Usakatonge ulivyopora suala la Katiba mpya

DAR ES SALAAM

Na Pawa Lufunga

Ukweli unaojitetea ni kwamba kila Mtanzania mwenye ufahamu wa masuala ya kisiasa na uongozi anahitaji marekebisho ya Katiba yetu.

Awe serikalini, awe upinzani au asiye na ufuasi wa chama. Awe Mkristo, Muislamu au asiyeamini na awe wa kabila hili au lile; Tanzania Bara na hata Zanziabar.

Wabunge, Mahakama, wakulima na watumishi wote wanatamani kuona uboreshaji wa Katiba kuendana na mustakabali wa hali halisi.

Watawala wote tangu Mwalimu Julius Nyerere hadi Benjamin Mkapa walitamka neno ‘Katiba mpya’ na hatimaye Rais Jakaya Kikwete, mtu wa watu, akiwa madarakani alijizatiti kukata kiu ya Watanzania kwa kuwapa Katiba itakayotokana na maoni yao.

Akaunda Tume ya Katiba chini ya Jaji Joseph Warioba na ikakamilisha mchakato vema, ambapo maoni ya wananchi yalichakatwa na kuandaliwa Rasimu ya Katiba Mpya ikibeba matakwa ya wananchi, matamanio ya namna ya kuiongoza nchi yao na mahitaji yao.

Kizaazaa cha kukwamisha mchakato huu kilijiri baada ya Bunge Maalumu la Katiba kuanza kujadili maoni ya wananchi.

Vurugu zikazuka bungeni na kukwamisha mchakato huo mzuri kwa maisha bora kwa kila Mtanzania.

Pamoja na juhudi zote za nguli wa demokrasia Tanzania na Afrika Mashariki, Kikwete, mchakato wa Katiba mpya ulikwama huku makundi ya wanasiasa yakisutana na kutofautiana juu ya baadhi ya maeneo pendekezwa katika Katiba hiyo mpya.

Wakati wapinzani wakilalamika kuwa wabunge wa chama tawala (CCM) waliokuwa wengi bungeni walipora mchakato kwa kupuuza maoni ya Watanzania na kujaza matakwa na masilahi ya chama.

Wapinzani wakaamua kutoka bungeni na kuanza mikutano ya hadhara kupinga Katiba pendekezwa, wabunge wa CCM waliendelea na mchakato hadi kufanikiwa kuandika Katiba Pendekezwa chini ya uongozi wa Samuel Sitta, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba.

Baadhi ya madai yaliyoleta mtafaruku ni suala la Muundo wa Serikali, ambapo Rasimu ya Tume ilipendekeza Muundo wa Serikali Tatu uliotakiwa na wananchi wengi.

Suala la ukomo wa ubunge na mengine ya kiitifaki ambayo wanasiasa aidha kwa misingi ya vyama vyao au utashi binafsi, yaliwagusa, hivyo kuamua kufyekelea mbali maoni ya wananchi!

Wakaweka matakwa yenye unafuu kwao ambayo hata hivyo hayakufanikiwa kutokana na mchakato huo kuishiwa muda kwa kuingiliana na michakato mingine muhimu, ukiwamo Uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka 2014.

Hata hivyo, tangu wakati huo kiu ya kuisaka Katiba mpya imeendelea kuwapo kwa wafuatiliaji wa siasa za Tanzania.

Hata Rais wa Serikali ya Awamu ya Tano, John Magufuli alipotelekeza mchakato huo, ameendelea kulalamikiwa na makundi mbalimbali nchini kuhusu suala hilo la Katiba mpya.

Kinachosikitisha zaidi ni kwamba, licha ya vyama vyote zikiwamo taasisi na wadau mbalimbali kupenda au kuhitaji Katiba mpya, ukimwondoa Kikwete, watawala wengi wamekuwa wakiliona mwiba.

Wanaharakati na wataalamu wa siasa na utawala bora nchini wanasema watawala hawapendi mabadiliko ya Katiba kwa kuwa wananufaika na udhaifu wa Katiba iliyopo; kwamba kuibadili kunaweza kuwapa ugumu wa kutawala.

Aliyekuwa Mkuu wa Kitengo cha Sayansi ya Siasa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Dk. Bashiru Ally, aliwahi kusema kuwa Katiba ya sasa haikidhi matakwa ya Tanzania ya sasa kwani imekosa muafaka wa kitaifa.

Kwamba ni ya muundo wa Tanzania ya chama kimoja na inampa mtawala madaraka makubwa.

Kauli hii iliungwa mkono na wadau mbalimbali akiwamo Humphrey Polepole na wanasiasa wengine.

Kiama cha mahitaji haya ya kitaifa kinakuja ambapo leo walioikosoa Katiba ya sasa, baada ya kupata uongozi wa kuteuliwa, hawazungumzii Katiba mpya.

Wanapambana na wanaodai Katiba, wanasiasa wengi wamekaa kimya na hata walioungana huko awali kama UKAWA leo baadhi yao wanapambana kivyao kuidai Katiba hiyo huku wengine wakiwa kimya kana kwamba hawajui wanahitaji Katiba mpya au wanataka ya sasa iendelee.

Kibaya kuliko yote, CCM ambayo ndiyo iliratibu mchakato huo kwa gharama kubwa, viongozi wake wa juu wanaonyesha kutokuridhia mabadiliko ya Katiba huku Chadema na ACT – Wazalendo wakipambana kila mmoja kivyake kuidai.

Leo Katiba mpya, taifa la kizazi cha dijitali, limeigeuza kuwa vita ya kisiasa kati ya CCM na Chadema.

Vijana wasomi na hata watu wenye uelewa, uzoefu na ushawishi ndani ya serikali, vyama na jamii, ama kwa sababu ya kujipendekeza au kwa kukosa uzalendo, wanaungana na wasiojua maudhui ya mchakato huu kwa kuutengenezea propaganda ya u-CCM dhidi ya u-Chadema.

Acheni michezo hii jamani, hii si haki kwa Watanzania wasiojua mambo ambao bado wanastahili kutetewa na kusemewa matakwa yao.

Mapambano ya CCM na Chadema juu ya Katiba mpya, yupi ni mzalendo anasimama na hoja ya umma? Nani ni mpotoshaji anayesaka masilahi binafsi? 

Je, ni kweli suala la Katiba mpya linapaswa kupuuzwa? Namna ya kuyaendea mambo haya inahitaji tafakuri ya kina katika kuchambua ukweli na kuchukua hatua sahihi, kwani licha ya watawala wote kuona umuhimu wa mabadiliko ya Katiba, ni Rais Kikwete pekee ndiye aliyethubutu kutaka kumaliza jambo hili kwa kusimama na matakwa ya wengi.

Baada ya hapo na hata kabla, madai hayo ya Katiba mpya yamejeruhi Watanzania wengi, wapo walioambulia magereza, wapo walioteswa na wapo waliopata misukosuko hii au ile kutoka kwa watawala na vyombo vya dola kutokana na kuitisha mikutano ya kudai Katiba mpya.

Waziri Mkuu mstaafu, Jaji Joseph Warioba, akiteta jambo na Dk. Bashiru Ally, wakati akiwa Mhadhiri wa UDSM