Ujerumani kuilipa Namibia fidia

WINDHOEK, NAMIBIA

Zaidi ya miaka 100 baada ya serikali yake ya kikoloni kufanya matendo ya kikatili kwa wakazi wa Namibia, Ujerumani imetambua makosa hayo kama mauaji ya kimbari.

Ukatili huo ulifanywa dhidi ya watu wa jamii za Herero na Nama, na sasa Ujerumani imeamua kuilipa Namibia fidia ‘kiaina’ kutokana na makosa iliyoyafanya.

Ujerumani imekubali kutoa fidia hiyo kupitia misaada katika miradi ya maendeleo yenye thamani ya Euro bilioni 1.1 (dola za Marekani bilioni 1.3) itakayotolewa kwa Namibia katika kipindi cha miaka 30 ijayo.

Aidha, Ujerumani imeomba msamaha rasmi kutokana na makosa hayo.

Hayo yamebainishwa na Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Heiko Maas, katika taarifa aliyoitoa wiki iliyopita.

“Lengo letu ni kutafuta namna ya pamoja na kumaliza tofauti zilizopo kama kumbukumbu kwa walioathirika. Hii ni pamoja na kutambua kuwa mambo yaliyotokea wakati Ujerumani ikiwa mtawala wa eneo ambalo leo ni Namibia, hasa mauaji kati ya mwaka 1904 na 1908, kuwa ni mambo mabaya. Kuanzia sasa tutatambua mambo hayo kama mauaji ya kimbari,” alisema Maas.

Serikali imekubaliana na kauli hiyo ya Ujerumani na kuiona hatua muhimu kuelekea mapatano baina ya pande hizo mbili.

Msemaji wa Ikulu ya Namibia, Alfredo Hengari, aliiambia CNN: “Huu ni mwelekeo mzuri sana katika mchakato wa muda mrefu ambao umeharakishwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Watu hawatasahau mauaji haya ya kimbari, wanaishi nayo. Hii ni hatua muhimu kuponya makovu waliyo nayo.”

Kwa mujibu wa kumbukumbu kutoka jumba la makumbusho la mauaji ya kimbari huko Marekani, kati ya mwaka 1904 na 1908, askari wa kikoloni wa Ujerumani waliwaua zaidi ya watu 80,000 wa jamii za Herero na Nama wakati wakizima harakati za watu waliokuwa wanapinga kukandamizwa na wakoloni.

Kwa mujibu wa wanahistoria, mapigano hayo yaliyosababisha umwagaji mkubwa wa damu, yalitokea wakati watu wa jamii ya Herero walipoasi hatua ya watawala wa Kijerumani kunyang’anya ardhi yao.

Ujerumani iliomba radhi kwa mara ya kwanza mwaka 2004 na tangu mwaka 2015 nchi hizo mbili zimeendesha mazungumzo kuhusu fidia hiyo.

Sanamu ya kumbukumbu ya mauaji yaliyowakumba watu wa jamii za Herero na Nama, yaliyofanywa na askari wa kikoloni wa Ujerumani kati ya mwaka 1904 na 1907 nchini Namibia.