*Malipo ya ndege utata mtupu

*Wahusika wakalia kuti kavu

*Waziri Membe aingilia kati

 

Kukiwa na taarifa kwamba uongozi wa juu serikalini umeagiza kuchunguza ulaji wa mamilioni ya shilingi wakati wa Mkutano wa Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote (Smart Partnership Dialogue), siri nzito za ufisadi zimeendelea kuanikwa.

Hali hiyo imemlazimu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe, atake maelezo ya kina ya matumizi ya fedha.

Uchunguzi unaonesha kuwa Membe hakuhusishwa, hasa kwenye hatua za mwisho za maandalizi ya mkutano huo, hali ambayo watu walio karibu naye wanasema ilimtia shaka.

Kwa upande wake, Waziri huyo amezungumza na JAMHURI katika mahojiano maalum, na kukiri kuwa amewataka wahusika wampe ripoti ya mambo yalivyokuwa, hasa matumizi ya fedha.

 

Amesema amefikia hatua hiyo kutokana na taarifa zilizoandikwa na gazeti hili zikiwahusisha baadhi ya maofisa wa Serikali kutoa zabuni tata za mamilioni ya shilingi kwa kampuni tano, lakini tatu kati ya hizo zikiwa “hewa”- kwa maana ya kutokuwapo kwenye Daftari la Wakala wa Usajili wa Kampuni (BRELA).

 

Wakati Membe akiwakomalia watumishi hao, kumepatikana habari nyingine kwamba dola 103, 533 (Sh milioni 165.652 kwa kiwango cha Sh 1,600 kwa dola moja ya Marekani), zimetumika kulipa tiketi za ndege za baadhi ya waalikwa.

 

Hata hivyo, habari nyingine zinasema wageni hao walijilipia wenyewe tiketi, lakini huku zimeoneshwa kwenye taarifa kwamba zililipwa na Kamati ya Smart Partnership.

 

Imeelezwa kwamba miongoni mwa waliolipiwa ni pamoja na marais wastaafu wawili – Joaquim Chissano wa Msumbiji, na Jerry Rawlings wa Ghana.

 

Wengine ni Martin Laing (Malta), Charles Masefield (London, Uingereza),  Thomas de Gregori na Gayle de Gregori (Houston, Marekani), Dianne Lalla (Antigua & Berbuda), Basil Springer (Trinidad), Susan Feindel (Halifax), Lira Ralebese (Maseru), Louis Paul (Kuala Lumpur),  Armando Pedro (Maputo), Rozina Jacob (Windhoek); na Vivian Ahumuza, Edwards Asiimwe, Andrew Kaahwa, Fred Opolot, Thaddeo Kasaija, Jeremiah Lubowa, Joseph Nkodyo, David Senyange, Racheal Turyamwijuka, na Robert Tusiime (Entebbe).

 

Wengine ni Raina Zarb, Kirit Dal, Brinda Dal, Helena Twist, Michael Wright, Joseph Clarke, Johnson Kyeswa, na Ian Strachan (London), Crusivia Hichikumba, na Willem Lourens (Lusaka), Augustino Muambe (Maputo), Kobina Amoakwa (Accra).

 

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Sekretarieti ya Smart Partnership Dialogue, Victoria Mwakasege, alipoulizwa kama Tanzania ndiyo iliyogharamia tiketi za wageni hao, aling’aka.

 

“Ukiniuliza mimi sina jibu, sijui mna guts (ujasiri) gani, mnaandika tu tuhuma za ajabu. Mnamfahamu Mungu? Kama mnataka taarifa, mzitafute kwa Mungu, mmeamua kuandika, andikeni tu. Mimi siwajibiki kwa hayo masuala. Mnamjua anayewajibika,” alisema na kukata simu.

 

Kampuni zilizotoa michango

Hadi Juni 17, mwaka huu, kampuni na taasisi 17 za hapa nchini zilikuwa zimechanga Sh milioni 329.

 

Waliochanga na kiwango kwenye mabano ni Benki Kuu ya Tanzania (Sh milioni 10), Benki ya CRDB (milioni 80), Benki ya Watu wa Zanzibar (Sh milioni 12), Vodacom Tanzania Limited (huduma bure ya mawasiliano kwa washiriki 600), Tigo Tanzania (Sh milioni 80), Barrick Gold (Sh milioni 15), PPF (Sh milioni 20), NSSF (Sh milioni 20), LAPF (Sh milioni 20), GEPF (Sh milioni 10), PSPF (Sh milioni 20), TANAPA (zawadi mbalimbali), Masasi Foods Industries Limited (maji ya kunywa), Huawei (mkutano kwa njia ya mtandao), CBA (Sh milioni 5), Azania Bank (Sh milioni 5), na Techno Brain Ltd (Sh milioni 32).

 

Hadi Juni 17 kampuni nyingine 20 zilikuwa zikisubiri uamuzi wa menejimenti au bodi zao, kampuni sita zilisema uwezo wake wa kifedha ni mdogo na wakuu wa kampuni mbili walikuwa nje ya nchi.

 

Sokomoko

Baadhi ya vifaa vilivyoorodheshwa kwenye zabuni hizo, ama havikuwasilishwa, au viliwasilishwa shughuli ikiwa imeshamalizika, na sasa vimetunzwa maghalani. Miongoni mwa vifaa hivyo ni shehena kubwa ya bendera za Tanzania ambazo licha ya kutotumika, rangi zake zilikosewa.

 

Wahusika wakuu kwenye ulaji huu ni maofisa kadhaa wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa waliokuwa waratibu wa ugeni huo. Uchunguzi umethibitisha kwamba Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue, aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Uendeshaji wa Majadiliano ya Kimataifa ya Ushirikiano kwa Manufaa ya Wote, hakuridhishwa kabisa na namna zabuni zilivyotolewa.

 

Kwenye kikao cha mwisho, Sefue, kwa maandishi, alisema ingawa yeye ameshiriki katika Kamati ya Uendeshaji, hakubaliani na bajeti pamoja na mchanganuo wa zabuni ulivyokosa uwazi.

 

Sefue amenukuliwa akisema ni jambo gumu kwake kukubaliana na ununuzi huo kwa vile hapakuwapo mchanganuo wa kuthibitisha namna mamilioni ya shilingi yalivyotengwa kuwalipa wazabuni na bei za vifaa vilivyohitajika.

 

Vyanzo vya uhakika kutoka ndani ya kikao kilichofanyika Juni 17, vinasema Balozi Sefue aliweka wazi msimamo wake baada ya kuona taratibu za ununuzi zikiwa zimekiukwa, na kuwa baadhi ya vitu vilivyoorodheshwa vilikuwa ni “vichekesho”.

 

“Mimi sitaki nihusishwe na jambo hili, waliolifanya wanapaswa wenyewe wabebe msalaba huu, mchanganuo uletwe ili kuonesha nini kinanunuliwa kwa kiasi gani badala ya utaratibu huu wa kuorodhesha vitu na kuweka gharama,” alinukuliwa aking’aka Balozi Sefue.

 

Kampuni zilizopata zabuni

Kampuni ya Luma International Ltd ilipewa zabuni ya kusambaza vitu mbalimbali vyenye thamani ya Sh milioni 391.1. Baadhi ya vitu hivyo ni vipeperushi, bendera za Tanzania (kubwa na ndogo), suti kwa watu wa itifaki, sare kwa watu wa mapokezi, mabegi kwa wageni mashuhuri na wageni wa kawaida, na beji.

 

Kampuni ya Softel Trading Company Limited ilipewa zabuni ya Sh milioni 392.6 kusambaza picha za mapambo ukumbini, miavuli 1,500, chupa za kahawa 800, vikombe vya kahawa 800, kalamu za zawadi 2,000 na vishikio vya funguo 800.

 

Kampuni hiyo hiyo ilipewa zabuni nyingine ya Sh milioni 48.25 kwa ajili ya kufanya kazi za usanifu kwa kutumia kompyuta na uchapaji wa mabango madogo madogo.

 

Kana kwamba hiyo haitoshi, kampuni hiyo hiyo ya Softel Trading Company Ltd ilipewa zabuni ya thamani ya Sh milioni 254 kwa ajili ya kutengeneza mabango makubwa 40. Wakati mkutano ukiwa unafanyika Dar es Salaam, iliamuriwa kwamba mabango hayo yasambazwe katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Mbeya, Dodoma na Zanzibar.

 

Kampuni ya Wild Cat Publishing ilishinda zabuni ya Sh 278,409,409,269 kwa ajili ya kuandaa machapisho 1,000 ya mkutano. Yalitakiwa yahusu masuala ya kisiasa, kiuchumi, fedha, teknolojia, mawasiliano, usafirishaji, kilimo, ujenzi, afya na elimu, utalii, n.k.

 

Kampuni ya tano iliyoshinda zabuni ni ya Big Mama’s Woodworks iliyopangiwa Sh milioni 29.96 kwa ajili ya kutengeneza zawadi za vinyago 60 yenye urefu wa sentimita 15 na upana wa sentimita 12 kila kimoja. Pia ilitakiwa itengeneze vinyango vinne vyenye urefu wa sentimita 150 na upana wa sentimita 35.

 

Kwenye masuala ya burudani, Kampuni ya Prime Time Promotion ilijipatia zabuni ya Sh milioni 194.7.

 

Kwenye orodha ya ugawaji zabuni, Kampuni ya True Colour Entertainment Group ilizawadiwa zabuni ya Sh milioni 50 kwa ajili ya kuandaa na kuonesha jarida. Ingawa haikufafanuliwa, hii yawezekana ndilo lile jarida lililooneshwa kwenye Ukumbi Kimataifa wa Mikutano wa Mwalimu Nyerere, siku ya ufunguzi wa Mkutano wa Smart Partnership. Lilihusu wanyamapori na vivutio kadhaa vya utalii vinavyopatikana hapa nchini.

 

Zabuni ya nane ilitolewa kwa Kampuni ya Simply Computers (T) Ltd. Iligharimu Sh milioni 187.478. Ilitakiwa kusambaza kompyuta kubwa mbili, idadi kama hiyo kwa kompyuta za ukubwa wa kati na projekta nne.

 

Kampuni hiyo hiyo ya Simply ilipata zabuni nyingine yenye thamani ya Sh milioni 210.198 kwa ajili ya kusambaza kompyuta tano za mezani, laptop (5), laptop za sekretarieti na mkutano (14), mobile computing equipment (14), black and white printer (2), colour printer (2), kompyuta za mezani (nyingine 5), colour printer (nyingine 2) na flash disk (32).

 

Kampuni tatu kati ya hizo, zimebainika kuwa ni ‘hewa’, hiyo ikiwa na maana kwamba hakuna kodi stahiki iliyolipwa TRA.

 

By Jamhuri