DAR ES SALAAM

Na Mwandishi Wetu

Pamoja na mawaziri Dk. Mwigulu Nchemba (Fedha na Mipango) na Dk. Faustine Ndugulile (TEHAMA) kusema kuwa Rais amesikia kilio cha Watanzania, mimi ninasema; “too good too late”!

Kwa heshima kubwa ninawaambia wao kuwa; “hilo ni tusi la kistaarabu la Waingereza.”

Watanzania wamekasirika tayari na wamelidharau Bunge kwa tukio/tamko hilo.

Haiwezekani kufanya uamuzi wenye nakisi kubwa sana ya uhalisia wa maisha ya Watanzania, kisha mawaziri, hususan Mwigulu, awaambie Watanzania kirahisi-rahisi tu kuwa Rais ati amesikia kilio chao, ati hayo sasa ni matakwa ya kisheria, ati Watanzania waifuate tu!

Je, hiyo ni kauli salama ya kutamkwa na waziri, tena wa Fedha na Mipango nchini Tanzania katika karne hii ya 21 ya sayansi na teknolojia?

Kama mzee mwenye jukumu la kulea na kushauri, je, Mwigulu anatambua ukuu wa wizara yake kitaifa na kimataifa?

Narudia, je, anatambua na kukiri juu ya ‘seniority’ ya Wizara ya Fedha na Mipango katika muundo mzima wa Baraza la Mawaziri kitaifa na kimataifa?

Je, anamkumbuka Waziri wa kwanza wa Marekani, Alexander Hamilton, kuhusu hekima na busara alizotumia katika ujenzi wa misingi imara/bora ya uchumi wa taifa hilo baada ya uhuru na ambayo Marekani wanaiheshimu na kuitumia hadi leo?

Kuhusu hilo, ninamshauri Mwigulu, mchumi mzuri tu, ajiongeze kwa kusoma kitabu kiitwacho ‘How rich countries got rich and why poor countries stay poor’ cha Erik Reinert, ukurasa wa 21 hadi 79 n.k.

Sasa tumuulize Mwigulu na wabunge, je, ni fedha kiasi gani zinapotea kwa ununuzi ya magari mengi aina ya V8 na magari hayo hayo ya viongozi kutwa nzima kushinda kwenye viyoyozi yakiwa yameegeshwa au kuzurura tu?

Hivi ni heshima kwa kila kiongozi kufuatwa na kupelekwa nyumbani kwa gari la serikali katika taifa maskini kama Tanzania!

Mbona taifa letu lilikwisha kutengeneza mwongozo wa ‘pool’ ya magari.

Kuwa viongozi wakopeshwe magari na watumie magari yao kwenda kazini na kurudi nyumbani.

Kuwa watumie magari ya serikali mara tu wanapowasiri ofisini kwa ratiba rasimi tu za kazi za serikali.

Je, nani aliyefuta utaratibu huo na kwa faida ya nani kama kweli tunayo nidhamu ya kusema kuwa kasungura (kabajeti) hakatoshi?  

Na je, hivi kweli tunajali suala la ukubwa wa serikali na idadi ya wabunge na wingi wa wilaya na mikoa Tanzania?

Je, kweli tunathamini vipaumbele vya mipango yetu ya maendeleo yenye sura ya utu?

Je, kwa baadhi ya maeneo hatuoni hilo linachochewa tu na woga wa baadhi ya wabunge kuogopa kupoteza nafasi zao za kuchaguliwa kwa kujitambua kuwa hawana mvuto tena jimboni na ndani ya jamii?

Angalia misururu ya magari katika misafara ati hata mbunge siku hizi kwenda kuzungumza na wananchi kwa kuandamana na DC na kamati za ulinzi na usalama! Kila kiongozi na gari lake peke yake!

Kila kiongozi siku hizi huko mikoani na wilayani utasikia akitafuta uhalali usiokuwa na maana kwa kuwaambia raia kuwa ‘hapa ninayo kamati ya ulinzi na usalama’, miye nauliza; ‘so what?’

Kama kweli si kujenga hofu kwa raia wema wa Tanzania na kuwanyima utulivu kwa kuwatisha kueleza kero zao na kuchangia kwa uhuru mpana mawazo yahusuyo vipaumbele vyao na jinsi ya kukuza moyo wa kujitolea katika shughuli za maendeleo yao!

Kushamiri kwa matumizi ya vyombo vya dola katika misafara kila kukicha nchini, muhimu viongozi wetu wawe na nidhamu stahiki kwa kuzingatia suala la ulinzi na usalama limo mikononi mwa kila raia/mwananchi.

Je, hilo nalo la wingi wa magari katika misafara halidhoofishi matumizi mazuri ya bajeti yenye kasungura kadogo?

Je, hatuoni kuwa kila kukicha viongozi wetu wanaua moyo wa wananchi kujitolea katika miradi ya maendeleo yao?

Je, viongozi wetu wanajali kufikiria juu ya kuwekeza na kulea vilivyo shughuli za utafiti na umuhimu wa viwanda vidovidogo nchini kwa lengo la kukuza uchumi na kuboresha uwezo wa kipato (purchasing power) kwa wananchi katika matumizi ya teknolojia za kisasa?

Je, kamati za Bunge zinapokwenda ziarani kukutana na wananchi vijijini, hivi kweli wabunge huwa wanadhamiria “kwenda kujifunza” juu ya vyanzo vya /sababu za kero za maendeleo ya hao wananchi, hivyo kuthamini maoni yao, au ni mwendelezo wa kufikiri tu kuwa mwananchi wa leo bado ni mbumbumbu na mila na desituri zao hazina uhusiano wa maana na maendeleo katika maeneo yao?

Je, viongozi wetu kweli hilo linawagusa vilivyo!

Hebu tuangalie idadi ya magari V8 yaliyopo serikalini na taasisi zake kulinganisha na Toyota Hardtop (gari za kazi) na tuelezwe gharama zinazotumika kununua V8 na umuhimu wake kwenda kuratibu miradi ya maendeleo vijijini nchini Tanzania na ‘dress codes’ za viongozi wanapokwenda kuzungumza na wananchi vijijini katika shughuli za kilimo, uvuvi, ufugaji na viwanda vidogo.

Hivi barabara na reli zinazotengenezwa ni kwa ajili ya kupitishia bidhaa za aina gani na zenye ubora gani kama bado hatujawekeza vya kutosha kwa Watanzania huko waliko katika kilimo, uvuvi na mifugo!

Je, tunajua uhusiano wa reli na usalama wa taifa letu au bado tumeganda kwa kufikiri tu kwamba usafiri wa reli ni anasa!

Mfugale, moja ya sifa kuu katika kumkumbuka, ni usanifu wa barabara na madaraja. 

Je, tunayo nidhamu stahiki ya kuthamini juu ya mchango wa madaraja katika ulinzi na usalama na ukuzaji/uimarishaji wa uchumi wa taifa letu?

Ni kwa nini wabunge na watendaji nchini Tanzania hawaonekani kujali/kujuta juu ya kukatikakatika kwa mawasiliano mikoani, wilayani na vijijini kila wakati wa masika!

Je, tunapoteza mapato ya kuboresha bajeti zetu kiasi gani kwa makusudi tu ya kuwa na miundombinu dhaifu nchini Tanzania na wakati mwingine tunaharibu barabara zetu za lami kwa makusudi kupitisha malori ya wakubwa juu ya hizo barabara?

Nini maana ya ‘repairs’, yaani ukarabati wa barabara zetu tena wakati mwingine katika maeneo yaleyale kila baada ya muda mfupi tu!

Je, Mwigulu na wabunge hili linawagusa kiasi gani hasa kwa kuzingatia gharama kubwa za ujenzi wa barabara za lami?

Leo hii tuulizane, hayo malori yanayoendeleza kufupisha uhai (life span) katika barabara zetu ni ya akina nani nchini Tanzania na yana uhusiano gani katika kutelekezwa kwa reli, bandari na meli zetu na wakati mwingine kung’olewa kwa mataruma na kuanguka hovyo kwa mabehewa?

Je, Mwigulu na wabunge wetu wanalo lipi la kutueleza katika hujuma hizi za kusababisha kilio kuwa kasungura hakatoshi, eti busara ni kupandisha bei za mafuta ya magari na kuanzisha tozo ya kodi katika simu?

Kweli, ni jambo jema leo hii tunakarabati bandari na meli zetu.

Hivi, huwa tunajiuliza ilikuwaje tukatelekeza tena kwa mbwembwe za hovyo tu kuwa “kubinafsisha tena haraharaka” ikiwa ni pamoja na kuua viwanda vingi tu nchini?

Je, tunaona furaha gani leo hii kuvaa mitumba ya nguo na viatu?

Mwigulu na wabunge kwa ujumla wanapokimbilia tozo ya kodi kwenye simu, je, wanakumbuka juu ya uamuzi wa hovyo uliowahi kufanyika bungeni na kusababisha madhara ambayo makovu yake ni aibu tupu leo hii?

Kwa mfano, Tanneries, Urafiki, Mutex, General Tyre, viwanda vya dawa n.k, viko wapi kuhusiana na ajira na vyanzo vya mapato?

Ni kiasi gani tunatumia mazao ya viwanda vya nyumbu JKT, Mzinga (JWTZ), Magereza na Nguvukazi ya vijana wa JKT katika kuboresha vyanzo vya mapato katika halmashauri Tanzania?

Je, usindikizaji wa makinikia na michezo michafu katika tanzanite yote hayo wabunge wanalo lipi la kuwaeleza Watanzania katika Tanzania yetu kujiimarisha katika uchumi wa kati au nalo wanasubiri kuelekezwa na Rais ambaye kwa tabia zilizopo sasa ati sasa ndiye pekee mwenye akili kubwa katika kubuni mipango ya ujenzi wa uchumi imara na endelevu, yaani ati ndiye ‘the only think tank Tanzania has’!

Katika hili, narudia kuhimiza kusomwa kwa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, sehemu ya pili, ibara ya 8 (a, b, c, d) hayo na mengine ndiyo baadhi ya maeneo yanayopaswa kumsumbua Mwigulu na wabunge wenzake kwa ujumla katika ujenzi wa uchumi imara kwa kuheshimu na kulea vilivyo maeneo yanayochachamua/chochea (stimulate) uchumi wa taifa letu.

Angalia mrundikano wa wanafunzi madarasani kwa uwiano wa walimu na wanafunzi.

Angalia makazi ya walimu na watumishi wa hospitali na vituo vya afya na zahanati.

Walio wengi huko mijini/vijijini wanapanga na kusafiri kwenda kazini wakiwa wanatokea katika makazi duni n.k. kwa kulipwa mishahara isiyokidhi viwango vya maisha bora.

Langu ni kuwaomba tu akina Mwigulu wawe makini sana katika kulinda heshima ya mafanikio ya mipango ya maendeleo iliyopo na watumie mbinu shirikishi katika kutafuta vyanzo vya mapato na wazingatie matumizi mazuri ya rasilimali zilizopo.

Watanzania kwa asili yao ni watu wapole, waungwana sana na wenye mapenzi mema kwa viongozi wao ila hawapendi kuburuzwa. 

Pindi wanapoona misingi ya utu wao, heshima yao wao n.k. vinatikiswa kwa kauli tatanishi, basi wahi kwa kutumia hekima na busara kama Mfalme Suleiman, watatafuta namna ya kuwasilisha hisia/maoni yao katika ngazi husika nchini.

Mungu Ibariki Tanzania.

Kasori S. H.

Katibu mstaafu wa Mwalimu J. K. Nyerere

By Jamhuri