NA MICHAEL SARUNGI

Ushindi wa klabu za Simba na Yanga katika mechi za kimataifa zilizocheza haziwezi kuwa kipimo cha ubora wao katika mashindano hayo ya kimataifa kutokana na udhaifu uliooneshwa na wapinzani wao, badala yake wanapaswa kujitathmini kabla.

Wakizungumza na JAMHURI kwa nyakati tofauti, wapenzi, wanachama na viongozi wa soka  wamesema pamoja na ushindi huo, kuna haja ya klabu hizo kujitathmini kama kweli washindani wao walikuwa ni kipimo kizuri kwao.

Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Rukwa (RUREFA), Blassy Kiondo, amesema limekuwa ni jambo la kawaida kwa klabu hizi kila mwaka  kupangwa na timu dhaifu, lakini hujikuta zikikwaa kisiki kila zinapovuka hatua hiyo.

Amesema kuna uwezekano hata mwaka huu hali ikajirudia endapo klabu hizi hazitakuja na mbinu na mikakati ya maana ya kukabiliana na washindani wenye nguvu katika michuano hii mikubwa Afrika.

Amesema mara baada ya kumalizika kwa michezo ya awali, klabu hizo zinapaswa kuanza kujiandaa mapema ikizingatiwa kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kukutana na klabu zenye uzoefu kama Zamalek ya Misri, TP Mazembe ya DRC na Al Ahly.

Amesema  miaka mingi klabu  kubwa barani Afrika zimekuwa zikifurahia kupangwa na klabu kutoka ukanda huu wa Afrika Mashariki na Kati katika hatua hizi za awali kutokana na udhaifu wa soka la eneo husika.

Mwenyekiti wa Chama cha Soka Mkoa wa Kigoma (KFA), Ahmed Mgoyi, amesema ushindi wa klabu hizo haupaswi kuchukuliwa kama ni ubora kwa klabu hizo katika mashindano hayo makubwa barani Afrika.

Amesema vinginevyo ushindi huo unapaswa kuchukuliwa kama njia ya kutumika kwa ajili ya kuwajenga kisaikolojia wachezaji ndani ya klabu hizo na kuongeza kuwa hilo linapaswa kuendana na maandalizi ya maana.

Amesema klabu hizo hazipaswi kubweteka, badala yake zinapaswa kuanza kufanya maandalizi ya kutosha mbele ya safari kuliko kulewa na sifa wanazopewa na magazeti ya michezo nchini.

Amesema udhaifu wa soka la ukanda huu umeendelea kuongezeka licha ya juhudi mbalimbali zinazofanywa na TFF ikiwamo kuandaa mechi nyingi za kirafiki kwa timu ya Taifa,  lakini kama Taifa  tumezidi kuporomoka katika viwango vya FIFA, hali ambayo imeendelea kuwa tishio kwa uhai wa soka letu.

Amesema katika siku za karibuni, Tanzania imezidi kuporomoka kwenye viwango vya FIFA; kwa mfano, Novemba mwaka jana iliporomoka kutoka nafasi ya 142 hadi ya 147, hali ambayo siyo nzuri kwa ustawi wa mchezo huo hapa nchini.

Mchezaji wa zamani wa Klabu ya Yanga na timu ya Taifa, Bakari Malima (Jembe Ulaya), amesema pamoja na klabu hizi kupata matokeo mazuri katika mechi za awali, bado zina  kazi kubwa na ngumu mbele ya safari.

Amesema endapo zitaendelea kuishi kimazoea na kushindwa kuanza kufanya maandalizi mapema, hali ambayo inaweza kuwa mbaya kama miaka yote pale ambako hujikuta wakishinda mechi za awali na kujikuta wakitolewa hatua inayofuata.

“Kuna haja ya klabu hizi kujifunza kutokana na makosa wanayofanya kila mwaka ya kutolewa katika mashindano haya kila mara katika hatua za awali, hasa zinapokutana na klabu kutoka Kanda ya Magharibi,” amesema Malima.

Klabu ya Simba inayowakilisha nchi katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika katika mechi ya kwanza ilipata ushindi wa mabao 4 dhidi ya  Gendermarie Tnale ya Djibouti, huku watani zao klabu ya Yanga ikishinda kwa bao 1 katika mashindano ya Klabu Bingwa Afrika dhidi ya St Louis kutoka Seychelles.

2568 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!