Kuvamiwa kwa mchezo wa soka na mamluki katika ngazi ya klabu na timu za taifa ni miongoni mwa sababu zinazochangia kudorora kwa mchezo huo nchini.
Akizungumza na JAMHURI, mchezaji wa zamani wa Klabu ya Yanga na timu ya Taifa ya Tanzania, Mohamed Hussein (Chinga One), amesema mchezo wa soka umevamiwa na mamluki wasiokuwa na dira wala mwelekeo wa kuuendeleza.
Mchezaji huyo ambaye enzi zake alijulikana kwa umahiri wa kucheka na nyavu, amesema itachukua miaka mingi kwa soka la Tanzania kupiga hatua endapo juhudi za haraka na makusudi hazitachukuliwa.
“Tunapaswa kuunganisha nguvu kwa pamoja ili kunusuru mpira wa Tanzania kutoka mikononi mwa watu wanaoitwa ‘wasaka tonge’,” amesema Hussein.

Amesema watu hao wamejipenyeza kuanzia ngazi za chini za uongozi kwa lengo la kutafuta umaarufu wa kisiasa bila ya kuwa na ufahamu wa mchezo huo.
Amesema vipaji vipya vya mpira wa miguu vimekuwa vikiibuka kila siku na kuacha historia kubwa nchini, lakini tatizo kubwa linakuwa ni uongozi ndani ya Shirikisho na klabu za soka nchini.
“Viongozi wengi tulionao hawana mipango madhubuti ya muda mrefu na mfupi ya kuhakikisha vijana na mpira kwa ujumla vinapiga hatua,” amesema Mohammed Hussein.
Amesema watu hao wamejipenyeza ndani ya klabu kwa kutumia nguvu ya fedha na kujikuta wakikabidhiwa uongozi ndani ya klabu hizo.

“Ufike wakati tukubali kujifunza kutoka kwa wenzetu waliotutangulia, mfano ukienda katika klabu kama Man united unamkuta Sir Bobby Charlton kwenye bodi ya klabu, Bayern Munich utamkuta Karl Heinz Rummenigge kama mmoja wa wakurugenzi,” amesema Hussein.
Mchezaji huyo amesema bila kukubali kujifunza kutoka kwa mataifa yaliyopiga hatua katika soka, si rahisi kwetu kuanza safari kuelekea waliko wenzetu.
Amesema maendeleo ya kweli yatapatikana pale soka na michezo mingine nchini itakapoongozwa na watu wenye dira na maendeleo.
Amesema tatizo jingine linalochangia soka letu kuendelea kudumaa ni wachezaji wenyewe kushindwa kujitambua na kuelewa wanahitaji nini.
Amesema wachezaji wengi nchini hawana nia ya kweli ya kuendeleza mchezo huo, na matokeo yake wametanguliza starehe mbele kuliko mchezo wenyewe.

“Katika miaka ya karibuni Tanzania imewahi kuwa na wachezaji mahiri wenye uwezo mkubwa lakini kutokana na kushindwa kujitambua tayari wamekwisha.
Mfano, kuna wachezaji wengi wa Kitanzania waliocheza na Emmanuel Okwi, raia wa Uganda, katika Klabu za Simba na Yanga na leo hawapo katika gemu,” amesema.
Amesema ni aibu kwa wachezaji wa hapa nchini, kwani wakati Okwi akiendelea kuvuna mamilioni wengi aliocheza nao wanacheza ndondo.
Mchezaji huyo ambaye wakati wake alikuwa akimudu kucheza nafasi ya ushambuliaji, amesema wachezaji wanatakiwa kujitambua kama wanahitaji kufika mbali katika soka.
“Leo mambo yamebadilika mpira unachezwa kwa uwazi, na ni miongoni mwa kazi zinazoendelea kuzalisha mabilionea duniani tofauti na miaka ya nyuma,” amesema.

Pamoja na hayo, amesema wachezaji wengi wa leo huweza kuwika kwa kipindi cha mwaka mmoja unaofuata anakuwa ameshapotea na kurudi mchangani na hii imesababishwa na kushindwa kujitambua.
Amesema vijana wanaocheza soka leo hawana budi kubadilika kifikra na kimtazamo na kuwa na maono ya mbali kuangalia namna ya kutoka hapo walipo.
Tatizo jingine amesema ni Serikali kutokuwa na mkazo wa michezo kwenye shule kama ilivyokuwa miaka ya nyuma ambako mpira ulikuwa ukichezwa kwa ngazi zote.
Gwiji huyo amesema nchi haiwezi kuwa na timu ya ushindani kama mipango itaendelea kuwa ya zimamoto kama ilivyo sasa.

“Wengi wa wachezaji waliowika miaka ya nyuma walipatikana katika michezo ya Umishumta, na Umiseta tofati na leo,” amesema Hussein.
Amesema hata gwiji wa Klabu ya Liverpool ya Uingereza, John Barnes, alipokuwa nchini, alisisitiza umuhimu wa kuwekeza kwa vijana kama nchi inahitaji maendeleo katika soka.
“Lazima tujiangalie kwa nini miaka ya nyuma nchi yetu ilikuwa ikitisha katika michezo, lakini leo kila kukicha tunaendelea kurudi nyuma,” amesema.
Amesema mabadiliko ya kweli yanatakiwa ili kuliokoa soka la Tanzania vinginevyo kama nchi tutaendelea kuwa wasindikizaji katika kila mashindano.

1080 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!