Na Aziza Nangwa, JamhuriMedia, Dar es Salaam
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetangaza kuwa na msimu wa Kipupwe Juni hadi Agosti mwaka 2026 unatarajiwa kuwa na hali ya baridi katika maeneo mengi ya nchi, huku mwezi Julai ukitajwa kuwa na vipindi vya baridi kali zaidi.
Akizungumza na wanahabari leo Mei 25,2026 Jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkuu wa TMA, Dkt. Ladislaus Chang’a, amesema maeneo ya Kanda ya Ziwa Victoria, Kanda ya Magharibi, Kusini pamoja na Nyanda za Juu Kusini-Magharibi yanatarajiwa kuwa na hali ya baridi ya wastani hadi joto kiasi.
Amesema maeneo ya Ukanda wa Pwani ya Kaskazini na Kusini pamoja na Mkoa wa Dodoma yanatarajiwa kuwa na hali ya joto kiasi hadi baridi ya wastani, huku baadhi ya maeneo yenye miinuko yakitarajiwa kushuka hadi chini ya nyuzi joto 10 za sentigredi.
Dkt. Chang’a amesema msimu huo utatawaliwa na upepo kutoka Kusini Mashariki wenye nguvu iliyopungua kidogo, lakini kutakuwepo vipindi vya upepo mkali zaidi katika miezi ya Juni na Julai hususan kwenye maeneo ya Pwani ya Bahari ya Hindi na baadhi ya maeneo ya nchi kavu.
Katika kipindi cha mvua TMA imeeleza kuwa licha ya msimu wa Kipupwe kwa kawaida kuwa wa ukavu, baadhi ya maeneo yanatarajiwa kupata mvua za nje ya msimu, ikiwemo Kanda ya Ziwa Victoria hususan Mkoa wa Mara pamoja na mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Morogoro, Pwani, Lindi, Mtwara na visiwa vya Unguja na Pemba.
Hata hivyo ,TMA imeonya kuwa hali ya baridi na vumbi inaweza kuongeza magonjwa yanayohusiana na mfumo wa upumuaji kama mafua na homa ya mapafu, pamoja na magonjwa ya macho na yale yanayoathiri mifugo.
Kutokana na hali hiyo, mamlaka hiyo imezitaka jamii, wakulima, wafugaji pamoja na wadau wa sekta mbalimbali kuchukua tahadhari na kuendelea kufuatilia utabiri wa hali ya hewa pamoja na tahadhari zinazotolewa ili kuongeza usalama na ufanisi wa shughuli zao za kila siku.
TMA itaendelea kufuatilia mifumo ya Hali ya hewa na kutoa mrejesho hivyo watumiaji wa taarifa za utabiri huu wanashauriwa kufuatilia na kuzingatia utabiri wa saa 24 ,suku 19,mwezi pamojw na tahadahari za hali mbaya ya hewa.
Aidha amesema upande mwingine, joto la bahari katika eneo la kusini magharibi mwa bahari ya Hindi(kusini mwa kisiwa cha Madagascar) linatarajiwa kuwa la juu ya wastani.
‘’Hali hiyo inatarajiwa kudhoofisha mgandamizo mkubwa wa hewa katika eneo hilo na hivyo kupunguza kasi ya upepo wenye baridi kutoka kusini kuelekea katika maeneo ya nchi yetu.
Katika msimu huu, magonjwa yanayohusiana na hali ya baridi kama vile homa ya mapafu na magonjwa ya mifugo yanaweza kujitokeza.
Kwa upande wa mifugo amewashauri wafugaji ,kuendelea kuzingatia ratiba za kuogesha mifugo ili kudhibiti usumbufu na magonjwa pamoja na kufuata ushauri wa wataalamu.






