Mfanyabiashara maarufu, Thobias Moshi (47), maarufu kwa jina la ‘Toby’ mkazi wa Shanty Town katika Manispaa ya Moshi, amefikishwa mahakamani akishitakiwa kwa makosa mawili ya kughushi nyaraka.

Moshi, ambaye ni Mkurugenzi wa Mabasi ya Amazon na mmliki wa vitegauchumi Moshi na Dar es Salaam, ameshitakiwa chini ya sheria ya makosa ya kughushi.

Shitaka la kwanza linalomkabili ni kughushi mkataba wa mauzo ya nyumba yenye thamani ya Sh milioni 600, mali ya Athony Kimatare, mkazi wa Marangu, Moshi Vijijini.

Nyumba hiyo ipo katika Kiwanja Na. 14, Kitalu ‘C’ sehemu ya III katika Manispaa ya Moshi. Hati ya mashitaka iliyosomwa mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi Mahakama ya Mkoa, Joachim Tiganga, mshitakiwa Moshi alitenda kosa hilo Januari 15, 2006.

Katika shitaka la pili, Wakili wa Serikali, Lucy Kyusa, anadai kuwa katika muda na tarehe isiyojulikana, ndani ya eneo la Manispaa ya Moshi, mshitakiwa huyo alighushi hati ya nyumba namba 2277 na kuonesha kuwa Anthony Kimatare amehamisha umiliki wa nyumba yake kwenda kwake (mshitakiwa).

Tayari upande wa mashitaka umeita mashahidi watano kuthibitisha mashitaka dhidi ya mfanyabiashara huyo, akiwamo Wakili wa Kujitegemea, Godwin Sandi, ambaye alishiriki kuandaa mkataba halisi na si ule unaodaiwa kughushiwa.

Chimbuko la kesi hiyo ni mkataba wa miezi sita wa kukopeshana fedha ulioingiwa na mshitakiwa huyo na Kimatare wa Sh milioni 26 ambao ulisainiwa Julai 12, 2005 ukiweka sharti la kuwa endapo mkopaji atashindwa kurejesha mkopo huo, dhamana ya nyumba aliyoweka itahesabika kuwa imeuzwa.

Kwa mujibu wa mkataba huo uliotiwa saini mbele ya Wakili Sandi ambaye ni shahidi wa pili upande wa mashitaka, Kimatare alitakiwa ndani ya muda huo wa mkataba awe amerejesha mkopo huo pamoja na riba ya Sh milioni moja na kufanya jumla ya mkopo huo kuwa Sh milioni 27. Hata hivyo, mkataba unadaiwa kuwa halisi unaonesha kuwa nyumba iliyowekwa dhamana ya mkopo ipo kwenye Kiwanja Na. 14, Kitalu ‘C’ sehemu ya III Moshi Township, lakini mkataba mwingine unaonesha herufi ‘C’ ikiwa imeghushiwa na kusomeka ‘G’.

“Kwa kusaini mkataba huu, muuzaji anakiri kuwa ameshapokea fedha zote za mauzo ya nyumba kutoka kwa mnunuzi na amemkabidhi mnunuzi nyumba iliyopo kwenye Kiwanja Na. 14 Block ‘C’ section III, Moshi Township,” inasomeka sehemu ya mkataba huo.

Akitoa ushahidi wake mbele ya Hakimu Tiganga, Wakili Sandi alitambua mkataba wa awali ambao aliusimamia huku akiukana mkataba unaoonesha herufi ‘G’ ambao, hata hivyo, hauna tofauti na mkataba halisi zikiwamo saini za mashuhuda.

Mkataba huo unaodaiwa kughushiwa ndiyo uliotumiwa na mshitakiwa kwenda kwa Msajili wa Ardhi kwa ajili ya kufanya taratibu za kuhamisha umiliki wa nyumba hiyo kutoka kwa Kimatare kwenda kwa mshitakiwa Moshi. 

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Machi 14, mwaka huu, itakapoendelea kusikilizwa ambako upande wa mashitaka utapeleka mashahidi wengine, akiwamo Kimatare anayedaiwa kuwa muuzaji wa nyumba hiyo.

Katika mkataba wa kukopeshana fedha, Kimatare alijifunga yeye na mkewe, Aneth Kimatare, kuwa endapo mkopo huo hautarejeshwa ndani ya muda huo, hati ya nyumba itabaki mikononi mwa mshitakiwa huyo na kuingia mkataba wa kuuziana hiyo nyumba.

“Mkopaji amemhakikishia mkopwaji kwamba yeye ni mmiliki halali wa nyumba iliyowekwa rehani na amepata ridhaa ya mke wake kuchukua mkopo huo pamoja na kuweka nyumba iwe dhamana ya mkopo,” inasomeka sehemu ya mkataba huo.

Wakati kesi hiyo ikiendelea mahakamani, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) mkoani Kilimanjaro, imeanza uchunguzi kubaini kama mfanyabiashara huyo alilipa kodi kwa mujibu wa sheria.

Meneja wa TRA Mkoa wa Kilimanjaro, Abdul Mapembe, ameiambia JAMHURI kuwa watamwandikia Moshi barua ya mwito ili awasilishe nyaraka za ununuzi wa nyumba hiyo na nyaraka zinazoonesha kama alilipa kodi.

By Jamhuri