DAR ES SALAAM

Na Mwl. Paulo Mapunda 

Naomba nitamke mapema kwamba mimi ni Mkristo mwenye mizizi katika Ukatoliki na baadaye wokovu, nimezaliwa na kukulia ndani ya Ukatoliki, hata ndoa yangu nilifunga Parokia ya Manzese.

Elimu yangu nimeipata katika shule zenye nasaba na Ukatoliki. Nitamke kwamba kwa muda mrefu sana dunia imekuwa na itaendelea kutawaliwa na Ukatoliki (Universal Church) hasa kutokana na sababu za kihistoria (The Ancient Rome Empire), na misingi ambayo kanisa hili limejengwa.

Kwamba mipango yote ya uendeshaji wa dunia hii inapangwa, kusukwa na kuratibiwa kutoka Vatican, hata niliposikia kwamba Rais SSH anakutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu wa Katoliki (Tanzania Episcopal Conference – TEC), nikahisi kuna jambo haliko sawa au kuna makubaliano fulani fulani yanakwenda kuingiwa baina yake na wazee hawa.

Kanisa Katoliki limejijenga kwa miaka mingi, falsafa yake ya viongozi wa kanisa kuwa na elimu ya kutosha (Mith. 4:13) kukidhi vigezo vya kiuongozi, imesababisha kanisa kuwa imara na kamwe hakuna uongozi unaoweza kujitenga na ushawishi wa kanisa hilo tena.

Kanuni za kiuchumi za kanisa hilo ndizo ziongozazo uchumi wa dunia leo hii, hata mbinu za kijeshi na kiutamaduni (mfumo maisha) ni za Kikatoliki zenye asili ya Dola ya Kirumi. Uwekezaji wa kanisa hili ni mkubwa sana kwenye maisha ya watu duniani kote.

Mwandishi wa kitabu kiitwacho ‘Past to Present World History’, Profesa (wa historia) Zabel, H.M, anasema hivi katika ukurasa wa 193): “…of all the institutions which have shaped medieval society by far the most influential, was the Roman Catholic Church.

“Nearly all the inhabitants of Western Europe lived and died within its fold. The church also played an important part in the government and education, so completely did it dominate people’s lives that the middle ages are often the age of faith.”

Katika ukurasa wa 244, mwandishi anaandika: “Kwa zaidi ya miaka 1,000, Kanisa Katoliki lilikuwa ndio mhimili wa imani ya Wakristo wote wa nchi za Magharibi, lilihimili tamaduni, siasa na uchumi wa zama za kati.”

Mwaka 1961, nchi yetu ilijipatia uhuru kutoka kwa Waingereza, na Mkatoliki, Mwalimu J ulius Nyerere akawa Rais wa Kwanza wa Tanganyika huru na baadaye Tanzania (baada ya Muungano wa mwaka 1964).

Tangu wakati huo hadi leo, mwaka 2021, Wakatoliki watatu wameliongoza taifa hili. Mwalimu Nyerere (1961-1985), Mwandishi Benjamin Mkapa (1995-2005) na Mwalimu wa Hesabu na Kemia, Dk. John Magufuli (2015-2021). Wote watatu ni marehemu. Sababu hasa ya vifo vyao ni nini?

Je, ni kile kilichopata kutamkwa katika mihadhara ya kidini katikati ya miaka ya 1990 kwamba Mwalimu Nyerere alisaini makubaliano (MoU) na Wazungu kulipa uelekeo fulani wa kiimani taifa hili, hivyo kuwasaliti wazee waliopigania uhuru wa nchi hii kwa hali na mali dhidi ya mkoloni; hali iliyosababisha wazee hao kutamka ‘neno’ linalowatafuna viongozi wa imani hiyo hadi leo?

Au sababu hasa ya vifo vyao nini? Tutafakari na kujiuliza pamoja tupate majibu.

Mungu ndiye mwenye mamlaka juu ya hatima ya uhai wa kiumbe chochote kwani yeye ndiye muumbaji, lakini inapotokea watu wa kariba fulani (ukoo, kabila, dini, rangi au eneo) ndio wanaokufa tu, akili ya kawaida inatusukuma kuhoji chanzo cha vifo vyao.

Mamlaka zinazohusika zilipata kutufahamisha kwamba wazee wetu hao walikuwa wagonjwa wakisumbuliwa na maradhi mbalimbali. 

Swali la kujiuliza ni hili; Je, ni wao tu wenye nasaba na imani kongwe ndio washambuliwao na maradhi hayo? 

Kwa nini uhai wao tu ndio Mungu anaupenda zaidi, kwa nini mapenzi yake yanatimia kwa kuutwaa uhai wa wazee wa imani hii tu, kuna siri gani tupaswayo kuitengua ili nao wapate kuishi na kufikia au kupita umri wa mzee Ruksa? (Mungu amuongezee miaka mingi; Amina).

Tawala za viongozi wenye asili ya Ukatoliki nchini, zina sifa moja kuu, nayo ni ‘ukapa’ hasa kutokana na sera zao za kifedha, yaani sera za ‘kimbinyo’ (Contractionary Monetary Policy – CMP) yenye mizizi kutoka sera ya kifedha ya kikardinali (Cardinalist Approach).

Sera hii ina tabia ya kuakisi sifa halisi ya fedha (scarceness or scarcity) ambayo huzalisha manung’uniko miongoni mwa watu, hasa kutokana na uhaba wa fedha katika mzunguko wa kiuchumi.

Kulithibitisha hili, angalia maneno yaliyowahi kutamkwa, kwanza, kwa walioishi nyakati za Mwalimu Nyerere, watakubaliana nami kuwa hali ya maisha ilikuwa ngumu sana! Sabuni, sukari, unga, dagaa vilipatikana kwa kupanga foleni.

Halikadhalika, wakati wa Mkapa hali ilikuwa ngumu hadi mfumo wa maisha ukaitwa ‘Ukapa’. Hali hiyo ilijirudia tena nyakati za Magufuli, na watu wakamueleza waziwazi kuwa ‘vyuma vimekaza mzee!’

Hali ni tofauti Kiongozi Mkuu akiwa ni Muislamu, nyuso za Watanzania hukunjuka, ishara ya matumaini ya kuishi hurejea mioyoni mwao. 

Mathalani, nyakati za mzee Mwinyi hali ilikuwa nzuri, fedha zilipatikana, wananchi wakawa na uwezo wa kununua.

Mzee Mwinyi alibatizwa jina la ‘Mzee Ruksa’ kutokana na kuruhusu watu kumiliki mali, kuleta bidhaa ndani ya nchi na kusafirisha nje. Katika nyakati za utawala wa mzee huyu, watu wamekula na kunywa huku wakimshukuru Mungu.

Halikadhalika, sifa hizi zilitamalaki katika nyakati za utawala wa Jakaya Kikwete. Wenye kujenga wamejenga, wenye kuoa na kuolewa walilitenda jambo hilo kwa ufanisi mkubwa. 

Jakaya aliwakilisha tabasamu halisi la Watanzania wote, kama vile yeye alivyokuwa akibembea kule Jamaica, nasi tulimudu kwenda kubembea Dege Beach, Coco Beach, Wet ‘n Wild na kwingineko ndani na nje ya nchi. 

Wananchi tulifurahi. Ni Rais wetu. Mungu akupe maisha marefu Dk. Jakaya Khalfan Mrisho Kikwete, bado tunazikumbuka fadhili zako.

Leo hii yupo mama Ikulu. Tafadhali turudishie furaha ile tuliyoipoteza tangu mwaka 2015, kwa muda mfupi mioyo ya Watanzania imekunjuka, sura zao zinaonyesha nuru na matumaini ya kuishi.

Nilipoona walimu tunapandishwa madaraja, watumishi wengine mishahara juu, nikajisemea moyoni; muungwana kaingia Ikulu.

Waliousoma, kuuelewa na kuuishi Uislamu ni waungwana. Hawahitaji dhuluma, uonevu, ukandamizaji wala ubambikiziaji riba, kodi na kesi ili kuchuma wasipopanda (falsafa ya talanta tano).

Niwaombe Wakristo wenzangu tujifunze kanuni hizi za kuishi kwa msingi wa Mathayo 7:12, tusiutukuze ufarisayo wa kina Kayafa na Anasi ili kuminya haki na kuzuia ustawi wa watu.

Ayubu anasema, mimi nilitoka tumboni mwa mama yangu nili uchi kama nitakavyokwenda (Ayubu 1:21). Kuna sababu gani ya kutengana tuwapo hapa duniani? Kuna sababu gani za msingi kuwafanya watu wajione wakimbizi ndani ya nchi waliyopewa na Muumba wao?

Kwa nini watu wakeshe wakimlilia Mungu wao kwa sababu ya aina ya utawala waliouweka wao wenyewe? Kiongozi Mkuu wa nchi ndiye mfariji mkuu wa watu wake, wanapohuzunika,  ahuzunike nao, wanapofurahi, afurahi pamoja nao, kamwe usiwazodoe kwa magumu wapitiayo. Hapana.

Bali Mama, waambie ‘kazi ziendelee’ au waambie ‘ruksa’. Siku zote wape matumaini watu wako ili wapate faraja na kujiona kuwa wako salama katika nchi yao na kwamba Mungu hakukosea kuwapa nchi hii.

Mama Rais SSH, Sisi wananchi wako tunamshukuru Mungu kwa kutupatia wewe, tunajua kila jambo na wakati wake, na lipo kusudi kwa kila litokealo chini ya mbingu (Mhubiri 3:1-8), tunakuahidi kuchapa kazi kwa ari, nguvu na kasi mpya.

Tunapomuomba Mungu akupe maisha marefu na mafanikio katika utawala wako, vilevile tunamuomba usije ukabadilika, upendo wako kwetu ubaki kuwa wa mshumaa. Nikuombe mambo machache ili Mungu aweze kulibariki taifa letu.

Mosi, tafakuri jadidi ya kitaifa inahitajika kuhusiana na chanjo ya UVIKO-2021, malengo ya maradhi ya virusi yanafahamika kwamba ni kupunguza idadi ya watu duniani ili kuingia kwenye Mfumo Mpya wa Dunia (New World Order) tofauti na mpango wa Mungu (Mwz.1:28).

Kuruhusu chanjo ni kuhalalisha mpango wa kishetani wa uharibifu. Ujumbe unaosambaa kwenye mitandao ya kijamii, kama ni kweli umetoka kwa Melinda Gates, basi tunakila sababu ya kuwa na shaka na chanjo hii.

Maelezo na ufafanuzi wa Askofu Gwajima bungeni vinatosha kutufikisha katika hitimisho hilo, hatuhitaji kushawishiana kwa maneno mazuri kuwa ni hiari ilhali siku si nyingi itakuwa ni lazima kuchanjwa uweze kupata huduma katika taasisi fulani. (Vaccine marks the beginning of unscrupulous days).

Pili, kumbukumbu zinaonyesha Kiongozi Mkuu wa nchi akiwa ni Muislamu, kunaibuka vikundi vinavyoendesha mihadhara yenye maudhui ya kidini, hususan Ukristo na Uislamu.

Imetokea hivyo kwa mzee Mwinyi na mzee Kikwete. Tafadhali, hilo lisitokee kwako Mama. Madhira ya mihadhara ni mengi na makubwa, sihitaji kuyaorodhesha hapa, bali itoshe kukumbusha kile kilichotokea Mwembechai miaka 1990 kiwe fundisho kwa kizazi hiki na kijacho.

Tatu, kwa muda wa siku 100 na ushei ulizokaa Ikulu kama raia namba moja, tunaweza kuripoti kwamba Mahakama inatenda haki.

Nne, ndani ya siku 100 za Rais SSH, tunaweza kuripoti kwamba ‘watu wasiojulikana’ hawajulikani walikokwenda. Iliwezekanaje nchi yenye mfumo imara wa ulinzi na usalama kuwa na watu wa aina hii?

Mungu ibariki Tanzania na watu wake. Haki itainua taifa (Mithali 14:34).

 [email protected]

 0755 671 071

By Jamhuri