Exif_JPEG_420

DAR ES SALAAM

Na Aziza Nangwa

Mamia kama si maelfu ya wafanyabiashara waliokuwa wakiendesha shughuli zao ndani na hata pembeni mwa Soko la Kimataifa la Kariakoo wameanza maisha katika masoko mengine jijini Dar es Salaam.

Wafanyabiashara hao wamelazimika kuondoka Kariakoo baada ya soko hilo kuwaka moto Ijumaa ya Julai 9, mwaka huu; na sasa wanapisha ukarabati ambao bado haujaanza.

JAMHURI limekuwa likifuatilia maisha yao mapya, wengi wakiwa wamedumu Kariakoo kwa miongo kadhaa, na kuwa ‘wenyeji’ wa eneo hilo.

Ni mateso, usumbufu Soko la Kisutu

Kisutu ni moja ya masoko yaliyopewa jukumu na Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam kupokea wafanyabiashara kutoka Kariakoo.

Miongoni mwa waliohamia Kisutu ni wafanyabiashara wa mizani na sasa wanaulalamikia uongozi wa soko hilo kwa kutowapa eneo la kufanyia kazi.

Mmoja wa wafanyabiashara hao, Abdallah Bashiru, anasema hadi sasa hawajapata sehemu ya kufanyia biashara sokoni hapo, wakielezwa kuwa hakuna eneo la ‘bidhaa za vyuma’.

“Uongozi unatuzungusha na kutupiga danadana. Wenzetu wanaendelea na biashara, lakini sisi hatuna eneo la kuweka bidhaa zetu. Tumekuwa tukihamishwa kutoka eneo moja kwenda jingine.

“Sasa wametupeleka Machinga Complex wala hatujui kama tutapata nafasi! Tukishindwa tutalazimika kwenda kwa mkuu wa mkoa,” anasema Bashiru.

Bashiru anasema wamekwenda kuangalia mazingira ya Machinga Complex kama watapokewa na kupatiwa nafasi na ikishindikana, waombe ufafanuzi serikalini.

Hofu yao ni kwamba huenda uongozi wa Soko la Machinga Complex nao hautaki vyuma.

Kuhusu hilo, Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, amesema ni vema viongozi wa soko kujipanga mara moja kuwapa sehemu ya biashara kama walivyowapa wafanyabiashara wa mazao.

Kwa upande mwingine Makalla amewapa wiki mbili wafanyabiashara ndogondogo waliopo nje ya Soko la Kisutu, kando ya kituo cha mwendokasi cha DIT, kuhamia mara moja ndani ya soko. 

Makalla amefanya ziara kufutatilia changamoto zinazowakabili wafanyabiashara waliotoka Kariakoo kwenda Kisutu na Machinga Complex, na kuahidi kuzitatua haraka iwezekanavyo.

Akiwa Kisutu, mbali na wafanyabiashara wa mizani, wenzao wa samaki na dagaa wamelalamika kuwa hawana sehemu ya kuhifadhia bidhaa zao na tatizo la umeme.

Wanasema mfumo wa lifti unaosaidia kuwafikisha wateja ghorofani husimama mara kwa mara.

“Hayo tutayashughulikia. Kazi kubwa kwa sasa ni kuhakikisha wafanyabiashara wote wanapata maeneo.

“Wapo wanaotaka kujengewa vizimba. Jamani, serikali imejitahidi sana, kwa hiyo hili la vizimba kwa mliohamia Soko la Kisutu, mjitolee wenyewe. Kaeni na uongozi waone namna gani mtarudishiwa fedha zenu kidogo kidogo,” anasema Makalla.

Makalla ameahidi kujenga paa Machinga Complex kuwahifadhi wafanyabiashara wageni na kuboresha mazingira ya kazi, huku akitoa miezi miwili ya bure.

“Hapa tunastahili pongezi kwa kuwa kwa miezi miwili, kila mtu angetakiwa kulipa Sh milioni 1.2,” anasema. 

Amewataka viongozi wa Kisutu na Machinga Complex kutoa ushirikiano na utatuzi wa changamoto zote, kisha kupanga utaratibu maalumu kuhakikisha wafanyabiashara wote wanaingia ndani ya masoko hayo badala ya kuzagaa nje. 

“Mkiwa ndani, mimi nitakuwa ofisa masoko wenu. Nitatangaza biashara zenu kote ili wateja wajue namna ya kuwapata kwa urahisi,” anasema Makalla.

Anasema kitendo cha wafanyabiashara wote kuwa ndani ya masoko kitaleta ushindani wa kweli wa kibiashara na kuinua ufanisi.

Wamzawadia Mkuu wa Mkoa

Mwenyekiti wa Soko la Kariakoo, Rashid Shabani, ameipongeza serikali kwa kuhakikisha wafanyabiashara wanapata faraja katika kipindi hiki kigumu.

Anasema walipopata matatizo hawakudhani kama serikali ingewajali kwa kiasi hiki na hata kukesha nao kuhakikisha utaratibu wa wao kuhamia masoko mengine unafanikiwa. 

“Wametupigania kuhakikisha tunapata eneo la kufanyia biashara. Hatukutarajia kurejea na kuishi kama awali,” anasema Shabani. 

Anasema wamepata ushirikiano wa hali ya juu, kwani walipofika Machinga Complex, tofauti na walivyodhani, wamepokewa vizuri, hivyo kufarijika japokuwa wamepoteza mali nyingi.

Anasema japokuwa hali zao ni mbaya, lakini kwa kuthamini mchango wa viongozi hao kwa maisha na biashara zao, wameamua kutoa zawadi za bidhaa wanazouza kwa Mkuu wa Mkoa, Makalla.

“Hatuna kitu, lakini tumetoa zawadi ndogo kama ishara ya furaha yetu. Uongozi wa Mkoa umegusa maisha yetu kwa kutupatia msaada wa haraka. 

“Kupewa nafasi ya kuendelea na biashara ni kitu ambacho hatukukitarajia, tulidhani tungeambiwa tukakae nyumbani kusubiri soko lifanyiwe ukarabati,” anasema Shabani.

Hali ni tofauti kwa wafanyabiashara wenyeji wa Machinga Complex, ambapo mmoja wao, Serenga Hamisi, anautupia lawama uongozi akisema huwanyanyasa kwa kuwatoa kwenye meza zao kuwapisha wageni kutoka Kariakoo. 

“Hatuna raha tena ya biashara, tunaondolewa kwenye sehemu zetu na kupelekwa sehemu nyingine kuwapisha wageni bila hata majadiliano! Hatuwakatai wageni, lakini kitendo hiki cha viongozi si sahihi,” anasema Hamisi.

Omary Mustapha anayetoka Kariakoo, anawataka viongozi kuwaondoa wafanyabiashara wote bila kuacha wengine wakizagaa katika mitaa ya karibu na soko lililoungua. 

Wafanyabiashara wenye vioski vya maziwa wanasema polisi wanawazuia, kuwakamata na kuwatoza faini kubwa kwa kuwasha gesi kwa ajili ya kupikia.

Katika hatua nyingine, Makalla amepokea kwa furaha zawadi aliyopewa na wafanyabiashara hao.

By Jamhuri