Umri wa Ekelege wa ‘TBS’ utata mtupu

Umri wa Mkurugenzi wa Shirika la Viwango Tanzania (TBS) aliyesimamishwa, Charles Ekelege umezua utata kutokana na yeye mwenyewe kujaza taarifa zinazoonesha miaka tofauti ya kuzaliwa kwake.

Ekelege ambaye anatuhumiwa kwa rushwa na matumizi mabaya ya ofisi alitakiwa kustaafu Januari 2014.

Lakini kutokana na utata wa umri wake, sasa huenda akastaafu 2016.

 

Katika taarifa za kupima utendaji kazi (Annual Appraisal Report) Ekelege aliajiriwa na TBS Aprili 24, 1982.

 

Kwa mujibu wa taarifa alizojaza katika fomu hizo mwezi Julai 1991 hadi Juni 1992, Julai 1992 hadi Juni 1993 na kwenye hati yake ya kusafiria zinaonyesha zinaonesha tofauti katika kipengele cha umri wake.

Fomu alizojaza Julai 1991 na Juni 1992 anaonesha alizaliwa Januari 18, 1954. Lakini katika fomu za Julai 1992 na Juni 1993  anaonesha alizaliwa Januari 18, 1956. Kwenye hati ya kusafiria pia inaonesha kuwa alizaliwa mwaka Februari 25, 1956.

 

Ekelege ambaye huenda akarudishwa kazini, anachunguzwa na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

 

Hatua hiyo inatokana na Kamati ya Bunge ya Mashirika ya Umma (POAC) kubaini kuwa chini ya uongozi wake, TBS iliingizia hasara Serikali kutokana na ukaguzi wa magari nje ya nchi.

 

Ilibainika kuwa mabilioni ya shilingi kwenye ukaguzi huo yaliishia mikononi mwa wezi.

Madudu hayo yalibainika baada ya kamati hiyo kutembelea vituo vya ukaguzi wa magari nchini Singapore na Hong Kong.

 

“Tulikwenda Hong Kong na Singapore na tumegundua kwamba TBS ni wababaishaji, huwezi kuamini anachokifanya Mkurugenzi (Ekelege) huko nje”,

 

“Ninasema haya bila woga wowote na hata nikiwekewa sumu, wajumbe wengine wa kamati yangu watasema,” alisema Deo Filikunjombe ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo.

Kamati hiyo ilipotembelea Hong Kong, iligundua kuwa ukaguzi wa magari haufanyiki na kwamba fedha zinazotolewa na wanunuzi zinaliwa na wajanja.

 

Ekelege aliwapeleka wajumbe wa kamati hiyo katika ofisi hewa ambayo baadaye waliigundua kuwa haikuwa ya ukaguzi wa magari.

 

Ekelege ambaye katika fomu zake za utendaji kazi maoni ya mwajiri wake yanamtaja kuwa mtu mwadilifu na mchapakazi, anatuhumiwa kununua cheti feki cha TBS mtaani ili kuhalalisha ofisi hizo feki za ukaguzi wa magari ya nje ya nchi.

 

Hata hivyo kamati hiyo ilipokwenda Singapore pia haikukuta kampuni ya kukagua magari na kwamba alipomuulizwa Ekelege alishindwa kuwapeleka zilipo ofisi za ukaguzi wa magari.

Hatua hiyo ya Ekelege kuidanganya kamati hiyo ilimpa hasira Mbunge wa Mwibara (CCM), Kangi Lugora  hivyo kutaka kupigana na Ekelege.

 

Halikadhalika uchunguzi uliofanywa na JAMHURI umeabaini kuwa wakati wowote kuanzia sasa Ekelege aliyesimamishwa kazi mwaka mmoja uliopita, atapandishwa kizimbani kujibu tuhuma za rushwa na matumizi mabaya ya ofisi.

 

Taarifa za uhakika zilizolifikia kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) zilisema uchunguzi dhidi ya Ekelege unaelekea ukingoni.

 

“Tuhuma za msingi ni za ukaguzi wa magari. Wabunge walikwenda Hong Kong waliyoyashuhudia ni aibu tupu, lakini mbaya zaidi amejipatia mamlaka ya kusamehe madeni wadeni wa TBS jambo ambalo ni kinyume cha sheria,” kilisema chanzo chetu kutoka TAKUKURU.

 

Taarifa zinaonesha kuwa Ekelege alitumia kampuni tata tatu za Jaffer Ali Mohamed ya Dubai, Quality Motors Limited ya Hong Kong na Planet Automotive Pty iliyodaiwa kuwapo Singapore.

 

“Mambo mengine ni aibu, kampuni hizi zilikuwa hazina hata mtambo mmoja wa kukagua ubora wa magari, lakini Ekelege akawa anasisitiza kuwa zinafanya kazi kwa ufanisi, hadi wabunge walipobaini ujanja huo,” kilisema chanzo chetu.

 

Uchunguzi ulionesha kuwa kampuni hizo tatu zinazomtia matatani Ekelege nyaraka za usajili zinaonesha kuwa zinamilikiwa na mtu mmoja, ajulikanaye kwa jina la Said Abood.

Chini ya mkataba unaodaiwa kuingiwa kati ya kampuni hizi na TBS, kampuni zilipaswa kuwasilisha asilimia 25 ya mapato yatokanayo na ukaguzi wa kila gari, lakini hadi Ekelege anasimamishwa kazi wakubwa hawa walikuwa hawajalipa.

 

Ukiacha kutokagua magari na kutotoa hiyo asilimia 25 iliyokubaliwa, kuna nyaraka zilizokusanywa na maafisa uchunguzi zinazoonesha kuwa Ekelege alikuwa anazisamehe kampuni hizo  asilimia 25 baada ya kuandika barua kwake na kusema hazina uwezo wa kulipa kiasi hicho.

“Mamlaka ya kusamehe deni kwa TBS ni ya Bodi na si ya Mkurugenzi Mkuu. Ekelege alijipa madaraka makubwa.

 

Taarifa zilizopo zinaonesha kuwa Ekelege alisamehe hadi dola 45,000 za Marekani. Hadi sasa kampuni hizo zinadaiwa dola 50,000.

 

Uchunguzi umeonesha kuwa Ekelege aliyesimamishwa kazi Mei 20, 2012 ikiwa umetimia mwaka mmoja, bado anaendelea kupata mshahara na mafao mengine ambayo ni wastani wa Sh milioni tano kwa mwezi.

Juhudi za kumpata Ekelege zimeshindikana. Mwandishi alipokwenda nyumbani kwake jijini Dar es Salaam aliambiwa amesafiri nje ya nchi.