Wakati  timu ya soka ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars) ilipopoteza mchezo wake dhidi ya timu ya Taifa ya Uganda (The Cranes) katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam, wiki iliyopita kwa kufungwa goli 1-0, wadau wa soka walikuwa na mengi ya kusema dhidi ya kipigo hicho.

Mchezo huo wa kwanza kwa Stars katika harakati za kuwania tiketi ya kucheza michuano ya fainali za wanandinga wanaokipiga Ligi za Nyumbani (CHAN), ulikuwa ni muhimu kwa Taifa Stars kushinda, ikizingatiwa kwamba ilikuwa ikicheza katika uwanja wa nyumbani.

Pia ushindi ungekuwa ishara ya matumaini katika kuwania kushiriki katika michuano hiyo ya kimataifa.

 

Kama vile anajibu mapigo, Kocha Mkuu wa Stars, Kim Poulsen, aliwapa Watanzania matumaini kuwa kuna uwezekano mkubwa wa kushinda mechi ya marudiano itakayofanyika Kampala, Uganda, siku chache zijazo. Kwa kawaida hakuna kocha yeyote anayeweza kusema kuwa yuko tayari kufungwa katika mechi hiyo.

 

Kwa hiyo, kocha Kim yuko sahihi kwa kujipa matumaini ya ushindi katika mechi ya marudiano na hili halina ubishi kwani linawezekana. Kama Uganda waliweza kuwafunga Stars katika ardhi yao, Stars pia wanaweza kuwafunga The Cranes katika uwanja wao wa nyumbani kwa sababu mpira unadunda.

 

Baadhi ya Watanzania wameshakata tamaa na hivyo kuipa Stars nafasi nyembamba kushinda mechi hiyo ya marudiano. Hili ni kundi la wale Watanzania wanaokumbuka kiwango kilichooneshwa Stars katika mtanange huo wa kwanza.

 

Kuna mambo mengi ya kuangalia pale tunapoipa Taifa Stars kipaumbele cha kufanya vizuri katika mechi za kimataifa. Kwanza ni lazima kukubali kuwa soka la Tanzania limegubikwa na changamoto nyingi zinazopaswa kushughulikiwa ndipo Taifa liweze kupiga hatua na kujiamini katika soka la kimataifa.

 

Serikali imejitahidi kuleta makocha wa kigeni kwa nyakati tofauti, na kwa kiasi fulani Stars imepiga hatua. Kwa mfano, kinachoonekana sasa hivi kwa wachezaji wengi wanaounda timu ya Taifa ni kama vile uwezo wao wa kufikiri kisoka umeishia hapo walipofikia. Si wakati wa kuwalaumu bali ni wakati wa kuwashukuru hapo walipotufikisha na sifa walioweza kuliletea Taifa letu.

 

Ni wachezaji hao hao waliochangia kwa kiasi kikubwa Stars kuzifunga Morocco, Cameroon na timu nyingine na hivyo kuwafurahisha Watanzania kwa wakati huo. Hapa kuna haja ya kujiuliza wachezaji wanaoitumikia Stars kwa sasa walitoka wapi na huu ni wakati gani kwao?

Sasa kama leo hii wanashindwa kuifunga Uganda, hakuna haja ya kuwalaumu bali ni wakati wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kwa kushirikiana na wadau wengine, kuweka nguvu zaidi katika kukuza soka la vijana ili kesho na keshokutwa tuwe na akina Mbwana Samatta na Thomas Ulimwengu wengi watakaoweza kuonesha uwezo binafsi.

 

Ni dhahiri kuwa moja ya mambo ambayo kwa sasa ni tatizo kwa wachezaji wa Stars na hata klabu za soka nchini ni uwezo binafsi wa mchezaji, wa kufanya uamuzi sahihi na wakati mwafaka pale anapokuwa uwanjani.

 

Mara nyingi mchezaji mwenye uwezo kisoka, hasa yule ambaye amefikia hatua ya kuchezea timu ya Taifa lake, anahitaji kuwa na ujuzi ili kumsaidia kufanya uamuzi ya haraka na wenye tija pale anapokuwa uwanjani kwa manufaa ya timu yake.

 

Tatizo hili pia limekuwa sugu kwa sababu wachezaji wengi wanajiunga na klabu mbalimbali vya soka hapa nchini, kwa sababu wana vipaji vya kucheza mpira lakini hawapati ujuzi wowote wa ziada katika umri mdogo wakati wakianza kucheza soka.

 

Lakini pia michuano hii ya  CHAN ni fundisho kwa viongozi wanaoongoza klabu za soka hapa nchini, kuacha tabia ya kuthamini wachezaji wa ndani na kukimbilia kusajili wachezaji kutoka nje ya nchi ambao kiwango chao hakiridhishi na hivyo kuishia kukaa benchi na wakati mwingine kukatisha mikataba yao.

 

Hali hii inaleta hasara kwa klabu husika kwani wanatumia fedha nyingi lakini wakati huo huo ikiwanyima nafasi wachezaji chipukizi wa hapa nyumbani.

 

Kama kunakuwa na uendeshaji mzuri wa ligi za ndani kutakuwa na wachezaji wazuri ambao pia wangeweza kuonesha vipaji vyao katika michuano kama hii ya CHAN, kwani kwa vyovyote vile baadhi yao watapata nafasi ya kuunda timu ya Taifa ikiwa wanaonekana bora kupitia timu zao.

 

Kuna haja ya viongozi wa klabu kama Simba au Yanga kutumia hizo pesa zao kusaka vipaji hapa nchini kuliko kusajili wachezaji feki kutoka nje ya nchi. Hali hii pia itawatoa viongozi hao katika wakati mgumu ambao mara kwa mara wamekuwa wakitupiwa lawama za hapa na pale kwamba wanafanya usajili kwa maslahi yao binafsi na si kwa ajili ya klabu zao.

 

Soko la Tanzania bado lina changamoto lakini haya ni baadhi ya mambo ambayo kama yangeweza kufanywa kwa usahihi, kuna uwezekano wa kuwa na timu nzuri ya soka ya Taifa kwa miaka ijayo kuliko staili tunayakwenda nayo kwa sasa.

 

Katika nchi yoyote duniani maendeleo ya soka hayaji bila kuthamini wachezaji wa ndani, kuwa na mipango maalum ya kukuza vipaji kwa vijana na mfumo mzuri wa ligi za ndani zenye utaratibu wa kupandisha wachezaji kwa kuzingatia umri wao na viwango vya uchezaji.

 

Watanzania waliokata tamaa wawe na imani kuwa Stars ina uwezo wa kuifunga Uganda katika mechi ya marudiano, lakini wakati huo kuna haja ya kufikiria njia mbadala za kufanya ili kukabiliana na changamoto zinazolikabili soka la Tanzania.

 

Huu si wakati wa lawama bali ni wakati wa kuangalia njia mbadala za kukuza soka la Tanzania na kuepuka ile kauli ya ‘vijana walicheza vizuri lakini bahati haikuwa ya kwetu’. Sasa tufanyeje ili wacheze vizuri na siku moja bahati iwe ya kwetu?

1445 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!