Ndiyo kusema kwamba elimu inayotolewa sasa ni kwa ajili ya
wachache tu wenye uwezo wa mitihani kuwazidi wengine;
inawafanya wale wanaofanikiwa wajione kuwa wakubwa, na
kuwafanya wale walio wengi wakitamani kitu ambacho
hawatakipata daima.
Inawafanya walio wengi wajifikirie kuwa wanyonge, na kwa hiyo
hawawezi kuunda wala taifa la usawa tunalotaka kulijenga wala
fikara zinazoelekea kwenye taifa lenye usawa.
Kinyume chake, elimu hiyo inawashawishi kuundwa kwa taifa
lenye tabaka, la ubwana na utwana, katikia nchi yetu.
Jambo la pili ni muhimu vile vile, nalo ni kwamba elimu ya
Tanzania inawatenga wale wanaosoma mbali na wananchi
wanaowasomesha. Hii ni kweli hasa katika shule za Sekondari,
ambazo karibu zote ni za wanafunzi kukaa huko shuleni.
Lakini ni kweli vile vile hata katika shule chache za praimari,
ijapokuwa hivi karibuni tumebadili kidogo mipango yetu.
Tunawachukua watoto wakiwa na umri wa miaka 7 kutoka kwa
wazazi wao, na tunawafunza masomo ya darasani saa 71/2
nzima kutwa.
Katika miaka michache iliyopita tumejaribu kuyafanya mafunzo
haya yafanane na hali ambayo watoto hao wanaiona. Lakini
shule yenyewe kila mara iko mbali, siyo karibu na jamaa au
kijiji.
Shule ni mahali ambapo watoto huenda kwa matumaini, yao
nay a wazazi wao, kwamba wakifanikiwa haitakuwa lazima
kwao kuwa wakul;ima au kuishi vijijini.
Wale wachache wanaoingia shule za Sekondari hupelekwa
mbali na makwao; wanaishi maisha ya pekee, wakiwa na
ruhusa ya kwenda mjini kujistarehesha, lakini kazi za mji au kijiji
kile hazilingani na maisha yao hasa, yaani maisha wanayoishi
wakiwa katika uwanja wa shule.

Baadaye wachache huenda Chuo Kikuu. Wakiwa na bahati
kuingia Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, wanaishi katika
nyumba za raha, wanalishwa vizuri na kusoma sana kupata
digrii zao.
Watakapopata digrii hiyo, wanajua mara moja kwamba
watapokea mshahara kiasi cha Shillingi 1,100/- kwa mwezi.
Hiyo ndiyo shabaha waliyo nayo, ndivyo walivyofunzwa wawe
nayo.
Wanaweza vile vile kuwa na haja ya kuuhudumia umma, lakini
fikara zao za huduma zinatokana na heshima na mshahara
ambao mtu aliyehitimu Chuo Kikuu anaweza kuupata.
Mshahara na hadhi vimekuwa haki inayotolewa na Digrii.
Tunakosea tukiwalaumu vijana wetu kwa fikara kama hizi.
Kijana aliyehitimu sasa hivi kutoka Chuo Kikuu ametumia
sehemu kubwa ya maisha yake mbali kabisa na watu wa
Tanzania. Inawezekana wazazi wake ni maskini, lakini yeye
kwa kweli hakuonja umaskini ule.
Hafahamu maisha ya mkulima maskini hasa yako namna gani.
Ataona raha zaidi kuishi na watu wenye elimu, kuliko kuishi na
wazazi wake mwenyewe. Kijana huyu amekwenda nyumbani
wakati wa likizo tu, na hata wakati huo wazazi na jamaa zake
wenyewe wamesisitiza fikara zake za ubwana na kudhani
kwamba ni makosa yeye kuishi na kufanya kazi kama mtu wa
kawaida.
Maana kweli ni kwamba watu wengi wa Tanzania
wamemhesabu mtu mwenye elimu kuwa na thamani sana hata
hawezi kuishi maisha ya taabu wanayoishi watu wengine.
Jambo la tatu ni kwamba mpango wetu wa elimu wa sasa
unawafanya wanafunzi wafikiri kwamba mambo yote ya maana
hupatikana katika vitabu, au hutoka kwa ‘watu wenye elimu’,
yaani wale waliopata elimu ya darasani.
Ujuzi na hekima ya wazee wengine hudharauliwa, na wao
wenyewe hujihesabu kuwa maamuma wasiofaa lo lote. Kwa
kweli si mpango wa elimu peke yake unaoleta mawazo kama

hayo.
Hata Serikali na Chama pia huwachagua watumishi kwa
kufuata ‘School Certificate’ au digrii, na kadhalika. Kama kijana
anazo hati hizo tunadhani kwamba anaweza kufanya kazi
fulani. Hatungojei tukamjua mawazo yake, tabia yake, au
uwezo wake mwingine, midhali tu amefaulu katika mtihani.
Kama mtu hana hati hiyo tunadhani kwamba hawezi kufanya
kazi, tunasahau kabisa habari ya ujuzi na mazoea yake ya kazi.
Kwa mfano, hivi juzi juzi nilimtembelea mwananchi mmoja,
mlima tumbaku hodari sana. Lakini kama ningejaribu kumwajiri
mtu huyu Serikalini awe Bwana Shamba wa tumbaku
ningekwama, maana hana hati ya kusomea darasani.
Kila kitu tufanyacho kinatilia mkazo masomo ya darasani, na
kudharau sana hekima ambayo mara kwa mara huipata watu
wanaotumia akili, waume kwa wake, jinsi wanavyoendelea
kuishi, hata kama hawawezi kusoma au kuandika.
Kusema hivi maana yake siyo kwamba mtu ye yote anaweza
kufanya kazi yo yote, mradi tu amekuwa mzee mwenye hekima,
wala si kusema kwamba hati za elimu si lazima. Wakati
mwingine watu wetu wamefanya makosa ya kufikiri hivyo kwa
sababu tu ya kuchukia majivuno ya wale wenye elimu.
Mtu hawi na busara tu kwa sababu ni mzee; mtu hawezi
kuendesha kiwanda kwa sababu tu ameajiriwa kama kibarua au
mtunza stoo kwa muda wa miaka 20 iliyopita. Lakini vile vile
pengine atashindwa kufanya kazi hiyo hata akiwa na digrii ya
biashara.
Huyu wa kwanza anaweza kuwa na uaminifu na uwezo wa
kusimamia wenzake, huyu wa pili huenda ana uwezo wa
kuanzisha na kupanga hesabu zake. Lakini, kama tunataka
kiwanda hiki kifanikiwe, kiwe cha kisasa, na kulifaidia Taifa, basi
meneja anatakiwa awe na sifa zote hizi mbili. Ni makosa vile
vile kufikiria kisomo ndicho kila mitu.
Na hivyo ndivyo ilivyo katika ujuzi wa kilimo. Wananchi wetu ni
wakulima wa siku nyingi. Ufundi wanaotumia ni matokeo ya

juhudi ya miaka mingi ya kutafuta riziki; na hata sheria na miiko
wanayoifuata ina sababu zake.
Haitoshi kumkashifu mkulima mzee kwa kudhani kuwa
anatumia maarifa ya kale. Hatuna budi kujaribu kufahamu kwa
nini anafanya jambo fulani, tusidhani tu kuwa ni mpumbavu.
Wala sisemi kwamba maarifa yake yanafaa katika siku zijazo.
Inawezekana kuwa maarifa ya asili yalifaa kwa uchumi wa siku
zili yalipotumiwa, kufuata ujuzi uliokuwepo. Lakini siku hizi
tunatumia vifaa tofauti, na tuna mipango tofauti ya kumiliki
ardhi.
Haiwezekani sasa kulima shamba kwa muda wa mwaka mmoja
au miwili, na halafu kulitekeleza kwa muda wa miaka 20, ili
rutuba irudi tena. Kutumia plau la ng’ombe badala ya jembe, au
hata kutumia trekta katika sehemu zingine, maana yake siyo
peke yake kubadili namna ua kulima.
Yatakiwa yaweko mabadiliko katika mpango wa kazi, ili
kuhakikisha kwamba chombo hiki kipya kinalima kwa faida
zaidi, na pia maarifa haya mapya hayaharibu kwa haraka ardhi
yetu wala misingi ya usawa wa taifa letu.
Kwa hiyo nasisitiza tena kwamba vijana wetu hawana budi
wajifunze kuheshimu hekima ya wakulima wazee wasiosoma
na kuelewa maarifa ya kisasa, na kwa nini maarifa hayo
yatatumika.

<<<<< Itaendelea>>>>>

Please follow and like us:
Pin Share