Mkononi nina Gazeti la JAMHURI (Julai 10-16, 2012) toleo Na. 33. Nimevutiwa na kichwa cha habari, ‘Dk. Ulimboka siri zavuja’. Nimevutiwa na habari hii kwa sababu ni moja ya mambo yanayoigusa jamii kwa sasa ikizingatiwa kuwa bado hali yake kwa walio wengi hatuijui, lakini pia mgomo wa madaktari bado unaendelea (naomba mgomo huo uishe ili tuweze kupata huduma).

Nikajikuta ukurasa wa pili; niliyoyasoma kwa mujibu wa ‘Mwandishi Wetu’ yanasikitisha. Nikajiona nimepelekwa dunia nyingine pasipo kujua kwa sababu mwandishi ameleta jambo geni. Mwandishi anataka Watanzania waaminishwe na stori yake anayodai inatoka kwenye vyombo vinavyochunguza tukio hilo (jambo ambalo si la kimaadili kutoa taarifa kabla ya uchunguzi kukamilika)!

 

Nikajilaumu kwa nini nimeshawishika kusoma kilichoandikwa! lakini nikakumbuka kwamba ni lazima nisome pande zote ili kama mchambuzi nipite katikati. Mwisho wa kusoma kwangu nikaamua yafuatayo: Niirudie kuisoma mara ya pili stori hii, nimjibu Mwandishi Wetu, nisome habari nyingine ili nione kama ni udaku au habari za uchambuzi, na ninunue gazeti la wiki ijayo (Julai 17-23, 2012) ili kuona maandishi haya yamechapishwa.

 

Kwa nini nimefikia uamuzi huu? Mosi, taasisi za fedha kufanikisha mgomo: Madaktari walikuwa na bado wana madai yao yanayojulikana na pande zote mbili (madaktari na serikali). Madaktari wanasisitiza madai yao yatekelezwe na mwajiri wao, wakati huo huo mwajiri anasema ametekeleza baadhi na mengine hayatekelezeki. Ni taasisi ipi inayoweka kujitokeza na kwa faida ipi kufanikisha mgomo ukizingatia wale madaktari ni wasomi, lakini pia ni wengi? Akili ndogo inawezaje kutawala akili kubwa?

 

Pili, wizi wa Dk. Ulimboka/mgogoro na wenzake: Kwa mujibu wa makala na vyanzo vingine ni kwamba baada ya kupata taarifa za kutekwa na kuumizwa kwa Dk. Ulimboka, si tu madaktari wa Dar es Salaam na wengine wa mikoani walianza kulia na kuacha kazi kwa muda, bali madaktari wa Dar es Salaam kwa asilimia kubwa walifika Muhimbili si tu kumjulia hali, bali kumsaidia ili apone haraka.

 

Taarifa zinasema zilihitajika pesa nyingi apelekwe nje apate matibabu zaidi. Madaktari bila kujali wingi au uchache wa mishahara yao walichanga na kufanikisha lengo lao kwa asilimia kubwa. Madaktari kwa umoja wao wakaweka ulinzi mkali ili asije akadhurika zaidi.

 

Kwa mujibu wa taarifa ya Mwandishi Wetu, madaktari walikataa msaada wa serikali, jambo ambalo Msemaji wa Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii, Nsachris Mwamaja, alisikitishwa lakini pia madaktari waliwazuia viongozi wa serikali kwenda kumjulia hali Dk. Ulimboka. Hapa kweli kuna mgogoro wa kimaslahi kati ya Dk. Ulimboka na madaktari wengine au wasomaji wanalishwa sumu?

 

Tatu, NGO na chama fulani: Mwandishi Wetu amerudia kile kilichokwisha kusemwa, ‘’nchi isitawalike’’! Hapa nikapata maswali ambayo bado sijapata majibu yake. Hivi nchi isipotawalika hicho chama fulani na hizo taasisi ziziso za kiserikali (NGO) kazi zao watazifanyia wapi na wanapata faida gani? Chama (hata kwa NGO) kazi yake kubwa ni kushawishi watu wakiunge mkono ili kuleta mabadiliko chanya kwenye jamii fulani.

 

Pamoja na kwamba sijajua neno ‘chama fulani’ linamaanisha chama gani (cha siasa, cha kufa na kuzikana, cha wakulima, wabeba mizigo n.k) siamini kama Watanzania wa leo wanaamini kuna NGO au chama chochote kinachoweza kufanya upuuzi huu na watu wakaendelea kukiamini na kuendelea nacho.

 

Nne, ndugu waliofiwa na wagonjwa wao: Katika hali ya kawaida, ndugu wanaowapeleka wagojwa wao Muhimbili ni kina sisi. Sasa ndugu huyu/hawa kuweza kumteka daktari tena kwa silaha mbele ya watu wengine na baadaye kutoa kipigo kisicho cha kawaida (kwa mujibu wa Dk. Ulimboka wakati anahojiwa), ili ni jambo la kufikirika zaidi kuliko hali halisi.

Tano, kuhusika kwa Chadema katika utekaji: Hapa si tu kwamba yanayotokea bungeni ni maigizo (kwa mujibu wa Januari Makamba), sipati muunganisho wa moja kwa moja kati ya pande hizi mbili kwamba Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) walimteka Dk. Ulimboka ili wananchi waichukie serikali yao.

 

Kuna mambo wananchi wanayoweza kuichukia serikali yao isipoyatimiza kama vile ukosefu wa maji, kupanda kwa gharama za maisha, kukosekana kwa dawa hospitalini na huduma zote za jamii kwa ujumla wake, na si Chadema  kumteka Dk. Ulimboka.

 

Chadema, kama ilivyo kwa vyama vingine vya siasa ni kuwaaminisha watu wengi zaidi kwa kutoa sera zao za kimaendeleo ili wajiunge nacho kwa maendeleo chanya, ili baadaye wapewe madaraka ya kuiongoza nchi au kuendelea kuiongoza nchi.

 

Mwandishi kawataja Mwigulu Nchemba na Injinia Stella Manyanya kwa jambo hili. Hapa vile vile ningependa niweka kumbukumbu vizuri kwamba kwanza watajwa hao wakiwa bungeni, walimaanisha Chadema ndiyo waliokuwa wanafanikisha mgomo ili serikali ichukiwe, na si kumteka Dk. Ulimboka.

 

Pia, si kwamba Spika alikataza kulizungumza bungeni suala hilo kwa sababu lingeleta mtafaruku, bali ni kwa sababu suala hilo liko mahakamani – japo serikali imelisemea wakati liko mahakamani!

 

Sita, serikali kuwa mtuhumiwa mkuu katika suala hili: Kwa mujibu wa ushahidi wa kimazingira, serikali ndiyo mtuhumiwa, si tu namba moja, bali pekee kwa sabu ndiyo inayomiliki silaha, ndiyo inayolinda raia wake na mali zao, ndiyo yenye watu mahsusi wa kuteka na kutesa, na ndiyo yenye sababu ya kumteka kiongozi wa mgomo.

 

Saba, mtuhumiwa kuongoza uchunguzi: Rais wetu anavitaka vyombo vya ulinzi na usalama kuchunguza suala hili na kuleta ripoti haraka iwezekanavyo. Tutarajie ripoti ipi hapa; kwamba usalama unahusika? Yawezekana Rais akawa hajui mpango kwa maana kwamba hakuhusishwa, lakini ni kosa kwake kutetea kabla ya uchunguzi kukamilika.

 

Tume huru hata kama itaundwa na Rais mwenyewe ifanye kazi hiyo kama kweli serikali inataka kujitoa katika tope hili, vinginevyo ina kazi ngumu sana (kwa mujibu wa Dk. Chitage).

 

Nane, hitimisho: Ningependa tumalize kwa kujiuliza maswali kadhaa: Kwanini madaktari walilia na kuacha kazi kwa muda na wengine kwenda Muhimbili? Kwanini madaktari walichangishana fedha za kumsaidia mwezao wakati huo huo wakikataa msaada na viongozi wa serikali kumwona Dk. Ulimboka?

 

Je, ni kweli kuna wizi (kupiga panga) unaosemwa na Mwandishi Wetu? Ni raia yupi mwenye ujasiri wa kuteka kwa silaha na kujeruhi? Je, ni kweli kuna mgogoro wa kimaslahi kati ya Dk. Ulimboka na madaktari wengine hadi (nasikia) waombe ulinzi mwingine? Hivi, ni suluhisho kumdhuru kiongozi wa mgomo au ni kuchochea mgogoro huo kukua?

 

Mwandishi wa makala hii, hakujitambulisha, lakini kwenye email yake kuna jina la Mwesiga Kyaruzi. Anapatikana kwa email: [email protected]

By Jamhuri