DAR ES SALAAM

Na Mwalimu Samson Sombi

Katika uwanja wa siasa na uongozi Afrika, imekuwa ni nadra sana kwa wanawake kushika nafasi za juu za uongozi wa nchi ikiwamo urais.

Itakumbukwa kuwa nchi nyingi za Afrika zilitawaliwa na wakoloni kutoka mataifa ya Magharibi, kila utawala wa kikoloni ulikuwa na mfumo wake tofauti kutegemeana na nguvu ya upinzani na mazingira ya kijiografia katika nchi husika.

Vyama mbalimbali vya kisiasa vilivyopigania uhuru katika nchi hizo vilifanikiwa kuunda serikali na kuchagua mfumo wa uongozi uliotumika kutawala mataifa hayo yaliyokuwa na shauku kubwa ya kujitawala yenyewe.

Hata hivyo, kumekuwa na harakati mbalimbali Afrika za kutafuta usawa katika vyombo vya uamuzi; maarufu kwa jina la 50 kwa 50. 

Harakati hizo zimelenga kutoa nafasi sawa za uongozi kwa wanawake katika uwakilishi (wabunge) na ngazi mbalimbali.

Kama hivyo haitoshi, kumekuwa na mwamko mkubwa wa kisiasa kwa wanawake barani Afrika. Baada ya kuingia kwa mfumo wa vyama vingi miaka ya 1990, mfumo wenye lengo la kudumisha na kupanua demokrasia, wanawake wengi wameingia na wanaendelea kuingia katika duru za kisiasa, huku wengi wakifanikiwa kushika nafasi za juu, ikiwamo urais katika baadhi ya nchi za Afrika. 

Katika vyombo vya uamuzi pia kumekuwa na idadi kubwa ya wanawake, huku Rwanda ikitajwa kuwa na idadi kubwa ya wanawake katika uwakilishi ikilinganishwa na nchi nyingine tano za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC). 

Pamoja na kuingia kwa mfumo wa vyama vingi, bado mfumo huo unaendeshwa kwa kufuata na kuzingatia misingi ya Katiba ya kila nchi.

Katiba ni dira kuu inayotoa mwongozo wa nchi katika nyanja mbalimbali za kisiasa, kiuchumi na kijamii.  

Tanzania imeandika historia ya kuwa na Rais mwanamke tangu kupata uhuru Desemba 9, 1961 na baadaye kuzaliwa kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Aprili 26, 1964.

Tanzania imeundwa na Tanganyika na Zanzibar na ina pande mbili katika muundo wa uongozi. Kuna Serikali ya Muungano na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar.

Katika muundo wa Serikali ya Muungano, Rais akitoka Tanzania Bara, Makamu wa Rais lazima atoke Tanzania Zanzibar.

Aidha, Rais akitoka Zanzibar, Makamu wa Rais wa Muungano lazima atoke Tanzania Bara.

Samia Suluhu Hassan aliapishwa Machi 19, mwaka huu kuwa Rais wa sita wa Jamhuri ya Muungano, kufuatia kifo cha mtangulizi wake, Dk. John Magufuli, kilichotokea Machi 17, mwaka huu.

Rais Samia amekuwa Rais baada ya kuhudumu katika nafasi ya Makamu wa Rais katika Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Magufuli, kuanzia Oktoba 2015 hadi Machi 2021.

Mkuu huyo wa nchi amechukua nafasi kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 inayosema: “Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uongozi au kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili au kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais. Basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano na kwa masharti yaliyoelezwa katika Ibara ya 40 ya Katiba.”

Rais huyu wa kwanza mwanamke Tanzania, Machi 22, mwaka huu akiwa jijini Dodoma, aliwatoa Watanzania wasiwasi kuwa yeye ni mwanamke anayejiamini na hakuna kitakachoharibika chini ya uongozi wake.

Jumatatu ya Juni 28, mwaka huu, Rais Samia alitimiza siku 100 tangu aingie madarakani na kuelezewa kuwa amefanya maboresho katika sekta mbalimbali ikiwamo biashara na uwekezaji, uhuru wa vyombo vya habari na kuimarisha umoja wa kitaifa, haki za binadamu na uhusinao wa kimataifa.

Mbali na Rais Samia wa Tanzania, mwanamke mwingine aliyewahi kushika wadhifa wa urais ni Ellen Johnson Sirleaf wa Liberia.

Ellen alingia Ikulu ya Liberia kwa kuchaguliwa na wananchi na alifanikiwa kuongoza taifa kwa mihula miwili, kuanzia Januari 2006 hadi Januari 2018.

Katika uongozi wake, mama huyo alifanikiwa kuwaunganisha wananchi wa Liberia na kunyanyua uchumi wa taifa hilo ambao ulianza kudorora.

Rais huyo mstaafu alipata tuzo ya MO Ibrahim ya mwaka 2017 kwa kuinua uchumi na uongozi uliofuata na kuzingatia demokrasia.

Januari 22, 2018, Ellen alikabidhi uongozi kwa George Weah baada ya kuongoza nchi kwa miaka 12!

Ndani ya mwezi mmoja tangu aondoke madarakani, alitunukiwa tuzo ya uongozi uliotukuka ya MO Ibrahim akiwa Rais wa tano Afrika kupata tuzo hiyo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2007.

Malawi imewahi kuongozwa na Rais mwanamke, Joyce Banda, kuanzia mwaka 2012 hadi 2014 kufuatia kifo cha mtangulizi wake.

Katika uongozi wake, Joyce aliwahi kuhoji juu ya umiliki wa Ziwa Nyasa huku akidai kuwa ziwa hilo ni mali ya Malawi tofauti na ukweli kwamba ziwa hilo limechangiwa na nchi mbili; Tanzania na Malawi.          

Ivy Matsepe Casaburri amewahi kukaimu nafasi ya urais wa Afrika Kusini kwa siku nne Septemba 2005 wakati Rais Thabo Mbeki na Naibu Rais walipokuwa nje ya nchi.

Kisha Septemba 25, 2008, akateuliwa na Baraza la Mawaziri kuwa Rais wa mpito kwa saa 14 baada ya kujiuzulu kwa Mbeki, kisha akakabidhi madaraka kwa Kgalema Motlanthe.

Gabon, kuanzia Julai 2009 hadi Oktoba 2009, iliongozwa na Rais Rose Francine Rogombe katika kipindi cha mpito baada ya kifo cha Rais Omar Bongo. 

Mbali na Gabon, Mauritius imewahi kuongozwa na Rais mwanamke; Agnes Monique, kati ya  Machi 3, 2012 hadi Julai 21, 2015 kutokana na kujiuzulu kwa Rais Anerood Jugnuth hadi alipoapishwa Rais mpya, Kallash Purryag. 

Pia Agnes alikaimu tena nafasi hiyo baada ya Purryag kujiuzulu hadi alipoapishwa Amenah Gurlb. Hiyo ilikuwa kuanzia Mei 29 hadi Juni 5, 2015.

Catherine Sanuba aliwahi kukaimu nafasi ya urais Jamhuri ya Afrika ya Kati kuanzia Januari  2014 hadi Machi 2016.

Alikaimu nafasi hiyo baada ya kiongozi wa waasi, Michael Djotodia, kujiuzulu nafasi ya urais aliyokuwa amejiteua.

Miongoni mwa nchi chache za Afrika zinazoongozwa na wanawake ni Ethiopia kuanzia Oktoba  25, 2018 hadi sasa.

Mfuatiliaji wa masuala ya kisiasa, Situwarti Samandalo wa Arusha anasema katika uongozi, wanawake ni waadilifu na wachapakazi; wengi hawana tamaa ya madaraka na kujilimbikizia mali.

“Jamii inapaswa kuelewa kuwa uongozi ni uwezo na uadilifu na si suala la kuangalia jinsia ya mtu,” anasema Samandalo.

0755985966.