Ninaandika makala haya baada ya kumtembelea Frank Mwaisumbe na kubadilishana naye mawazo, wiki mbili zilizopita. Ni mfanyabiashara aliyepo mjini Iringa anayemiliki kampuni ya uwakala wa safari za anga iitwayo Getterland Company Limited. Mwaisumbe pia ni mmoja ya waasisi wa Shirika la Mindset Empowerment linaloendesha mashindano ya mbio za Ruaha Marathon.

Nilimfahamu zamani kidogo na kuna kitu cha kusisimua hapa; kwa sababu ni mwalimu aliyenifundisha kozi ya masoko nikiwa Chuo Kikuu Tumaini kilichopo Iringa. Mtakumbuka wiki iliyopita nilieleza namna wasomi wetu (wahadhiri, maprofesa na madaktari wa biashara) wanavyokwama kuzalisha wafanyabiashara halisi kwa kufundisha mambo ambayo wenyewe hawayatendi.

 

Mwaisumbe ni mmoja kati ya wahadhiri ambao walinipa hamasa kubwa kibiashara kwa sababu alikuwa akifundisha biashara halisi na alikuwa mfanyabiashara aliyefanya biashara nyingi. Vyuo vyetu nchini vinawahitaji watu kama Mwaisumbe katika kuwasaidia wahitimu wetu kujiajiri badala ya kulilia ajira ambazo ‘hazipo’.


Ninashirikiana kwa ukaribu na Mwaisumbe katika Mindset Empowerment; mimi nikiwa Mratibu. Kuna mambo mengi kuhusu uzoefu wa kibiashara ambayo nimejifunza kutoka kwake. Siku niliyomtembelea tulitumia muda mwingi kujadili mipenyo, staili, mbinu na mambo yanayosababisha wafanyabiashara mbalimbali duniani kufanikiwa. Nimejifunza mengi katika mazungumzo hayo na nikakumbuka visa vingi vilivyowahi kunipata katika harakati zangu za kibiashara.

 

Katika kujadili tulibaini kuwa hakuna mfanyabiashara yeyote duniani anayesimama mara moja kirahisi. Kila mfanyabiashara aliyefanikiwa ukimfuatilia historia yake atakueleza namna alivyoanguka-anguka na kusimama, namna alivyojaribu mambo mengi lakini akafanikiwa katika machache, ama katika moja, na namna alivyopokea upinzani mkali katika kufanikisha hilo unaloliona limefanikiwa.


Binafsi ninakumbuka mtaji wangu wa kwanza niliupata (kwa jasho langu mwenyewe bila kupewa na mtu) nikiwa na miaka 19 kwa kuchuuza vitunguu kutoka Mang’ula, Karatu na kuvipeleka mjini Arusha. Ilikuwa ni biashara niliyoipatia ipasavyo kiasi cha kuweka malengo ya kuanzisha chuo cha mafunzo ya kompyuta na biashara.


Ndani ya mwaka mmoja nilifanikisha lengo langu hilo kwa kufungua chuo hicho wilayani Mufindi.  Nakumbuka thamani ya kile chuo ilikuwa takriban Sh milioni 20. Nilijiona niliyefanikiwa na kila nilikokuwa ninapita nilikuwa ninapokea heshima na pongezi za mafanikio hayo hasa ikizingatiwa kuwa nilikuwa nimezikamata ‘milioni’ nikiwa mdogo wa miaka 20, tena nikiwa ndio kwanza nimehitimu kidato cha sita.


Ukweli ni kwamba saa niliyodhani kuwa nime-win kumbe ndio saa ambayo nilikuwa naelekea kuanguka. Ile biashara ilianguka yote ndani ya miezi miwili, nikawa sina kitu! Kufilisika kwangu kulitokana na mambo mawili. Mosi, wafanyakazi niliowaajiri kuendesha chuo walijigeuza miungu watu, wakaanza kuwanyanyasa wanafunzi na kuzembea kufundisha. Nilipewa taarifa mwishoni mambo yakiwa yameharibika, niliambiwa kuwa wamebaki wanafunzi wanane kati ya wanafunzi 104 waliokuwa chuoni!

 

Nilichanganyikawa na nikaenda haraka sana kuwatimua kazi, lakini nikawa nimechelewa na mambo yalikuwa yameshaharibika. Pili; kulitokea shoti ya umeme (kwa uzembe wao) na ukaunguza sehemu kubwa ya vifaa vya chuo kile zikiwemo kompyuta na vifaa vingine. Sikuwa na ujanja zaidi ya kukifunga na kukubali matokeo ya kufilisika.

Leo hii ninapojikumbusha kuhusu biashara ile namtafakari mwandishi aitwaye Mchungaji Daktari Robert Schuller aliyeandika kitabu kiitwacho, “Success is Never Final Failure is Never Ending”. (Kufanikiwa sio kikomo na kushindwa sio mwisho). Anamaanisha kuwa ukifanikiwa usijisahau na ukianguka usikate tamaa.


Ukweli ni kwamba kwenye biashara kuna mapito mengi kiasi ambacho mfanyabiashara unahitaji uvumilivu mkubwa mno kuendelea. Biashara sio lelemama! Unaweza kutumia miaka mingi katika kujenga biashara zako na kukusanya mali; lakini baadaye ukapoteza kila kitu ndani ya dakika chache. Huhitaji kukata tamaa, unahitaji uvumilivu na kuanza upya. Huo ndio ujasiriamali. Sifa ya mjasiriamali ni kutokukata tamaa.


Unadhani mchezo umeishia hapo? La hasha! Sikukata tamaa, nilisimama na kuanza kujikongoja tena; safari hii nikaamua kufanya biashara ya kukusanya na kuuza alizeti wilayani Njombe katika maeneo ya Irembula. Kama kawaida, si rahisi kufanya biashara peke yako; ni lazima uwe na watu. Hata huko kwenye alizeti nilikuwa na watu niliowaamini kunikusanyia na kunitunzia.


Mwanzoni nilikwenda vizuri; nikajisemea moyoni; loo! Biashara si ndio hii? Kumbe nilikuwa nimepotea kwani mkasa mwingine ukanitokea. Nikiwa nimekopa fedha kutoka kwa watu na kukusanya alizeti kwa wingi huku nikijua nitakapoiuza nitakuwa milionea; nikadhulumiwa mchana kweupe! Mwenye eneo nilipotunza alizeti akauza magunia yote kisha akatoroka na fedha zote na hadi leo ninapoandika makala hii ikiwa imepita miaka kadhaa sifahamu alipo.


Huu ukawa ni msiba mwingine kibiashara kwangu. Tena ni bora angekuwa alitoroka na mtaji wangu pekee; lakini aliondoka na hela hata nilizokopa; hii ina maana nilipoteza mtaji wote nikabakiwa na madeni. Hii ndio biashara, sikukata tamaa ndio maana hadi leo ‘nimekomaa’ na biashara. Kimsingi sina miaka mingi kiumri na wala sina miaka mingi sana katika biashara, lakini kuna visa vingi mno vya kushindwa na kufanikiwa vilivyonitokea hadi sasa kiasi kwamba nikisema nivilete vyote gazeti zima halitatosha kwa juma moja.


Hata hivyo; katika mikasa yangu miwili niliyoileta hapo juu kuna mambo machache napenda uyajue ambayo Mwaisumbe amenisaidia kuyajua. Mosi, unapokuwa katika biashara unatakiwa uwe na imani isiyoteteleka ya kuwa kuna siku utafanikiwa. Inawezekana ukawa unafanya biashara lakini haujui ‘utatoka’lini.


Inawezekana umeshapata hasara nyingi mno katika biashara zako; lakini kama ukibaki na imani hii hakika ipo siku utafanikiwa. Mwaisumbe huwa anapenda kusema hivi “Mtu aliyeanguka-anguka sana katika ujasiriamali, siku akiinuka, hataanguka tena. Anayeanguka na kusimama hahofii kuanguka kesho kwa sababu anajua ataamka tu.”


Pili, asilimia kubwa ya wajasiriamali tunaangushwa sana na watu wengine, ama tunaowaamini, tunaowaajiri au tunaoamua kupanda nao kibiashara. Pamoja na uweli huu; haimaanishi kuwa usiwaamini watu, la hasha! Jambo la kufanya ni kuhakikisha unajitahidi kadiri uwezavyo kutafuta, kushirikiana na kuajiri watu sahihi katika ujasiriamali wako. Itakumbukwa kuwa nimewahi kuandika kupitia gazeti hili makala yenye kichwa; “Mjasiriamali na Sayansi ya kuajiri wafanyakazi.”

 

Tatu, unapofanya ujasiriamali ama kama unatamani kuingia katika ujasiriamali hutakiwi kuogopa kupoteza mtaji au hatua uliyonayo. Kitu cha thamani katika ujasiriamali siyo mali ama fedha unazofanikiwa kuzipata; bali ni ‘akili ya fedha (financial IQ)’, kujiamini na uzoefu unaoupata kila unapofanya biashara. Ni vema mjasiriamali kujenga ujasiri na kujiamini kiasi ujisemee kuwa; “Hata kama nikipoteza kila kitu nilichonacho leo, ninaweza kurudisha na zaidi ya nilivyokuwa navyo.”

stepwiseexpert@gmail.com;  0719 127 901


1654 Total Views 1 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!