MOSHI

Na Charles Ndagulla

Watu 30 wanadaiwa kuvamia na kuendesha shughuli za kilimo kwenye shamba lenye ukubwa wa ekari 70 katika Kijiji cha Mtakuja, Mabogini, wilayani Moshi.

Shamba hilo linadaiwa kuwa mali ya Edward Merishoki, aliyefariki dunia mwaka 1986, sasa likimilikiwa na warithi wake.

Wavamizi hao wanadaiwa kupata nguvu zaidi na hata kuuza sehemu ya eneo la ardhi ya Merishoki kutokana na Serikali ya Kijiji cha Mtakuja kubariki vitendo hivyo kwa kuidhinisha na kuthibitisha mauziano.

Wakizungumza na JAMHURI, wawakilishi wa familia ya Merishoko; Arbogasti, Isayas, Narsis, Aloyce na Rogath Olotu, wanasema yote hayo yanafanyika huku kukiwapo amri ya Mahakama Kuu ikielekeza kuondolewa wavamizi shambani hapo.

“Amri hiyo ilitolewa Agosti 15, 2007 na Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Moshi, Fakih Jundu, lakini hadi sasa hakuna utekelezaji uliofanyika.

“Hali hii inakatisha tamaa. Amri ya Mahakama inakiukwa na serikali? Maana yake nini? Hadi sasa sehemu ya shamba letu inaendelea kuuzwa,” anasema Rogath kwa niaba ya wenzake.

Anasema uvamizi ulianza mwaka 1986 ambapo nyumba iliyokuwapo shambani ilivunjwa na vitu vilivyokuwamo kama mbao na mabati vikachukuliwa.

Kwa mara ya kwanza walifungua shauri mahakamani na kusajiliwa kwa namba 14/1986.

“Uamuzi ulipotolewa tulishinda, lakini wakati tukiendelea na maboresho ya shamba, wavamizi wakaja tena. Zuio jingine likatolewa Februari 24, 1986,” anasema.

Rogath, kiongozi wa wawakilishi wa ukoo wa Olotu, anasema pamoja na amri mbalimbali kutolewa na vyombo vya kisheria, hakuna utekelezaji uliofanyika, ikiwa ni sawa na kubariki uvamizi wa eneo hilo.

“Hata sijui nani wa kutusaidia, kwa kuwa sasa tunaishiwa nguvu. Mgogoro huu umetuchosha,” anasema Isaya Olotu.

JAMHURI lina nyaraka kadhaa kuthibitisha uhalali wa umiliki wa shamba hilo kama stakabadhi ya malipo ya Sh 140,000 ya Machi 1, 2008 kwa Serikali ya Kijiji cha Mtakuja kwa ajili ya usajili wa shamba.

Pia kuna barua ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Moshi ya Februari 2, 2018 ikijibu malalamiko ya familia kuhusu uvamizi wa shamba, na sehemu ya barua hiyo inasomeka:

“Kutokana na sheria ya ardhi pamoja na hukumu ya mahakama ikizingatiwa na risiti ya malipo ya umiliki iliyotolewa na Halmashauri ya Kijiji cha Mtakuja, ni dhahiri kabisa familia ya Edward Merishoki na wenzake watano ndio wamiliki halali.”

Kuhusu suala hilo, Mtendaji wa Kijiji cha Mtakuja, Frans Laswai, anakiri kuwapo amri ya Mahakama Kuu katika mgogoro huo wa ardhi, lakini hakuwa tayari kuzungumza kwa kina, akidai lipo shauri kwenye Baraza la Ardhi la Wilaya linaloshughulikia suala hilo.

Hata hivyo, JAMHURI linafahamu kuwapo maombi ya familia ya marehemu kwa Baraza kutoa kauli juu ya nani hasa ni mmiliki wa shamba, ikizingatiwa kuwa amri ya Mahakama Kuu haijatekelezwa.

Akijibu swali kuhusu viongozi wa vijiji na vitongoji kushiriki katika kuidhinisha mauziano ya eneo la shamba hilo kwa kugonga mihuri ya serikali, Laswai anasema kuanzia sasa Ofisi ya Utumishi Halmashauri ya Wilaya ya Moshi imepiga marufuku viongozi hao kujihusisha na masuala ya ardhi.

‘‘Leo (mwezi uliopita) tulikuwa na kikao na ofisa utumishi na moja ya yaliyojadiliwa ni kuhusu viongozi wa vijiji na vitongoji kujiingiza kwenye masuala ya uuzwaji wa ardhi. Tumepiga marufuku suala hilo,” anasema.

By Jamhuri