Tusipuuze taarifa hizi

Katika moja ya habari zilizochapishwa kwenye gazeti hili ni taarifa za tishio la ugaidi zinazotolewa na moja ya makundi ya kigaidi linalojihusisha ushambuliaji.
Wiki mbili zilizopita, magaidi wa al-Shabaab walifanya shambulio kubwa la kigaidi katika Chuo Kikuu cha Garisa, mpakani mwa Kenya na Somalia. Watu 148 waliuawa katika shambulio hilo.


Kadhalika, hivi karibuni kikundi cha kigaidi cha Boko Haram cha Nigeria kilitoa ahadi ya utiifu kwa ISIS, hatua iliyotafsiriwa na wachunguzi wa masuala ya ugaidi kuwa inaweza kuongeza nguvu za ISIS katika maeneo mbalimbali barani Afrika.
Wadau walizungumza katika taarifa hiyo, moja kwa moja wameiasa serikali kuwa makini kuhakikisha inavitumia vyombo vyake vya ulinzi na usalama na wananchi kukabiliana na tishio hilo kutoka al-Shaabab la Somalia.


Miongoni mwa viongozi hao waliozungumzia umakini huo ni Mbunge wa Kigoma Kusini – NCCR-Mageuzi, David Kafulila aliyeliambia gazeti hili kwamba ugaidi unaozungumzwa kila mahali nchini linaweza kufanyika kutokana na magaidi kutekeleza uhalifu huo bila kujulikana kirahisi.
Utaona kwamba Kafulila anaungwa mkono na Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi, anayesema kuwa hizi ni dalili mbaya kwa nchi maana suala la ugaidi haliangalii dini ya mtu wala kabila, bali ni kuchafuka kwa dunia.
Sisi wa JAMHURI tunaungana na kauli ya kiongozi huyo tukitoa tahadhari kuwa magaidi wanaweza kuwa ndani na nje kwa kuwa waandaaji, watekelezaji na wafadhili wa vitendo hivyo.


Kutokana na hali hiyo, tunasema kwamba itakuwa vyema kila Mtanzania akajitazama na kujitathmini kutokana na mchafuko uliopo ambao umekuwa tishio la amani ya dunia huku nchi nyingi duniani zikikumbwa na tishio la ugaidi na kupoteza watu wake.
Ukweli ni kwamba ni lazima iwe dhima ya kila Mtanzania kuhakikisha nchi inakuwa na amani kama ambavyo tunashauri, wananchi kutoa taarifa kwa vyombo vya ulinzi na usalama pindi linapobainika jambo lisilo la kawaida.
Hii ni kwa sababu mwaka huu ni mwaka wa uchaguzi mkuu hivyo si ajabu suala la ugaidi kuhusishwa na masuala ya kisiasa.


Kwa msingi huo, tunatoa tahadhari kwa Watanzania na wageni walioko nchini kuepuka mikusanyiko kama isiyo ya lazima kama vile shule, misikiti, makanisa na kwenye sherehe.
Tunasema hivyo kwa sababu tishio la magaidi ni hatari na wala tusipuuze taarifa za nchi yetu kutaka kuvamiwa na watu hao wabaya.