NA MOSHY KIYUNGI
TABORA

Sauti ya Hemed Maneti ‘Chiriku’ kila isikikavyo kupitia
redio, nyoyo za baadhi ya wapenzi wa muziki wa dansi
hupatwa na simanzi kubwa.
Nguli huyo alifariki dunia Mei 31, 1991 akiwa katika
Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar es Salaam ambako
alikuwa amelazwa baada ya kuugua kwa muda mrefu.
Mwili wa Maneti ulizikwa kijijini kwake ukisindikizwa na
umati mkubwa wa mashabiki na viongozi mbalimbali wa
Chama Cha Mapinduzi na serikali yake kutoa heshima
zao za mwisho.
Miaka 28 imepita akiwa ndani ya kinywa cha ardhi, sauti
yake kila isikikapo, huonyesha ni jinsi gani mwanamuziki
huyo alivyokuwa na talanta kubwa katika utunzi na
uimbaji.
Maneti aliyepachikwa jina la ‘Chiriku’

, alikuwa kiongozi na

mwimbaji wa Vijana Orchestra kwa miaka 16.
Aliacha pengo kubwa si kwa bendi yake tu, bali kwa taifa
zima, ambalo bado lilikuwa likiuhitaji mchango wake kwa
hali na mali.
Maneti alizaliwa katika Kijiji cha Mamboleo, wilayani

Muheza, Tanga mwaka 1954.
Kipaji cha utunzi na uimbaji alichojaliwa na Al-Qudusi,
kilionekana wazi katika tungo zake maridhawa.
Alikuwa mwanasiasa safi ambaye hakuhutubia kwenye
mikutano ya siasa, bali aliuonyesha uanasiasa wake
kupitia jukwaa la muziki.
Alitunga nyimbo nyingi za siasa na moja kati ya kazi zake
bora ni ule wimbo wa ‘Ali Hassan Mwinyi apewe kura za
ndiyo’ alioutunga mwaka 1985.
Katika kumpigia debe aliyekuwa mgombea pekee wa kiti
cha urais wa Jamhuri ya Muungano kwa wakati huo, Rais
mstaafu wa Awamu ya Pili, Alhaji Ali Hassan Mwinyi.
Wimbo huo ulipigwa kila siku na Radio Tanzania (RTD)
wakati huo, ukatokea kupendwa na watu wakiwemo
viongozi wa kisiasa na ubora wa wimbo ulionekana katika
Uchaguzi Mkuu wa mwaka 1990 pale bendi yake ya
Vijana ilipoukarabati na kuutumia tena kwenye kampeni
za Rais Mwinyi na Rais wa Zanzibar, Dakta Salmin
Amour Juma.
Maneti hakuwa nyuma katika masuala ya ukombozi
pamoja na kutetea amani na alidhihirisha wazi kwamba ni
mtetezi wa amani alipotunga wimbo safi wa ‘Magaidi wa
Msumbiji’ mwaka 1987.
Wimbo huo pia ulikuwa kipenzi cha watu, ni moja kati ya
kazi za kukumbukwa.
Nyimbo nyingine za siasa ni ‘Muungano umekamilika’
,

‘Rushwa adui wa haki’
,
‘Vijana nguzo na jeuri ya Chama’
,

‘Operesheni Maduka’
,
‘Mwenge umulike nje ya mipaka ya

Tanzania’
,
‘Tamasha la Vijana Moshi’ na nyinginezo

nyingi.
Maneti ‘Chiriku’

, alionyesha kipaji chake pia katika tungo

za mapenzi kiasi kwamba vibao vyake vingi bado

vinawakuna wengi hadi sasa.
Miongoni mwa vibao hivyo alivyotunga na vingine
kutungiwa na kuviimba, ni ‘Niliruka ukuta’ (sehemu ya I
na II mwaka 1975),

‘Mary Maria’
,
‘Maggy wanipa mateso’
,

‘Kosa la wazazi’
,
‘Chiku saizi yangu’
,
‘Ilikuwa lifti tu’
,

‘Aza’
,
‘Pili wangu nihurumie’ (ulitungwa na Abdallah

Mensah),

‘Penzi halina umaarufu’
,
‘Penzi haligawanyiki I

na II’
,
‘Heshima ya mtu kuoa na kuolewa’
,
‘Chaurembo’

na nyinginezo.
Pia aliimba nyimbo nyingi za kijamii kama vile
‘Masimango’
,
‘Mwanaume gani anasuka nywele’
,
‘Nsabi’
,

‘Kamata Ooh Sukuma’
,
‘Matata Matata’
,
‘Watoto wanalia

sana’
,
‘Mudinde acha fitina’
,
‘Ooh Masido’
,
‘Amba kawa

baharia’
,
‘Acha acha ngoma jirekebisheni’
,
‘Wifi zangu’
,

‘Bujumbura’ na ‘Safari yetu Zambia’ ambao
haukurekodiwa.
Maneti alikuwa ni mvumilivu na wala hakubweteka na
umaarufu kwa muda wote aliokuwa na bendi ya Vijana
Orchestra. Hakujaribu hata siku moja kuihama bendi
hiyo.
Wanamuziki wengi walikuwa wakiingia bendi hiyo na
kutoka, lakini kamwe Maneti hakutingishika licha ya
vishawishi vingi kutoka bendi kadhaa za hapa nchini
ambazo zilikuwa zikimtafuta kila kukicha.
Katika safari yake katika muziki alijiunga na bendi ya
Vijana Orchestra mwaka 1974 akitokea katika bendi ya
TK Lumpopo iliyokuwa ikiongozwa na mwanamuziki
mkongwe nchini Juma Kilaza.
Maneti akiwa katika bendi ya Vijana Jazz, alipewa nafasi
ya kiongozi msaidizi wa bendi hadi mwaka 1982
alipoteuliwa kuwa kiongozi wa bendi.
Bendi hiyo ya Vijana Jazz iliyokuwa na makao yake

makuu Kinondoni, iliweza kupitia kwenye mitindo mingi
ambayo kati ya hiyo ikiwa ni ubunifu wake.
Mitindo hiyo ni kama vile Takatuka, Koka koka, Heka
heka, Pamba moto I na II na Pamba moto shambulia hot
dance.
Akakubalika na kundi kubwa la wapenzi na mashabiki,
hivyo kurundikiwa shehena ya majina yakiwemo ya
‘Simba Mwendapole’ na ‘Chiriku’

, jina ambalo lilimkaa
mpaka likaonekana kama moja ya majina yake halisi.
Pia aliweza kupitia ngazi kadhaa za uongozi katika siasa
kama mjumbe wa Baraza la Utekelezaji la Taifa la Umoja
wa Vijana wa CCM.
Kutokana na uongozi wake imara bendi hiyo haikuyumba
chini yake hata pale wanamuziki wake nyota walipokuwa
wakihama. Baadhi ya wanamuziki ambao waliihama
bendi hiyo katika vipindi tofauti na kusababisha mapengo
makubwa katika bendi hiyo ni Cosmas Chidumule,
George Mpupua, Hassan Dalali, Komandoo Hamza
Kalala ambaye aliondoka na baadaye kurejea tena kabla
ya kuihama tena na kwenda Washirika Tanzania Stars
‘Watunjatanjata’ pamoja na Eddy Sheggy na Adam
Bakari ‘Sauti ya Zege’ waliokuwa nyota katika bendi hiyo.
Wengine ni Kida Waziri, Mohammed Shaweji, Athumani
Momba, Jerry Nashon ‘Dudumizi’

, Mohammed Gotagota
na Msafiri Haroub, ambao nao kama Kalala, waliihama
bendi hiyo na kurejea tena.
Maneti bado anakumbukwa na baadhi ya wanamuziki
waliokuwa naye akiwemo Rashid Pembe, alikaririwa
akisema kuwa pengo aliloliacha Maneti si rahisi kuzibika.
Kipindi cha miaka ya 1990 baadhi ya wanamuziki
waliokuwa wanaunda Vijana Jazz walikuwa na
utamaduni wa kutembelea kaburi la Maneti kila mwaka

kijijini Mamboleo.
Katika ziara hiyo pia walipata fursa ya kuwajulia hali
wazee na ndugu wa marehemu.
Utaratibu huo kwa sababu zisizoeleweka, umetoweka.
Mwaka 1994 bendi hiyo baada ya kupigiwa kelele sana
na mwandishi mmoja mkongwe wa burudani, ilitoa
albamu ya kumbukumbu ya Maneti iliyoitwa ‘Homage de
Maneti’ ambayo ilikuwa na baadhi ya nyimbo zilizotamba
enzi za uhai wake.
Kwa sasa familia yake inaongozwa na bintiye Komweta
‘Khairat’ na mwanawe wa kiume Maneti Hemed.
Komweta ‘Khairat’

, amerithi mikoba ya baba yake ya
kuimba. Yupo katika bendi ya Vijana Jazz, anaonekana
kuwa mhimili mkubwa katika kuhakikisha jina la baba
yake halipotei katika medani ya muziki nchini.
Binti huyo ya Hemed Maneti aliwahi kuwashukuru
wanamuziki wakongwe waliopata kuimba na baba yake
pamoja na wanahabari ambao bado wangali
wanaukumbuka mchango wa mwanamuziki huyo nguli
nchini.
Uongozi wa umoja wa vijana wa chama hicho uliahidi
kuwasomesha watoto wa marehemu hadi vyuoni.
Ahadi hiyo iliyotolewa kijijini Mamboleo wakati wa
mazishi, haikuwahi kutekelezwa hata mara moja ambapo
Khairat mwenyewe aliishia kidato cha tatu baada ya
mama yake Stella kufariki dunia huku kaka yake, Maneti,
akishindwa hata kuuona mlango wa sekondari.
Mungu azidi kung’arishia nuru yako huko uliko. Amina.

Mwandishi wa makala hii anapatika kwa namba:

0713331200, 0784331200 na 0767331200

Mwisho

By Jamhuri