Jakaya_KikweteDeni kubwa ambalo Serikali inadaiwa na Mifuko ya Hifadhi ya Jamii, linatishia uhai wa mifuko hiyo, kiasi cha baadhi kuanza kusuasua na hata kushindwa kulipa mafao kwa wanachama wake, JAMHURI inathibitisha.

Hadi mwanzoni mwa mwaka jana, mifuko yote sita ilikuwa ikiidai Serikali Sh trilioni 7.134 ambazo ni mikopo na riba. Deni hilo ni matokeo ya uamuzi wa Rais (mstaafu) Jakaya Kikwete, kukopa kwa ajili ya shughuli za kimaendeleo. Pamoja na nia njema, sasa mzigo wa deni hilo unaonekana kuisumbua Serikali ya Awamu ya Tano ya Rais John Magufuli, na tayari mipango imeanza kufanywa na Serikali ili kuinusuru mifuko hiyo.

Fedha nyingi zilizokopwa zinatajwa kutumika katika ujenzi wa Chuo Kikuu cha Dodoma kinachotajwa kuwa chuo cha aina hiyo kikubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

Mifuko hiyo ni Mfuko wa Akiba wa Watumishi Serikalini (GEPF), Mfuko wa Akiba kwa Watumishi wa Serikali za Mitaa (LAPF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Jamii kwa Wafanyakazi wa Mashirika ya Umma (PPF), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSPF), na Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF).

Vyanzo vya habari kutoka serikalini vimesema kutokana na Serikali ya Awamu ya Nne, ama kushindwa, au kusuasua kulipa; sasa deni hilo, likijumuishwa na riba, linakaribia Sh trilioni 10. Bajeti ya Serikali kwa Mwaka wa Fedha wa 2015/2016 ni Sh trilioni 22.

Imebainika kuwa Serikali ya Awamu ya Nne, kupitia Wizara ya Kazi, Ajira  na Vijana ilishabaini na kukiri mtanziko wa ulipaji deni hilo, kiasi cha kuilazimu kutangaza ‘hali ya hatari’ inayolikabili Taifa endapo deni hilo halitalipwa haraka.

Taarifa ya siri ambayo JAMHURI imeipata inaonesha kuwa hali ni mbaya zaidi kwa mifuko ya PSPF na LAPF. PSPF ililazimika kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuwalipa watumishi wa umma ambao hawakuwahi kuchangia kwenye Mfuko huo.

Vyanzo vya habari vimesema hali hiyo imeitisha Serikali, na tayari Rais John Magufuli ameshaanza kuchukua hatua za dharura katika kuhakikisha kuwa deni hilo linalipwa ili kuilinda mifuko na kuwaondolewa usumbufu wastaafu kupata mafao yao.

Mwaka jana, Wizara ya Kazi ilikiri kuwa hali ya Mifuko ya Jamii si nzuri, hususan kwa mifuko ya PSPF na LAPF ambayo katika kipindi cha muda mfupi iliaminika kuwa ingeshindwa kuwalipa wanachama wake, na hivyo kusababisha matatizo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Kiasi ambacho mifuko inaidai Serikali kikiwa kwenye mabano ni: PSPF (Sh trilioni 4.828), NSSF (Sh trilioni 1.334), NHIF (Sh bilioni 458.6), PPF (Sh bilioni 288.6), LAPF (Sh bilioni 207.7), na GEPF (Sh bilioni 18).

“Madeni haya yanaathiri sana mtiririko wa fedha pamoja na uwezo wa mifuko kuhimili malipo ya mafao ya wanachama wake. Uwezo wa mifuko kuhimili malipo ya mafao kwa wanachama hupimwa kwa kulinganisha kiwango cha dhima dhidi ya mali za mfuko (liability vs asset).

“Kulingana na tathmini deni kubwa la Serikali kwa Mfuko wa PSPF limechangia sana katika kuufanya Mfuko huu kuwa na uwiano dhaifu wa dhima na mali ikilinganishwa na mifuko mingine ya Hifadhi ya Jamii.

“Uwiano kati ya dhima na mali (funding level katika mfuko wa PSPF ni asilimia 10.1,” inasema taarifa ya siri ya Serikali.

Inaelezwa kuwa uwiano huo ni dhaifu na inakadiriwa kuwa mwaka huu Mfuko huo huenda ukakosa kabisa uwezo wa kulipa dhima ya mafao kwa wanachama wake wanaostaafu na hivyo kutishia uendelevu wa Mfuko.

Pamoja na changamoto ya madeni makubwa ambayo Serikali inadaiwa, nyingine inatajwa na Wizara ya Ajira, Kazi na Vijana kuwa ni baadhi ya mifuko kulipa mafao makubwa yanayoathiri mtiririko wa fedha za mifuko.

Sababu nyingine ni uchache wa Watanzania wanaojiunga katika mifuko hiyo. Takwimu za Sensa ya Watu na Makazi ya mwaka 2012 zinaonesha kuwa ni Watanzania milioni 1.3 pekee walio wanachama wa mifuko ya jamii.

Kwa takwimu hizo za mwaka 2012, idadi hiyo ilikuwa sawa na asilimia 6 pekee ya nguvukazi ya Taifa ambayo ilikuwa watu milioni 22. Idadi hiyo si sawa na asilimia 3 ya Watanzania wote ambao kwa Sensa hiyo walikuwa milioni 45.

 

Malipo ya Pensheni ya Mkupuo kushushwa

Kwenye Rasimu ya Mapendekezo ya Kuimarisha Mifuko ya Hifadhi ya Jamii na Kuboresha Viwango vya Mafao ya Pensheni kwa Wastaafu, Wizara ya Ajira, Kazi na Vijana inatoa mapendekezo kadhaa yanayolenga kupunguza malipo ya mkupuo.

Rasimu hiyo inasema matatizo yaliyoainishwa yanaonesha kwamba kunahitajika hatua za haraka za kufanya marekebisho ili kunusuru na kuimarisha mifuko hiyo.

Inasema kulingana na hali iliyopo, ipo baadhi ya mifuko itakayoshindwa kulipa mafao, jambo ambalo Serikali inakiri kuwa litaleta madhara makubwa kiuchumi, kisiasa na kijamii.

Kwa sababu hiyo, wataalamu wa wizara wanasisitiza kuwa ni muhimu kwa Serikali kuchukua hatua haraka kurekebisha hali hiyo.

“Ili kuweza kukabiliana na athari za Mfuko kuwa na mtiririko hafifu wa fedha unaosababishwa na malipo makubwa ya mkupuo wa pensheni, inapendekezwa kiwango cha malipo ya pensheni ya mkupuo asilimia 50 yanayolipwa na mifuko ya PSPF na LAPF kipunguzwe hadi asilimia 33.3,” inapendekezwa.

Kwa sasa, mwanachama aliyefanya kazi kwa miaka 35; katika mifuko ya PSPF na LAPF, ambaye mshahara wake kwa mwezi ni Sh 2,445,000; kwa kikokotoo cha asilimia 50, malipo ya mkupuo ni Sh milioni 176.885; ilhali pensheni yake kwa mwezi ni Sh 950,833.

Lakini kwa mabadiliko yanayopendekezwa, kwa mwanachama aliyefanya kazi kwa miaka hiyo hiyo, na kwa kiwango hicho hicho cha mshahara kwa mwezi; endapo kikokotoo kitapungua hadi asilimia 33.3; hiyo ina maana kwamba atapata malipo ya mkupuo ya Sh 117,891,543 na pensheni yake kwa mwezi itakuwa Sh 1,267,841.

Wataalamu wa Wizara ya Ajira, Kazi na Vijana wanasema faida nyingine itakayotokana na kutekeleza pendekezo hilo ni kuongezeka kwa malipo ya pensheni ya kila mwezi kwa wastaafu kwa kiwango cha asilimia zaidi ya 50.

Inapendekezwa mifuko ya PSPF na LAPF itumie wastani wa mshahara wa miaka mitatu badala ya utaratibu wa kutumia mshahara wa mwisho kukokotoa mafao; hali ambayo inasababisha mifuko hiyo kulipa viwango vikubwa vya mafao tofauti na viwango cha uchangiaji. Lengo la mapendekezo hayo ni kuimarisha uwezo wa kifedha wa mifuko hiyo.

“Pia inapendekezwa mifuko ya PPF na NSSF irekebishe wastani wa mshahara wa kukokotoa pensheni kutoka wastani wa miaka mitano hadi wastani wa miaka mitatu kama ilivyopendekezwa kwa PSPF na LAPF. Hatua hii itasaidia kuondoa malalamiko kwa wanachama wa mifuko ya PPF na NSSF kwa kuwa mifuko yote itakuwa na viwango sawa,” imesema taarifa ya wataalamu wa wizara hiyo.

Mathalani, mtumishi aliyefanya kazi kwa miaka 35 mwenye mshahara wa mwisho wa Sh milioni 2.445; kwa kikokotoo cha asilimia 50 atapata malipo ya mkupuo ya Sh milioni 176.885; ilhali pensheni yake kwa kila mwezi itakuwa Sh 950,833.

 

Umri wa kuishi wa mwanachama ‘kupunguzwa’

Rasimu hiyo inapendekeza mifuko ya PSPF na LAPF itumie kiwango cha umri wa miaka 12.5 badala ya kiwango cha umri wa miaka 15.5. Hatua hiyo, inalenga kuleta uwiano mzuri wa mtiririko wa fedha katika mifuko hiyo.

Wizara inatetea mapendekezo hayo kwa kusema yanaendana na viwango vinavyokubalika kimataifa vya umri wa kuishi baada ya kustaafu vya miaka 9.5 hadi miaka 12.5 ambavyo havina madhara makubwa ya mtiririko wa fedha katika mifuko.

Mapendekezo mengine ni kwa vikokotoo limbikizi (accrual rates) vya mifuko yote. Inapendekezwa kikokotoo cha 1/540 kwa mwezi sawa na limbikizo la asilimia 2.22 kwa mwaka kinachotumiwa na mifuko ya PSPF na LAPF kirekebishwe kuwa 1/580 kwa mwezi sawa na asilimia 1.07 mwa mwaka. Taarifa ambazo JAMHURI imezipata wiki iliyopita zinaonesha kuwa tayari kikokotoo hicho kimeanza kutumika.

Aidha, inapendekezwa kikokotoo limbikizi cha 1/600 kwa mwezi sawa na limbikizo la asilimia 2 kwa mwaka, kinachotumiwa na Mfuko wa PPF kirekebishwe kuwa 1/580 mwa mwezi, sawa na asilimia 2.07 kwa mwaka; na kikokotoo cha asilimia 30 na nyongeza ya asilimia 1.5 kwa kila miezi 12 baada ya mwaka wa 15 wa uchangiaji katika mfuko kirekebishwe kuwa 1/580 kwa mwezi; sawa na asilimia 2.07 kwa mwaka.

“Utekelezaji wa pendekezo hili utakuwa na matokeo yafuatayo; kwanza, itakuwa ni kuimarisha mtiririko wa fedha wa mifuko ya PSPF na LAPF; na pili, itaongeza viwango kwa vikokotoo kwa mifuko ya PPF na NSSF hivyo kuongeza mafao ya wanachama ambao wamekuwa wakilalamika kwa muda mrefu,” inapendekeza wizara.

Mbinu nyingine inayopendekezwa ili kuilinda mifuko inayoelekea kufilisika ni kupunguza umri wa kuishi wa mwanachama baada ya kustaafu. Lengo ni kukokotoa kiwango cha rasilimali zinazohitajika kulipa mafao ya mkupuo mara mtumishi anapostaafu.

Wizara inasema kiwango hicho kikiwa kikubwa rasilimali nyingi zaidi zitahitajika kugharimia malipo ya pensheni kwa mwanachama, hali ambayo inasema inadhoofisha Mfuko kifedha.

 “Kiwango kinachokubalika kimataifa cha miaka ya kuishi baada ya kustaafu ni kati ya miaka 9.5 hadi miaka 12.5. Mifuko ya PSPF na LAPF inatumia makadirio ya umri wa kuishi baada ya kustaafu wa miaka 15.5 kiwango ambacho ni cha juu ya kiwango kinachokubalika kimataifa.

“Kwa kutumia kiwango hicho mifuko hii inalipa mafao makubwa ya mkupuo na hivyo kudhoofisha mtiririko wao wa fedha. Aidha, Mfuko wa PPF unatumia makadirio ya miaka 12.5 na Mfuko wa NSSF unatumia utaratibu wa kulipa pensheni ya mkupuo ya miezi 24, hali ambayo haina madhara kwa mifuko hii,” inasema wizara.

Ulinganisho wa vikokotoo limbikizi vinavyotumika kwa sasa kwa NSSF kwa mshahara wa Sh 1,000,000 kwa mwezi kwa kikokotoo cha asilimia 52.5 kwa umri wa miaka 30 kazini ni malipo ya mkupuo ya Sh milioni 12.6 na pensheni kwa mwezi ni Sh 525,000.

Mfuko wa PPF kwa mshahara huo huo kwa kikokotoo cha 1/600 kwa umri wa miaka 30 kazini ni malipo ya mkupuo ya Sh milioni 22.5 na pensheni ni Sh 450,000 kwa mwezi.

PSPF kwa mshahara huo huo wa Sh milioni moja kwa mwezi, kikokotoo limbikizi ni 1/540; na kwa umri wa miaka 30 kazini malipo ya mkupuo ni Sh milioni 62, ilhali pensheni kwa kila mwezi ni Sh 333,330.

Kwa Mfuko wa GEPF kwa kiwango hicho hicho cha mshahara, kwa kikokotoo cha 1/580 kwa umri wa miaka 30 kazini malipo ya mkupuo ni Sh milioni 28.862. Pensheni kwa mwezi ni Sh 465,520.

Nao Mfuko wa LAPF, kwa mwanachama anayestaafu baada ya miaka 30 akiwa analipwa mshahara wa Sh 1,000,000; malipo yake na mkupuo ni Sh milioni 62 na pensheni kwa mwezi ni Sh 333,330.

Wizara inataka muda wa wastani wa miaka ya kuishi upunguzwe na pia vikokotoo na malipo ya mkupuo vipungue kama njia ya kulinda mifuko. Hata hivyo, huenda hatua hiyo ikapingwa vikali na wastaafu wengi, hasa katika mifuko ambayo kwa sasa inawalipa mkupuo mkubwa.

 

Umri wa wanachama

Sehemu nyingine ambayo inalengwa kama sehemu ya mpango mahsusi wa kuiokoa mifuko ni kukabiliana na umri wa wastaafu.

Kwenye mapendekezo yake, wizara inasema: “Wastani wa umri wa wanachama wanaochangia Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ni kigezo muhimu katika kuona kiwango cha dhima ambacho Mfuko unalipa katika kipindi kijacho. Wastani wa umri wa wanachama unavyoongezeka ndivyo dhima ya Mfuko kwa wanachama inavyoongezeka.

“Katika tathmini imebainika kuwa wastani wa umri wa kuishi wa wanachama wanaochangia katika mifuko ya jamii hapa nchini ni wastani wa miaka 41.5. Hii ina maana kwamba katika kipindi cha miaka 18 ijayo (kuanzia mwaka mwaka 2014) idadi ya wastaafu itaongezeka kwa kasi kwa kuchukulia kwamba umri wa kustaafu katika sekta rasmi ni miaka 60.”

Wastani wa umri wa wanachama kwa kila Mfuko ni PSPF (43.3), PPF (41), NSSF (39), LAPF (42), na GEPF ni miaka 46. Umri wa wastani wa wanachama wa PSPF na GEPF uko juu ya wastani ikilinganishwa na NSSF na PPF.

Kwa tathmini ya Wizara ya Ajira, Kazi na Vijana, hii inamaanisha kuwa mifuko ya PSPF n GEPF ina wanachama wengi wanaokaribia kustaafu kuliko mifuko mingine, hivyo inahitaji fedha nyingi zaidi kulipa mafao ya wastaafu.

 

Serikali kulipa madeni

Kutokana na hali mbaya ya kifedha, hasa kwa baadhi ya mifuko, Wizara ya Ajira, Kazi na Vijana inapendekeza madeni hayo yalipwe haraka.

 “Madeni ya Serikali kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii yamechangia kwa kiasi kikubwa kudhoofisha uwezo wa mifuko hii na hata kusababisha kuwapo kwa wasiwasi wa uendelevu wao miongoni mwa wanachama. Sehemu kubwa ya madeni haya yametokana na deni la Mfuko wa PSPF; fedha zilizokopwa na Serikali kutoka mifuko hii na kuzitumia katika miradi ya maendeleo ya Taifa; na riba na tozo kutokana na Serikali (Awamu ya Nne) kutozingatia ratiba ya kulipa madeni yake.

“Hivyo, inapendekezwa Serikali ichukue hatua za haraka kulipa madeni yake kwa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ili kuimarisha uwezo wa mifuko na kuepuka matatizo ya mifuko hii kufilisika na kushindwa kutekeleza wajibu wake, hali ambayo itasababisha matatizo ya kiuchumi, kisiasa na kijamii,” imesema.

 

Utaratibu unaopendekezwa kulipa deni la PSPF

Kuna mapendekezo kadhaa yanayotolewa na Wizara ya Ajira, Kazi na Vijana kwa ajili ya kulipa deni la PSPF. Hatua za muda mfupi na kati kuanzia Julai, mwaka jana hadi Juni 2018 ni: “Serikali kulipa fedha kiasi cha Sh bilioni 10 kila mwezi kwa muda wa miaka minne.

“Serikali kubadili sehemu ya deni kuwa hati fungani za muda mfupi (treasury bills) za Sh bilioni 4.17 kila mwezi kwa miaka minne; na

“Serikali kubadili hati fungani za muda mrefu (treasury bonds) za miaka miwili na mitano za Sh bilioni 10 kila mwezi mwa miaka minne.”

Wizara inasema utekelezaji wa pendekezo la hatua za muda mfupi utaiwezesha Serikali kulipa Sh trilioni 1.22 hadi Juni 2018 sawa na malipo ya Sh bilioni 24.17 kila mwezi.

Kwa upande wa hatua za muda mrefu, mapendekezo ni: “Kubadili kiasi cha Sh bilioni 700 kuwa hati fungani za miaka saba ambako Serikali itabadilisha Sh bilioni 4.86 kila mwezi kwa miaka 12; na

“Kubadili kiasi cha Sh bilioni 700 kuwa hati fungani ya miaka 10 ambako Serikali itabadilisha Sh bilioni 4.86 kila mwezi kwa miaka 12.

“Utekelezaji wa pendekezo hili hadi kufikia Juni 2026 utaiwezesha Serikali kulipa kiasi cha Sh trilioni 1.22 kwa kipindi cha miaka 12.”

 

Kuwabana wanachama wanaojitoa

Serikali kwa sasa ipo mbioni kuanzisha utaratibu wa kisheria wa kuzuia wanachama wa mifuko kujitoa na kudai michango yao mapema kabla ya kufikisha umri wa kustaafu.

“Utaratibu unaopendekezwa ni wa kuanzisha bima ya ajira itakayotumika kuwalipa wafanyakazi wanaokuwa wamepoteza ajira zao katika kipindi wanachotafuta kazi nyingine. Utaratibu huu unaandaliwa na utawasilishwa serikalini kwa uamuzi,” inasema wizara na kuongeza:

“Wanachama wa mifuko kujitoa na kudai michango yao kabla ya muda wa kustaafu kisheria kunaathiri mtiririko wa fedha kwa mifuko.

Mifuko ya NSSF na PPF inatajwa kuathiriwa zaidi na utaratibu huu kwa kuwa ina wanachama wengi wanaotoka sekta binafsi.

 

Dau azungumza

Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Dk. Ramadhan Dau, anatamba kuwa Mfuko wake uko imara. Katika mahojiano na JAMHURI hivi karibuni, Dk.Dau anasema: Hatuna wasiwasi wowote. Sisi kwa mujibu wa sheria yetu kila baada ya miaka mitatu tunatakiwa tufanye tathmini ya Shirika, tathmini ya Mfuko. Na hili nimelizungumza sana.

“Katika biashara hizi za kawaida, mashirika kama Bandari, Reli, Air Tanzania, na kadhalika; ukitaka kujua uwezo wao unaangalia balance sheet (mizania) yao, Cash Statement na kadhalika, kwamba je, hili shirika mwaka jana au miaka mitano, sita nyuma utendaji wake ukoje, linakua au linadidimia?

“Unaangalia historical performance, lakini mifuko kama yetu ya Pensheni, pamoja na hilo ni muhimu, lakini muhimu zaidi ni kuangalia mbele. Mimi nimeajiriwa NSSF. Nakatwa mshahara nachangia. Interest yangu siyo kuona tu leo NSSF iko hai, lakini zaidi miaka 40 ijayo mimi nimeshastaafu hawa NSSF bado watakuwa na uwezo wa kulipa mafao? Shirika bado litakuwa hai?

“Ili ulijue hilo ndiyo hiyo Actuarial Valuation inakupa jibu. Kisheria inatakiwa kila miaka mitatu tufanye. Actuarial Valuation ya mwisho tumeifanya Septemba, 2015 ikaonesha kwa miaka 50 hatuna wasiwasi. Shirika linaweza kujiendesha lenyewe bila wasiwasi wowote.”

 

PSPF hali si nzuri

Wakati Serikali ikiendelea kuandamwa na deni la mifuko ya jamii, taarifa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango zinaonesha kuwa PSPF inaidai Sh bilioni 245 ambazo ni malimbikizo ya michango ya watumishi wa umma kwa miezi saba ya mwaka jana.

Hatua hiyo, kwa mujibu wa wizara hiyo, imeufanya Mfuko huo ukwame kuwalipa mafao baadhi ya wanachama wanaostahili kulipwa.

Kabla ya kupandishwa kima cha mishahara Julai, mwaka jana, Serikali ilikuwa ikipeleka michango ya wastani wa Sh bilioni 35 kila mwezi, lakini baada ya mabadiliko hayo kiwango hicho kimepanda hadi Sh bilioni 40 kwa mwezi.

Takwimu za Hazina zinaonesha kuwa mara ya mwisho kwa Serikali kupeleka michango yake ilikuwa Aprili, mwaka jana.

Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, katika ziara yake Makao Makuu ya PSPF mwishoni mwa mwaka jana, alisema Serikali ilikuwa ikidaiwa Sh bilioni 177, na kuwa kati ya kiasi hicho, ilishalipa Sh bilioni 154.

Dk. Kijaji akasema Novemba na Desemba mwaka jana, Serikali ililipa Sh bilioni 70, hivyo akaitaka PSPF iwalipe wastaafu hao ndani ya siku saba.

Lakini taarifa ya PSPF kwa Naibu Waziri huyo ilisema kiasi kilichopokewa ni Sh bilioni 35 pekee, hali inayozua maswali kujua kiasi kingine kilipelekwa wapi na Hazina.

“Ninachoshangaa ni kutoonekana kwa hundi za wastaafu hao wizarani na PSPF hazipo,” akasema Dk. Kijaji katika ziara hiyo.

PSPF ilimweleza Kijaji kuwa Sh. bilioni 35 zilitumika kuwalipa wastaafu 444 kati ya Aprili na Oktoba mwaka jana.

“Wastaafu 302 wamelipwa na wengine 142 waliofariki dunia malipo yao yamefanyika kwa ndugu zao kutokana na kiasi hicho cha fedha kilichotolewa na Serikali,” Mkurugenzi Mkuu wa PSPF, Mayingu, alimweleza Naibu Waziri.

Afisa wa Mawasiliano wa Wizara ya Fedha, Eva Valerian, aliiahidi JAMHURI majibu kuhusu sintofahamu hiyo, lakini alipotafutwa baadaye simu yake iliita bila kupokewa.

Chanzo cha habari kutoka Hazina kimethibitisha kuwa fedha za PSPF ni sehemu ya mabilioni ya shilingi ambayo Serikali ya Awamu ya Nne iliyaelekeza kwenye matumizi mengine, yakiwamo ya Uchaguzi Mkuu, semina, safari za viongozi ndani na nje ya nchi, zikiwamo za Kikwete, na matumizi mengine.

Ni kwa sababu hiyo, chanzo hicho kinasema, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, alifichwa taarifa sahihi wakati akienda PSPF kujua ni kwanini inasuasua kulipa mafao.

 

Mkurugenzi Mkuu LAPF anena

Mkurugenzi wa LAPF, Eliud Sanga, kwa upande ameiambia JAMHURI kuwa: “Kimsingi sisi tunadai, na fedha nyingi tulitumia kujenga Chuo Kikuu Dodoma, lakini ninachoweza kusema ni kwamba anayeweza kulizungumza hili vema ni regulator (SSRA).”

 

Majibu ya SSRA

Mamlaka ya Usimamizi na Udhibiti wa Sekta ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) kupitia kwa Afisa Uhusiano na Uhamasishaji wake, Sabato Kosuri, inasema: “Mamlaka imepokea malalamiko mengi kuhusu ucheleweshwaji wa mafao kwa wanachama, jambo ambalo ni kinyume cha Sheria ya Mamlaka Na. 8 ya mwaka 2008 iliyorekebishwa na Sheria Na. 5 ya Mwaka 2012 pamoja na Sheria zote za Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

“Mamlaka inapenda kuufahamisha umma, hususan wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii kwamba kwa mujibu wa Kifungu cha 35 cha Sheria ya Mamlaka, kulipwa mafao ni haki ya mwanachama pale anapokidhi vigezo vilivyowekwa kwa mujibu wa sheria.

“Hivyo, Mamlaka inakemea vikali tabia iliyozuka ya kuchelewesha mafao kwa wanachama kwa kisingizio cha kutopokea michango kutoka kwa waajiri. Ifahamike kwamba ni jukumu la Mfuko husika kwa mujibu wa sheria kukusanya michango kutoka kwa waajiri. Jukumu hili si la mwanachama,” anasema.

Anasema Mfuko unapochelewesha mafao unapaswa kumlipa mwanachama tozo kwa kiwango cha asilimia 15 kwa kila kiasi cha mafao kilichocheleweshwa.

Kwa mujibu wa kifungu cha 6(2), kupitia Waraka wa Mamlaka Na.1 wa mwaka 2016; Mamlaka imeielekeza mifuko yote kulipa mafao kwa wanachama wote waliokidhi vigezo kwa wakati.

Please follow and like us:
Pin Share