Ipo dhana kwa baadhi ya watu hapa nchini kwamba Serikali ni Kiongozi Mkuu wa Nchi, kwa maana ni Rais. 

Ni dhana ambayo mara kadhaa imezusha malumbano ya kisiasa na kijamii kwa fikra kwamba Rais ni mtu. Iko haja tena ya kuweka wazi Serikali ni nini na Rais ni nani katika nchi.

Ukitazama kwa ndani unaweza kuona ni dhana inayokinzana na utaratibu kwamba Serikali ni taasisi au chombo cha utawala katika nchi. 

Hizi ni fikra za baadhi ya wananchi katika mustakabali wa uongozi na utawala juu ya mambo ya kisiasa, kiuchumi na kijamii.

Katika lugha sahihi, yenye kueleweka na kukubalika na watu, Serikali ni chombo kikuu chenye mamlaka ya kutawala nchi kwa kutumia Katiba, sheria na taratibu ilizojiwekea. 

Nazungumzia Dola ambayo ni chombo chenye madaraka kamili ya kusimamia shughuli za utawala na siasa ndani ya nchi bila kujali ukubwa au udogo wa eneo.

Watu wanaobeba dhana kwamba Serikali ni kiongozi fulani si taasisi au chombo cha utawala, wamekuwa wepesi kubadilika kitabia katika shughuli zao za kila siku za kutafuta riziki. Utii wao kwa kiongozi mkuu wa nchi huwa wa shaka na kujenga nidhamu ya woga. Kwao Serikali ni mtu ( kiongozi).

Watu wanaotambua Serikali ni chombo cha utawala iliyowekwa kwa mujibu wa Katiba, sheria na taratibu walizojiwekea, wanakuwa na tabia njema na kutii mamlaka na madaraka yaliyopo. Wanajenga nidhamu ya dhati, na wala hawababaishwi na mabadiliko ya awamu ya Serikali.

Awamu ni mfumo wa kipindi maalumu cha utendaji jambo katika madaraka serikalini. Muda wa kiongozi mkuu wa kuwa madarakani huisha au kuondolewa au kufa na kiongozi mwingine mpya huingia kushika madaraka hayo, kwa mujibu wa Katiba ya nchi.

Katika muktadha huu, raia au wananchi ni wajibu wao kwa kila hali kuendelea kuheshimu, kuthamini na kuenzi utawala mpya. 

Utawala uenziwe kwa dhati si kwa woga, au kwa shaka shaka. Utawala unapokuwa katika hali na mazingira mema na mazuri hufanya kazi zake kwa umakini na wananchi wanapata matunda mazuri ya maendeleo.

Serikali ya Awamu ya Tano ya hayati Rais Dk. John Pombe Magufuli imepita, na Serikali ya Awamu ya Sita imeingia na ipo madarakani kwa mujibu wa Katiba ya nchi, chini ya Rais Samia Suluhu Hassan. Hii ina maana tumo katika zama mpya ya uongozi na utawala na kuendelea kuwa chini ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tangu mwaka 1964 hadi sasa. 

Hivi karibuni nimepata kumsikia Rais Samia Suluhu Hassan akisema wapo watu katika baadhi ya maeneo nchini wanafanya uhalifu kwa kutumia silaha na kuua watu na kuwapora mali zao. Na wengine kufanya wizi, hila na hujuma katika mali za taifa.

Matendo haya ni dalili ya kutaka kuvunja utulivu na amani iliyopo. Rais ameinyooshea kidole Polisi na kuvitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuwa macho. 

Polisi ndio wenye dhama kubwa ya usalama wa raia na mali zao. Chombo hiki kimetakiwa kukaza buti na kufumbua zaidi macho yao kukabiliana na uhalifu nchini.

Ukweli wa mambo, kidole kile cha Rais Samia hakilengi tu vyombo vya ulinzi na usalama, pekee, kinawalenga pia watumishi wa umma na raia wa kawaida hapa nchini. 

Watanzania wote tunatanabahishwa kwamba serikali ipo na ni hai. Wale wanaojaribu kutingisha kiberiti au kupima kina cha maji kwa mti, waache.

Watanzania ni wajibu wetu kutambua kwamba serikali yetu ina viongozi wakiongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ni mkuu wa nchi, kiongozi wa Serikali na Amiri Jeshi Mkuu. Anaposema jambo ni tamko, ni agizo, ni amri. Wale wanaojenga tabia ya kubeza waache.

Nchi au taifa halijengwi kwa mitutu ya bunduki na kupora mali za watu na za taifa. Utajiri wa mtu au nchi haupatikani kwa kudhulumu na kuua raia. 

Taifa linajengwa kutokana na uongozi bora, utawala makini, wananchi wema, wachapakazi, waaminifu na waadilifu. 

Watanzania wenzangu, hekima ituongoze katika kauli na matendo yetu. Amani tuliyonayo tuendelee kuitunza. 

Tuwape raha viongozi wetu, wapate kutufanyia mema. Waungwana hawasukumani, wanaelewana. Watanzania ni waungwana. Tutimize wajibu wetu. Uovu ni haramu. 

462 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!