NA MICHAEL SARUNGI

Ubingwa wa Kombe la Chalenji walioupata vijana wa Tanzania chini ya miaka 17 (Serengeti boys) unapaswa kuwa chachu ya kutwaa ubingwa wa Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), mashindano yanayotarajiwa kufanyika hapa nchini mwakani.

Wakizungumza na JAMHURI baada timu hiyo kutawazwa mabingwa wa Afrika ya Mashariki na Kati wamesema ushindi huo ni ishara njema kwa Tanzania itakayokuwa mwenyeji wa michuano hiyo mikubwa Afrika.

Kocha wa Singida United, Mholanzi, Hans van der Pluijm amesema kuanzia sasa vijana hao wanapaswa kuangaliwa kwa umakini ili mwakani waweze kutoa ushindani unaotarajiwa.

Amesema ni jukumu la Shirikisho la Soka nchini (TFF) kwa ushirikiano wa karibu na  Serikali na  wadau wengine kuanza kuja na mbinu mbadala kuhakikisha timu inapata mechi nyingi za majaribio kabla ya kuanza kwa michuano hiyo.

Amesema kila mmoja aliona uwezo ulioonyeshwa na timu za Ghana, Mali, Guinea na Niger katika fainali za AFCON zilizofanyika Gabon na  kupata tiketi za kuliwakilisha Bara la Afrika kwenye fainali za dunia zitakazofanyika mwaka huu nchini India.

Amesema bila ya maandalizi ya uhakika Serengeti Boys  inaweza kujikuta ikitolewa katika hatua za makundi kugeuka watazamaji.

Naye kocha wa zamani wa Toto Africans ya Mwanza, John Tegete, amesema maandalizi hayo yanapaswa kuanza mapema kutokana na ubora wa timu nyingine zinazotarajiwa kushiriki michuano hiyo.

Amesema endapo Serengeti Boys, hawatapewa maandalizi ya kutosha huenda ikakumbana na kile kilichoikuta timu ya taifa ya Gabon ilivyotia aibu katika michuano ambayo walikuwa wenyeji na kujikuta wanafungwa magoli 10 katika mechi tatu za hatua ya makundi na kuondolewa.

Amesema kuna uwezekano mkubwa wa vijana hao kufanya vizuri endapo watapewa maandalizi ya kutosha kwa kupewa michezo mingi ya kirafiki ya kimataifa itakayowajengea uzoefu kuweza kupambana na timu yoyote.

Amesema wadau wa michezo wanapaswa kuunganisha nguvu kuhakikisha vijana hawa wanaendelea kuwa sawa hadi wakati wa mashindano utakapofika na hilo litawezekana kwa uwepo wa kambi ya pamoja na michezo ya majaribio.

Amesema TFF inapaswa kuanza kutengeneza timu imara ambayo itatoa ushindani na si kuwa wasindikizaji wa mataifa mengine yenye uwezo mkubwa kisoka.

Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Yusuph Singu amesema Serikali kwa kushirikiana na mamlaka nyingine itahakikisha ustawi wa vijana hao kwa kutoa misaada ya hali na mali.

Singu ameiomba TFF kuhakikisha vijana hao wanaendelea kupewa mahitaji muhimu ili mwakani wawe wawakilishi wenye uwezo mzuri wa kuipeperusha vyema  bendera ya nchi katika michuano hiyo.

Kocha wa Serengeti Boys, Oscar Milambo, amesema mara baada ya ubingwa huo wamejipanga kuhakikisha vijana wanaendelea kuwa sawa tayari kwa mashindano yoyote yajayo kwa manufaa taifa.

Amesema kushinda kwao kombe la vijana wa Afrika  Mashariki na Kati (Cecafa) chini ya miaka 17 ni ishara njema kuelekea mashindano ya Afcon U17 yanayotarajiwa kufanyika hapa nchini.

Tanzania itaandaa Fainali za Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, baada ya kukabidhiwa wenyeji na Shirikisho la Soka Afrika (CAF) katika hafla iliyofanyika wiki chache zilizopita nchini Gabon; mashindano hayo yaliasisiwa miaka 32 iliyopita.

By Jamhuri