Nilipata fursa ya kushuhudia kwenye runinga majadiliano ya Muswada wa Sheria ya Makosa ya Mtandao ya mwaka 2015. Kwa mtazamo wangu, sheria ikianza kutumika kutakuwa na ongezeko kubwa la watumiaji wa mawasiliano; hasa ya simu, kubebeshwa makosa, kulipa faini, na kutumikia vifungo gerezani.
Kusudio la itakayokuwa Sheria ya Makosa ya Mtandao 2015, kwa mujibu wa muswada uliowasilishwa bungeni na Serikali, ni: “…kutunga sheria ambayo itaainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, kuweka utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kielektroniki.”


Ni kweli kuwa vipo vipengele ndani ya muswada vinavyoainisha makosa ambayo yanastahili adhabu. Mfano, wahalifu wengi leo wanatumia mtandao kuiba pesa kutoka kwenye akaunti za benki, pamoja na kutumia majina ya watu wasiokuwa na hatia kufanya uhalifu huo ili kuficha utambulisho halisi wa wahalifu hao. Aidha, kutoa taarifa zinazolinda ulinzi na usalama wa Taifa bila shaka kunastahili adhabu kali.


 Hakuna ubishi pia kuwa kushirikisha watoto kwenye vitendo vya ngono na kutumia picha au taarifa hizo kwenye mitandao ya kompyuta na simu ni makosa ambayo hayapaswi kuvumiliwa. Wanaoshiriki vitendo vya aina hii wanastahili kuhamishiwa gerezani na kubaki huko maisha yao yote.
Aidha, nimewahi kuandika kwenye safu hii kuwa wanaotumia mtandao wa habari na mawasiliano kusambaza uongo hawatumii vyema wajibu wao kama wanajamii. Hawa, kwa maoni yangu, wanastahili adhabu iliyoainishwa kwenye kifungu cha 16 cha Muswada wa Sheria hii.


Lakini pamoja na yale ambayo wengi tutakubaliana ni makosa dhahiri, kuna makosa yaliyoainishwa kwenye muswada ambayo yatawakumba wasiokusudiwa. Kifungu 7(2)(b) ambacho kinabainisha kuwa anayepokea data kompyuta ambayo haijaidhinishwa, atakuwa ametenda kosa mwa mujibu wa sheria hii, kinampa mwanya mtu yeyote mwenye nia mbaya na uwezo wa kutuma data hizo kwa mtu mwingine bila anayepokea taarifa hizo kuziomba, na hizo taarifa zilizopokewa zitakuwa ushahidi wa kumtia hatiani anayekutwa nazo.


Pamoja na kuwa muswada unatambua kuwa ni kosa kwa mtu kutuma taarifa kwa mwingine bila ya ridhaa ya anayezipokea, teknolojia iliyopo inaruhusu kutotambuliwa kwa aliyezituma. Sheria hii inaacha mwanya kwa watu kukutwa na hatia na kulipa faini au kutumikia vifungo kutokana na vitendo vya makusudi vya watu wengine.


Sheria hii itasababisha umiliki wa simu kuwa sawa na ule wa silaha. Inakuwaje pale mtu anapoiba simu yangu na kutuma ujumbe ambao maudhui yake, kwa mujibu wa sheria hii, ni kosa la jinai? Mtu anaweza kujibu kuwa ni wajibu wangu kuhakikisha naichunga simu yangu, kama ambavyo mmiliki wa silaha anavyowajibika kuchunga silaha yake isitumike kwenye matukio ya uhalifu. Tayari wanadamu hatuaminiani kwa mengi, na hali hii itatuongezea sababu nyingine ya kutoaminiana.


Katika muswada huu ipo dhamira ya kuzuia uhalifu, lakini yawezekana pia kuna kusudio la kudhibiti harakati za kijamii na za kisiasa. Kipengele 20(1) kinachoelekeza kwamba ni hatia kutuma ujumbe bila ya ridhaa ya anayeupokea una sura mbili. Kwanza, upo ujumbe tunaopokea kila siku wa kampuni za simu ambazo zinaleta usumbufu mkubwa kwa baadhi ya wateja kutokana na kuwa si kila anayezipokea anazihitaji. Naafiki kuzuia taarifa za aina hii. Mtumiaji wa simu anapaswa kupewa uwezo wa kuchagua iwapo anataka kupokea taarifa za kibiashara kupitia kwenye kampuni za simu.


Lakini kuna sura ya pili inayoibuliwa. Zipo taarifa za kijamii na kisiasa ambazo pia tunapokea. Siku kadhaa zilizopita, nimepokea ujumbe wa mgombea mtarajiwa wa jimbo mojawapo la ubunge ambaye anajiandaa kugombea ubunge, akiomba kuungwa mkono kwenye harakati zake. Sheria ikipitishwa huyu naye anapaswa kwenda na maji, kwa kunitumia ujumbe bila ridhaa yangu. Hapa naona kuna kasoro.


Ni kweli kuwa naye ni msumbufu kwa watumiaji wa mtandao wa simu, lakini kuna umuhimu wa kulinda haki ya raia kupokea taarifa zenye madhumuni ya kupanua ufahamu wao na uwezo wao wa kushiriki kwenye michakato inayojenga demokrasia. Kwa mtazamo wangu, hizi taarifa ni muhimu kuliko taarifa za kila siku ambazo tunapokea kutoka kwenye kampuni za simu.


Kampeni za uchaguzi zikipamba moto huyu mgombea angeweza kutumia simu yake kutuma taarifa kuwaelimisha wapiga kura wake kuhusu masuala muhimu ya harakati zake, lakini sheria inatishia kudhibiti fursa hiyo, na itawanyima wapigakura wake fursa ya kupata taarifa hizo kwa urahisi.
Baya zaidi, sheria inawapa fursa wapinzani wake kulalamika kupokea bila ridhaa yao ujumbe wake na hivyo kuhatarisha yeye kukutwa na hatia. Ni kipengele kinachodhibiti uhuru wa kupata habari.


 Mpaka leo hii ninayo nafasi ya kupokea ujumbe wa harakati mbalimbali za kijamii na kisiasa kutoka kila pembe ya Tanzania, lakini ikishapitishwa sheria hii nitategemea taarifa za vyombo vya habari pekee. Siamini kama demokrasia inalindwa kwa kutegemea taarifa za waandishi wa habari tu.
Wakati mwingine tatizo la baadhi ya vyombo vya habari ni kuelemea na kuwa na misimamo ambayo inaunga mkono upande mmoja dhidi ya mwingine. Si vibaya kuwa na misimamo ya aina hiyo, lakini ni muhimu pia kuwapo fursa kwa wapokea taarifa kuunganishwa moja kwa moja na watoa taarifa bila kuwekewa chujio wala chumvi.


Anayeamini kuathirika na taarifa za uongo kwa njia hii bado anabaki na fursa ya kutumia sheria kupata haki dhidi ya mtoa taarifa.
Hii itakuwa sheria inayodhibiti maovu kadhaa katika matumizi ya kompyuta na teknolojia ya habari na mawasiliano, lakini ni sheria ambayo pia itatishia uhuru wa kupokea habari na kubadilishana mawazo.

2319 Total Views 6 Views Today
||||| 1 I Like It! |||||
Sambaza!