Kijana wa kiume Mzungu mwenye asili ya Afrika Kusini, amefanyiwa tohara ya kimila nchini humo. Tohara ya kimila katika baadhi ya makabila nchini Afrika Kusini huashiria hatua ya ukuaji kwa kijana inayompatia hadhi ya kuitwa mtu mzima katika familia.

Kijana huyo, Brandon de Wet (17), mkazi wa ukanda wa mashariki wa nchi hiyo, amefanyiwa tohara hivi karibuni pamoja na rafiki yake, Yanelisa Somyo (13), kutoka kabila la Waxhosa.

 

Brandon ameliambia Shirika la Utangazaji la Uingereza (BBC) kwamba hatua ya kufanya tohara imembadilisha kuwa na maisha mazuri tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

 

“Ilikuwa safari ndefu kwani sijawahi kufanya kitu kama hicho, tulikaa wiki tatu mafichoni sehemu za milimani,” amesema na kuendelea: “Kabla ya hapo nilifahamu machache kuhusu kabila la Waxhosa, lakini ngariba alinieleza kwa undani kila kitu kitakachofanyika na umuhimu wa kufanya tohara ya kimila, nilipata wakati mgumu lakini maelezo yake yalikuwa na maana sana.”

 

Tohara ya kimila imekuwa maarufu kwa makabila ya Waxhosa na Wandebele, ambayo ni miongoni mwa makabila makubwa nchini humo.

 

Brandon na Yanelisa wamekuwa marafiki tangu wakiwa na umri mdogo. Vijana wa kiume katika kabila la Waxhosa wanapofikia umri wa miaka kati ya 15 na 17, familia zao huwapelela katika mafunzo ya awali kabla ya tohara.

 

Mafunzo hutolewa na Incibi, yaani ngariba wa kiume na Ikhankatha kwa upande wa wasichana. Mafunzo haya yanayoambatana na tohara hufanyika kila mwaka mwezi Juni au Desemba wakati shule zimefungwa.

 

Mambo yote hufanyika mafichoni milimani. Vijana hupewa mafunzo ya jinsi ya kukabiliana na changamoto mbalimbali za kifamilia katika jamii zao. Wavulana hutengwa kwa wiki kadhaa katika sehemu ambayo wasichana hawaruhusiwi kufika.

 

“Kuna wakati nilijaribu kumshawishi ngariba aahirishe kunifanyia tohara, kwani nilikuwa na hofu kutokana na yale mafunzo ya awali, lakini kwa vile alikwishaamua, hivyo hakukuwa na jinsi ya kubadilisha jambo hilo.”

 

Baada ya kufanyiwa tohara, vijana huingia katika nyumba ya msonge maarufu kama Iboma ambapo hukaa kipindi chote  wanachokuwa huko. Chakula huandaliwa na familia zao na hupelekwa na mabinti wadogo.

 

Taratibu zote kuhusu chakula hutolewa na ngariba, ambaye muda wote anakuwa makini kutunza majeraha na kuhakikisha wanapata tiba za asili. Wakati huo vijana huvishwa nguo maalum na kufunga blanketi kiunoni huku wakipakwa udongo mweupe mwili mzima.

 

Baada ya muda wa jando kumalizika, vijana wote huoga mtoni kwa ili kuondoa udongo wote mwilini ikiwa ni ishara ya kuanza hatua nyingine katika maisha na kusahau yaliyopita. Huchoma nyumba (Iboma) walizokuwa wakiishi kama ishara nyingine ya maisha mapya. Wanapakwa udongo mwekundu tayari kurudi nyumbani wakivalia blanketi nyeupe ambazo ni ishara ya kufuzu mafundisho.

 

Hivi karibuni wananchi wengi nchini Afrika Kusini wamekuwa wakihoji umuhimu wa tohara ya kimila, ambayo imekuwa ikisababisha vijana wengi kupoteza maisha kila mwaka.

 

Kwa mujibu wa takwimu kutoka kitengo cha afya ukanda wa mashariki wa nchi hiyo, vijana zaidi ya 20,000 kutoka ukanda huo hufanyiwa tohara ya kimila kila mwaka, ambapo idadi kubwa ya vijana hutoka katika makabila ya Waxhosa na Wandebele.

 

Katika msimu wa mwezi Juni mwaka huu, vijana zaidi ya 70 kutoka sehemu mbalimbali Afrika Kusini wamepoteza maisha kutokana na upungufu wa maji mwilini, vidonda kushindwa kupona na kushambuliwa na ndugu na jamaa  baada ya kutoka jandoni.

 

Vijana 300 wa kiume walilazwa katika hospitali mbalimbali ambapo 10 kati yao walikatwa uume kutokana na kuliwa na vidonda. Pia watu watano walitiwa mbaroni kufuatia vifo vya vijana wa kiume 30.

 

Awali wazazi wa Brandon hawakutaka kijana wao afanyiwe tohara ya kimila kutokana na hali hiyo. Kilichowapa matumaini ni uwezo wa familia ya rafiki yake, ambaye aliahidi kuwapa matunzo bora baada ya tohara, na ndivyo ilivyokuwa baada ya kutoka huko.

 

Mama wa Brandon alisikitika pale kijana wake alipoaga na kuelekea kwenye  tohara. Kwa kawaida vijana wa kiume hawaruhusiwi kuwasiliana na wanawake wakiwa katika mafunzo ya kufanyiwa tohara.

 

Baba yake Brandon, Dave de Wet, alikuwa akimtembelea mwanaye mara kwa mara kumjulia hali. Anasema alijifunza mambo mengi juu ya mwanaye na kwamba angalau aliweza kujua hali yake ya kiafya kila siku.

 

“Siku waliporejea nyumbani, majirani walikuwa wakishangaa kuona Mzungu naye kafanyiwa tohara, lakini kwa mwanangu ilikuwa ishara ya kishujaa na pia kuonesha ukaribu na ile jamii ya watu tunayoishi nayo,” amesema Dave de Wet.

 

Hospitali nyingi nchini Afrika Kusini zimekuwa zikitoa huduma ya tohara. Vyanzo mbalimbali vya habari nchini humo vinasema ngariba wote wametakiwa kujisajili kwa mamlaka husika.

 

Siku za karibuni limejitokeza wimbi kubwa la ngariba ambao hawana utaalamu na wamekuwa wakiendesha shughuli hiyo kwa ajili ya maslahi yao pasipo na utaalamu.

 

Waziri mwenye dhamana ya kusimamia mila na desturi katika ukanda wa mashariki nchini humo, Mlibo Qoboshiyane, anasema vijana wanaofanyiwa tohara ya kimila kwa utaalamu unaotakiwa hawapati tatizo lolote na hupona vizuri.

 

“Hizi ni mila ambazo zimekuwapo tangu zamani, ni muhimu pia katika ukuaji wa vijana wetu. Mimi mwenyewe pia nilipitia hatua hiyo na ilinisaidia kuwa mwanaume mkakamavu kama ninavyoonekana sasa, jambo la muhimu ni kupata ngariba mwenye utaalamu,” Waziri Qoboshiyane ameiambia BBC.

Please follow and like us:
Pin Share