Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia,Dodoma

Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imeomba Bunge la Tanzania kuidhinisha bajeti ya jumla ya shilingi trilioni 2.443 kwa ajili ya matumizi yake katika mwaka wa fedha 2026/2027.

Bajeti hiyo imewasilishwa leo Mei 25, 2026 bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka ujao wa fedha.

Amesema kiasi hicho kinajumuisha shilingi trilioni 2, bilioni 443, milioni 215, laki tisa na ishirini na saba elfu (2,443,215,927,000) ambazo zitagharamia shughuli mbalimbali za wizara na taasisi zake.

Katika hatua nyingine, Waziri Katambi amesema wizara hiyo imejipanga kukusanya jumla ya shilingi bilioni 499.09 kutoka katika vyanzo mbalimbali vya mapato ndani ya mwaka huo wa fedha.

Amesema ili kufikia malengo hayo, wizara itaendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya kielektroniki sambamba na ununuzi wa vitendea kazi vya kisasa kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa utendaji kazi na utoaji huduma kwa wananchi.

Kwa mujibu wa ufafanuzi wa Waziri Katambi, shilingi trilioni 1.953 sawa na asilimia 80 ya bajeti yote zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida.

“Shilingi trilioni 1.183 ni kwa ajili ya mishahara huku shilingi bilioni 769.599 zikitengwa kwa matumizi mengineyo,” amesema Waziri Katambi.

Aidha, amesema shilingi bilioni 489.849 sawa na asilimia 20 ya bajeti hiyo zimetengwa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Amefafanua kuwa kati ya fedha za maendeleo, shilingi bilioni 453.955 ni fedha za ndani huku shilingi bilioni 35.893 zikiwa ni fedha za nje.

Waziri Katambi amesema wizara itaendelea kuimarisha usalama wa nchi, kuboresha huduma kwa wananchi pamoja na kuongeza matumizi ya teknolojia katika utekelezaji wa majukumu yake mbalimbali.