Tufute mfumo wa vyama vingi

Balile

Na Deodatus Balile

Ni wiki mbili sasa sijawa katika safu hii
kutokana na matatizo yaliyo nje ya uwezo
wangu. Naomba uniwie radhi msomaji.
Katika ‘Sitanii’ mbili zilizotangulia, niliahidi
kuzungumzia mbinu bora za kufanya
biashara na nikagusia wenzetu wa Morocco
walivyogeuza mwelekeo kwa kuruhusu
uwekezaji wa kuanzia dola 15,000 (yaani
Sh milioni 35 hivi) na jinsi walivyoweka
mazingira wezeshi katika biashara.
Sitanii, wiki iliyofuata ikaja ndege ya
Dreamliner, ambayo ilizua mjadala, nami
nikasimama kidete kusema bayana kuwa
ununuzi wa ndege una faida kubwa kwa
taifa hili kuliko hasara. Ukiacha suala la
heshima kwa taifa, usafiri wa ndege ni injini
ya utalii. Hakuna mtalii atakayekuwa tayari

kukamuliwa fedha ndefu kuja Tanzania na
kutumia muda mwingi kwenye viwanja vya
jirani Bujumbura na Nairobi, kisha useme
tutajenga utalii.
Kwa sasa utalii unachangia asilimia 17 ya
pato la taifa, na hii ni kwa wastani wa watalii
milioni 1.5, tunaowapata kwa tabu sana kwa
mwaka. Leo nauli ya ndege ya kutoka Dar
es Salaam kwenda Nairobi, Kenya ambako
ni mwendo wa saa moja inalingana katika
kipindi cha msimu wa tiketi za punguzo na
nauli ya kutoka Dar es Salaam kwenda
London, Uingereza.
Wakati Kenya Airways ikiwatoza watalii
wastani wa Sh 600,000 kwa safari ya
Nairobi – Dar – Nairobi, ambao ni umbali wa
saa 1, Kenya Airways hiyo hiyo inakuwa na
tiketi za punguzo za hadi Sh 800,000 kwa
safari ya Nairobi – London – Nairobi, umbali
ambao mtu anakaa hewani kwa saa 9. Hii
ina maana inakatisha tamaa watalii wenye
nia ya kuja hapa Tanzania kwa kuona nauli
inatisha. Ndege za Air Tanzania zitamaliza
kadhia hii.
Sitanii, wiki hii wakati nahangaika huku na

kule, nikasikia taarifa zilizonishtua. Nikasikia
kuwa Mbunge wa Ukonga (CHADEMA),
Mwita Waitara amejiuzulu ubunge na
kujiunga na Chama Cha Mapinduzi (CCM).
Nasikia na mwingine yuko njiani. Hatua hii
ya Waitara imekuja siku chache baada ya
wabunge Dk. Godwin Mollel wa Siha
(CHADEMA) na Abdallah Mtulia wa
Kinondoni (CUF), kuwa wamevihama
vyama vyao wakajiunga na CCM, kisha
wakateuliwa kugombea majimbo hayo hayo
kwa tiketi ya CCM na sasa wamo bungeni.
Mimi sina tatizo na uamuzi binafsi wa mtu
kujiuzulu uanachama wa chama chake na
kujiunga na chama kingine. Napata tabu
uamuzi huo unapotugharimu sisi walipa kodi
katika mazingira yanayotiliwa shaka.
Gharama tunazozitumia katika uchaguzi
mdogo iwapo tungezitumia kuchimba visima
vya maji, Watanzania wengi
wangeneemeka.
Si hilo tu, kinachokera zaidi ni kuona mtu
anaacha ubunge kisha anagombea ubunge
katika jimbo hilo hilo. Zimekuwapo tuhuma
za michezo michafu yenye lengo la kuua

ushindani wa kisiasa. Mbunge wa Singida
Kaskazini, Lazaro Nyalandu, alifanya kosa
hilo hilo la kujivua ubunge wa CCM na
kuingia kwenye upinzani (CHADEMA).
Naye akaliingiza taifa katika gharama ya
uchaguzi mdogo.
Sitanii, sababu zinazoelezwa na wabunge
husika wanaohama haziniingii akilini.
Najiuliza, tuna sababu gani ya kuendelea na
mfumo wa vyama vingi? Kwa nini kwa
mtindo huu tusifute mfumo wa vyama vingi
tukawa kama China? China wana chama
tawala cha CPC na vyama vya ushauri
(upinzani) vinane. Ushauri wa vyama hivi
unafanyiwa kazi bila kubezwa.
Tatizo ninaloliona hapa kwetu, inawezekana
elimu ya siasa hatujaielewa vema.
Tumechukulia ushindani wa kisiasa kama
uhasama, badala ya harakati za kuliletea
maendeleo taifa letu. Lakini pia nadhanai
wakati umefika kama nchi tuwe na utaratibu
wa kuwachunguza hawa wabunge
wanaohama vyama. Tuwachunguze hawa
kina Nyalandu, Mwita, Mtulia na Mollel.
Tuangalie akaunti zao zina fedha kiasi

gani? Tuangalie mali walizokuwa wanamiliki
kabla ya kuwa wabunge na mali
wanazokuwa nazo hadi wanajiuzulu, kisha
tulinganishe na mshahara wanaopata kama
vinaendana. Tukiendelea na utaratibu huu
wa watu kujiengua kwenye vyama tukaenda
kwenye uchaguzi mdogo, na pengine
utakuta mtu kama Mwita naye anagombea
tena kwa tiketi ya CCM, nadhani tutakuwa
hatuna sababu ya kuendelea na vyama
vingi nchini. Tuufute mfumo huu.

….Mwisho….