Kwa muda mrefu sasa, nimejijengea utamaduni wa kujisomea vitabu. Sisomi kila aina ya vitabu, isipokuwa ninapenda sana vitabu vya biashara na uchumi (finance, economic, entrepreneurship and business), vya uhamasisho na shuhuda (motivational and inspirational) na vinavyohusu ustawi wa kiroho na kimaisha (spiritual and personal improvements). Mara chache sana huwa nasoma vitabu vinavyohusu siasa hasa zile za kimataifa.

Nimejiwekea ratiba ya kusoma angalau vitabu viwili kila mwezi, sawa na vitabu 24 kwa mwaka. Pia ni msikilizaji mzuri wa rekodi zenye maudhui kama ya vitabu nilivyovitaja. Pamoja na kusoma kote vitabu, huwa nina mchujo mkali wa vitabu vya kusoma kutegemea na sifa za mwandishi husika.


Daima huwa nasoma kazi za waandishi ambao wamepitia kwa vitendo waliyoyaandika na si wanaoandika nadharia. Kama ni kitabu kinachohusu biashara nitakisoma ikiwa tu mwandishi ni mfanyabiashara, kinyume cha hapo sikisomi hata kama aliyekiandika ni profesa. Sisomi kazi za wenye vyeti vikubwa vya madarasani, ninasoma kazi za wenye uzoefu kwa yale waliyoyaandika kivitendo.

 

Ndiyo maana ninapenda sana vitabu kama ‘Guide to Investing’ (Robert Kiyosaki), ‘As a Man Thinketh’ (Allen James), ‘Secrets of Millionaire Minds’ (T Harv Eker), ‘Think and Grow Rich’ (Napoleon Hill) kwa kuvitaja vichache. Nawapenda waandishi hawa kwa sababu wameandika kile walichokiishi. Huu ni mtazamo na msimamo wangu. (Usijichoshe kuuhoji wala kuukosoa).


Mtazamo na msimamo wangu huu ulisababisha kupishana na wahadhiri wangu wakati nikisoma chuo kikuu, shahada ya kwanza ya usimamizi na utawala wa masuala ya biashara. Sikuwa na ugomvi katika masomo mengine isipokuwa katika masomo mawili ambayo kwa muono wangu yamebeba kiini cha shahada hiyo.


Somo la kwanza lilikuwa ni la ujasiriamali (Entrepreneurship, Small business management & International Entrepreneurship), na jingine lilikuwa ni uanzishaji na usimamizi wa miradi (Projects Planning and Management).


Kabla hawajaanza kunifundisha nilitaka kufahamu sifa walizonazo katika maeneo hayo. Wa ujasiriamali nilitarajia angekuwa mfanyabiashara mkubwa, na yule wa miradi mmiliki wa miradi halisi iliyofanikiwa.


Kwa bahati mbaya hawakuwa na sifa nilizozitazamia (uzoefu wa vitendo katika maeneo hayo), badala yake walikuwa ni wasomi wenye shahada nyingi na sifa zinazong’aa katika vyeti vyao, wenyewe wanaita ‘CV’. Nakiri wazi kuwa pamoja na kusoma masomo hayo, lakini walionifundisha (yaani wahadhiri wangu) hawakuweka hamasa yoyote katika fikra zangu kuhusu ufanyaji ujasiriamali na uendeshaji wa miradi.


Hadi leo huwa nawahesabu kama watu wanaofundisha vitu ambavyo wao wenyewe vimewashinda! Ni bahati kuwa nilikuwa nikisoma masomo hayo huku nikiwa tayari nina nguvu na hamasiko binafsi moyoni mwangu, la kufanikiwa katika miradi na ujasiriamali. Hii ndiyo iliyokuwa salama yangu.


Ndiyo maana kila siku ninapojiuliza ni kwa nini tunazalisha wasomi wengi wenye vyeti katika maarifa ya biashara lakini hatuoni wakitumia elimu zao kuibua miradi, biashara na kutengeneza ajira; ninabaini kuwa tatizo lipo kwenye mifumo yetu ya kielimu.


Ni vigumu kwa daktari ama profesa wa biashara (ambaye hana hata banda la chipsi tu) kuzalisha mfanyabiashara halisi. Anachoweza kufanya ni kuzalisha wenye vyeti wengi wanaobaki kuwa mizigo mitaani. Kama ambavyo huwezi kujifunza kuogelea kwa kusoma maandishi, pia haiwezekani kujifunza biashara kwa kusoma vitabuni pekee.


Kama inavyotakiwa kuingia majini na kuanza kugusa maji, ndivyo ilivyo hata kwa biashara, lazima uingie na kuionja. Mkufunzi wa uogeleaji atafanikiwa kuzalisha waogeleaji wengi na walio mahiri kwa kuonesha kwa vitendo namna ya kuogelea (ikiwamo upigaji mikono na urushaji miguu ukiwa majini).


Mkufunzi akikaa ukingoni mwa bwawa na kuwasomea wanafunzi maandishi kisha kuwaamuru wajitose majini, anaweza asishuhudie hata mmoja anayejitosa. Lakini hata wakijitosa majini na wakapata tatizo la kuanza kuzama, huyu mkufunzi atawaokoaje wakati yeye mwenyewe hayajui maji?


Ndivyo ilivyo pia kwa wasomi wakufunzi wa mambo ya biashara na ujasiriamali. Hatuwezi kuzalisha wajasiriamali wa ‘ukweli’ ikiwa wanaowafundisha hawajawa mifano ya kuigwa (they are not role models). Hali hii tete inaibua tatizo jingine kubwa katika ujasiriamali wa Kitanzania pale zinapohitajika huduma za kitaalamu ikiwamo ushauri wa kibiashara.


Kiukweli, ushauri wa kitaalamu katika ujasiriamali na biashara unahitajika sana hasa katika nyakati hizi ambazo tunapambana na ushindani wa kimataifa. Unaposikia neno ‘ushauri’ pamoja na mantiki yake ni kwamba huwa una machaguo matatu. Unaweza kuukataa wote, unaweza kuutumia wote ama ukachukua kidogo na kuikataa sehemu fulani. Yote katika yote ushauri wa kibiashara tunatazamia unapotumika ulete tija ya uboreshaji wa biashara ama eneo uliloshauriwa.


Asilimia kubwa ya wafanyabiashara nchini Tanzania wanadhulumiwa kwa kutozwa kodi kubwa kuliko inavyostahili kutokana na ukosefu wa elimu katika eneo hilo. Kwa kukosekana mifumo ya utunzaji wa hesabu, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) huamua kukadiria viwango vya kodi bila kuzingatia faida inayokusanywa kwa mwaka.


Angalia mfano huu mdogo; unapokuwa na duka lako, kabla ya kulipa kodi unatakiwa kutoa mshahara wako (wewe mjasiriamali), mshahara wa wafanyakazi pamoja na gharama za uendeshaji. Baada ya hapo ndipo unatakiwa kulipa kodi kutoka katika kile kinachobaki.


Lakini ni wangapi wanaofanya hivyo? Bila shaka utagundua kuwa ni wachache mno. Habari njema ni kuwa huhitaji kuwa msomi ili kuendesha biashara zako kisomi, watumie wasomi wakusaidie kufikia malengo yako (lakini nakushauri utumie aina ya wasomi ninaowaamini – wale wanaoishi kwa vitendo maarifa yao).


Kwa mfano; kama wewe ni mfanyabiashara wa huduma za daladala, ama unakusudia kuanzisha biashara hiyo, ni vema ukamtafuta mfanyabiashara mzoefu katika eneo hilo la daladala akupe mbinu na mazingira halisi. Huyu kwako ninamhesabu ni mtaalamu wako. Itakuwa ni bahati tu inapotokea umeniomba ushauri wa kibiashara halafu ikawa kuwa biashara unazofanya ama kukusudia kufanya ni zile ambazo mimi pia  ninazifanya.


Maana yangu hapa ni kuwa, utaalamu katika biashara upo wa aina mbili. Kuna wale waliokaa darasani na kufundishwa biashara (bila kujali ikiwa wanafanya ama hawafanyi biashara), na wengine ni wale ambao licha ya kutoingia darasani, wana uzoefu mkubwa wa kibiashara. Hawa wote ni vema kuwatumia kwa kadiri ya mazingira na mahitaji yako kibiashara (japokuwa mimi huwa siwatumii hata kidogo wasomi wa biashara wanaozijua nadharia, lakini hawajawahi kuzitumia katika mazingira halisi ya kibiashara).


Unapotafuta mtaalamu wa kukushauri (ikiwa unataka msomi), mimi ninadhani ni vema kuwapata wataalamu ambao wana uzoefu wa kivitendo katika biashara mbalimbali. Najua hii ni changamoto kubwa kwa sababu wasomi wengi wa mambo ya biashara hawafanyi biashara, lakini kwa kuwa tunao wasomi wachache wa biashara wanaofanya biashara ni vema kuwatumia hao. Bila kuwa makini unaweza kupotezwa kwa sababu ‘wataalamu’ wengi hutumia muda mwingi kueleza namna mambo yasiyowezekana.


Hata hivyo, katika ufanyaji biashara, ni vema kuachana na mazoea ya kufanya biashara kienyeji, badala yake kuna umuhimu wa kuingiza utaalamu katika ujasiriamali wetu. Hii itasaidia sana kuratibu mafanikio yako na kuachana na hesabu za kubahatisha kwa kwenda kwa kupapasa.


Tunapaswa kuwatumia wataalamu washindi katika biashara zetu.


[email protected],  0766 74 24 14


By Jamhuri