Na Dotto Kwilasa, JamhuriMedia, Dodoma
Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi imetolea ufafanuzi kuhusu picha iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ikimuonesha mfungwa akiwa amevaa hereni gerezani, ikielezwa kuwa picha hiyo ilitumiwa kwa namna ya kupotosha umma na kuibua tafsiri zisizo sahihi kuhusu uhalisia wa tukio hilo.
Akihitimisha mjadala wa bajeti ya Wizara hiyo bungeni jijini Dodoma leo Mei 25, 2026, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Patrobas Katambi amesema tukio hilo ni mfano wa matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii yanayolenga kuaminisha wananchi taarifa zisizo na ukweli.
Katambi amesema Serikali haitaruhusu teknolojia kutumiwa kama chanzo cha madhila, uchochezi na uvunjifu wa amani, akisisitiza kuwa hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaobainika kusambaza taarifa za uongo au zinazodhalilisha watu.
Amesema sheria zilizopo ikiwemo ya Huduma za Habari pamoja na kanuni ya adhabu zinazuia vitendo vya kutweza utu wa mtu, kusambaza taarifa za uongo na kudhalilisha wananchi kupitia mitandao ya kijamii au vyombo vya habari.
“Wapo watu wamejaribu kutweza utu na heshima za watu, wapo ambao wamewadhalilisha kwa kuwavumishia na kuwazushia mambo ya uongo na wapo pia waliotoa taarifa za uongo, uzushi na uchochezi,” amesema Katambi.
Waziri huyo amebainisha kuwa picha hiyo ya mfungwa ilitumika kama mfano wa jinsi baadhi ya watu wanavyoweza kutengeneza au kusambaza maudhui yenye lengo la kupotosha umma, ikiwemo kuibua mashaka yasiyo na msingi kuhusu taasisi na viongozi wa nchi, wakiwemo viongozi wakuu kama Rais Samia Suluhu Hassan.
Aidha, Katambi amesema Wizara ya Mambo ya Ndani tayari imeanza kushirikiana na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Wizara ya Teknolojia ili kuweka mikakati ya pamoja ya kudhibiti matumizi mabaya ya majukwaa ya kidijitali.
Amesisitiza kuwa Serikali haitasita kuchukua hatua kali kwa mtu yeyote atakayebainika kutumia mitandao ya kijamii au vyombo vya habari kusambaza chuki, uzushi, taarifa za uongo au maudhui yanayoweza kuhatarisha amani na mshikamano wa Taifa.


