‘ROMARIO’  Mwanamuziki mwenye vituko jukwaani

TABORA

Na Moshy Kiyungi

Unapoingia ukumbini kusakata muziki wa bendi ya Msondo Ngoma Classic, hakika utalazimika kushikilia mbavu zako utakaposhuhudia vituko, mbwembwe na vimbwanga vya mpuliza tarumbeta, Roman Mng’ande ‘Romario’.

Takriban kila onyesho la bendi hiyo yeye hufanya utundu wa kuwachekesha wapenzi ama kwa ‘kurap’ huku akiwa ameliacha wazi tumbo lake nene au kwa kuvuta kidevu chake chenye ‘mzuzu’ mrefu na kunengua mtindo wa Msondo, ulioasisiwa na Maalim Gurumo.

Roman Mng’ande ndilo jina lake halisi japo wengi humwita ‘Romario’. Huyu ni miongoni mwa wanamuziki maarufu wa Msondo, mwenye historia ndefu katika tasnia ya muziki, amevuma masikioni mwa mashabiki wengi ndani hata nje ya mipaka, hasa Nairobi, Kenya ambako ni gumzo.

Umaarufu wake umetokana na mambo mbalimbali yakiwamo uvaaji, ambapo hupendelea kuvaa mashati makubwa na kaptula ndefu, unyoaji wa nywele, pia uchangamfu wake jukwaani.

Mg’ande alisoma Shule ya Sekondari Kigurunyembe mjini Morogoro, baadaye, mwaka 1973, alijifunza kupuliza tarumbeta akiwa katika kundi la Father Kanuti aliyekuwa mwalimu mzuri wa ala hiyo ya upepo mjini humo.

Pia alijifunza kupiga vyombo vingine mbalimbali vya muziki lakini akajikita zaidi upande wa tarumbeta, alidumu katika kundi hilo kwa miaka sita. 

Mwaka 1979 akaenda jijini Dar es Salaam kujiunga katika bendi ya Urafiki Jazz kwa madhumuni ya kupata ukomavu na kukuza kipaji chake cha muziki chini ya uongozi wa Juma Mrisho ‘Ngulimba wa Ngulimba.’

Sifa zake zikasambaa jijini humo. Hakudumu muda mrefu katika bendi hiyo kwani mwaka 1981, Tanzania Stars wakampandia dau, Mng’ande hakusita kujiunga na kundi hilo.

“Unajua sisi wasanii ni kama wacheza mpira, mtu akikupandia dau hauwezi kuliacha, lazima umfuate… Tunafanya muziki ili tupate fedha, sasa kama umepewa, hauziachi!” anasema Romario.

Anaongeza kuwa alipofuatwa na viongozi wa Tanzania Stars hakukataa, kwani aliangalia masilahi zaidi, mambo mengine baadaye.

Akiwa na bendi hiyo, alijiongezea umaarufu na kuanza kusikika kwa mashabiki wengi wa muziki wa dansi. Alidumu hapo hadi mwaka 1983.

Kadiri siku zilivyosonga sifa zake nzuri katika muziki zilisababisha kufuatwa na viongozi wa bendi ya Juwata Jazz kipindi hicho ili ajiunge.

“Viongozi wa Juwata walinitafuta wakanieleza dhamira yao ni kutaka nikajiunge na bendi yao ambayo kipindi hicho ilikuwa tishio,” anasema Romario.

Anasema baada ya kufuatwa na viongozi hao hakufanya kosa na aliwaambia milango iko wazi.

“Lengo langu lilikuwa kuimba kwenye bendi kubwa kama Juwata, hivyo nilipofuatwa sikufanya kosa nikawaambia milango iko wazi waje tuzungumze,” anakumbuka.

Mwaka 1983 akajiunga rasmi na bendi ya Juwata Jazz wakati huo ikiwa na watunzi na waimbaji mahiri akina Gurumo, TX Moshi William, Joseph Maina, Athumani Momba, Suleiman Mbwembwe na wengine wengi.

Tokea kipindi hicho hadi sasa hajatoka kwenye bendi hiyo wala hatarajii kutoka mpaka atakapoamua kuachana na muziki.

“Kama nilirogwa, basi viongozi wa Msondo walipata mganga, kwani tokea nilipojiunga na bendi hii hadi sasa sijatoka wala sifikirii kutoka hata iweje,” anasema Romario.

Akielezea juu  ya mafanikio aliyoyapata kupitia muziki, Romario anasema: “Nimepata mafanikio makubwa nikiwa katika bendi hii na imenisaidia kufahamiana na watu wengi, viongozi wa serikali, kwa kweli nimepata mafanikio makubwa katika maisha yangu.”

Anakiri kwamba bendi ya Msondo imemtoa kimaisha, imemfanya kiwango chake cha muziki kukua siku hadi siku, hataweza kuisahau katika maisha yake yote.

Romario hana mpango wa kuanzisha bendi na lengo lake ni kuzidi kujiimarisha katika kazi yake hiyo ili bendi yake ya Msondo Ngoma iweze kufanya vema zaidi.

Anasema katika maisha yake ya muziki hawezi kumsahau TX Moshi William kwani alikuwa rafiki yake mkubwa na alikuwa akimshauri mambo mengi.

Romario anasema wanamuziki wengine ambao hawezi kuwasahau ni pamoja na Said Mabera na Gurumo.

Kibao ambacho hawezi kukisahau ni wimbo wa ‘Isikutonza Iyudi Chaum’, uliotungwa na aliyekuwa muungurumishaji wa gitaa la besi, Suleiman Mwanyiro, yeye alishiriki kwa kiasi kikubwa kupiga vyombo katika wimbo huo.

“Huo wimbo ukichezwa hata niwe wapi lazima nisimame kidogo niusikilize, ninaupenda sana kuliko wimbo mwingine, nilishirikishwa kuupiga,” anatamba Romario.

Anasema albamu za Msondo ambazo hawezi kuzisahau ni ‘Wanaume Tumeumbwa Mateso’ na ‘Kilio cha Mtu Mzima’.

Romario mbali na kipaji cha kupuliza tarumbeta, amejaliwa kipaji cha uimbaji ambapo mara nyingi ameonekana akiimba nyimbo mbalimbali.

Licha ya kazi yake ya muziki, Romario akiwa nyumbani kwake hupata faraja na familia yake yenye mke na watoto wanne.

Makala hii imeandaliwa kwa msaada wa vyanzo mbalimbali.

Mwandaaji anapatikana kwa simu namba: 0713331200, 0767331200, 0736331200 na 0784331200.