafanyabiashara na wanasiasa kadhaa.

 

Anawataja wanasiasa wengine kuwa wapo katika Kata ya Mwamayombo, Ngudu mkoani Mwanza. Anasema wapo wanasiasa wawili marafiki ambao mwaka 2010 waligombea udiwani (jina la kata tunalihifadhi kwa sasa) kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA).

 

Ananukuliwa akisema, “Hawa ni marafiki sana, waligombea [kupitia] vyama tofauti kama kupoteza lengo, lakini walichotaka ni kuhakikisha mmoja wao anakuwa diwani. Kwenye uchaguzi akashinda wa CCM. Hawa ni majambazi, na ndiyo tulioshiriki nao kumuua yule mama wa Geita. Nilikuwa nasimamia miradi yao, nakusanya fedha kwenye maduka yao… waliniamini sana.”

 

Anasema kwenye ujambazi huwa wanatumia bunduki zilizokamatwa kutoka kwa majambazi wengine.

 

“Bunduki walichukua zile zinazokamatwa kwa majambazi, risasi zilikuwa zinapatikana Polisi,” anasema.

 

Uamuzi wa kuacha ujambazi

Malele anasema mama yake ni Mchungaji, na kwamba ameamua kuachana na ujambazi baada ya kuona anapata fedha nyingi, lakini haoni faida yake.

 

“Mama yangu ni Mchungaji, ameshiriki kuniombea sana niache ujambazi nikawa sitaki, lakini sasa nimeona sina sababu ya kuendelea kwa sababu sioni faida, napata pesa lakini sijui zinakwenda wapi,” amenukuliwa akiwaambia viongozi wa vyombo vya Ulinzi na Usalama mjini Dodoma kabla ya kusafirishwa kwenda kupewa hifadhi maalumu.

 

Habari zinasema kuwa Waziri Mkuu Mizengo Pinda ameamuru kijana huyo apewe hifadhi maalumu na apewe huduma zote za malazi, chakula na ulinzi kwa ajili ya usalama wake. JAMHURI inaendelea kufuatilia ili kujua hatima yake.

 

Kauli ya Waziri Nchimbi

Kwa upande wake, Waziri Nchimbi alipoulizwa juu ya Malele, alikiri kuwa na taarifa zake, lakini hakutaka kuingia kwenye undani wa suala hilo akisema ni nyeti.

 

Awali, uchunguzi wa mauaji ya Barlow ulianza kuelekea katika dhana kwamba zipo sababu zaidi za mauaji hayo.

 

Kikosi cha uchunguzi kilichoko Mwanza ambacho kilifuatilia, kilibaini kwamba Kamanda Barlow hakuuawa kwa sababu zinazohusiana na mapenzi pekee. Mapenzi inaweza kuwa njia moja ya kutaka kupotosha sababu za kweli za mauaji hayo.

 

Taarifa za kikosi cha uchunguzi zinasema kuna uwezekano wa mauaji hayo kuwa yamefanywa na vikundi vya kihalifu vya ndani ya Jeshi la Polisi, kwa kushirikiana na mitandao ya kihalifu nje ya Jeshi hilo.

By Jamhuri