DAR ES SALAAM

Na Mwalimu Samson Sombi

Kijiografia Afrika Mashariki inaundwa na nchi tatu; Tanzania, Kenya na Uganda. Tanzania na Kenya zinapakana na Bahari ya Hindi kwa upande wa mashariki. Nchi hizi tatu zimeunganishwa na Ziwa Victoria.

Baada ya nchi hizo kupata uhuru, Tanzania ikiwa ya kwanza mwaka 1961, Uganda ya pili mwaka 1962 na Kenya mwaka 1963, ziliamua kuanzisha ushirikiano.

Ushirikiano huo chini ya uongozi wa marais Mwalimu Julius Nyerere wa Tanzania, Jomo Kenyatta (Kenya) na Militon Obote (Uganda), ulilenga maeneo kama mamlaka ya huduma za pamoja, ushirikiano wa fedha (East African Shilling), forodha na huduma nyingine za usafiri wa ardhini, angani na majini.

Ushirikiano huo ulianza kutetereka mwaka 1965 pale kila nchi mwanachama ilipoanzisha fedha yake. Hata hivyo, mwaka 1967 nchi hizo zilianza kuunda upya ushirikano na kuimarisha umoja ambao ulipewa jina la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Makao Makuu yake Arusha.

Pamoja na mambo mengine, umoja huo ulilenga zaidi ushirikiano katika nyanja za kisiasa na uchumi, huku mifumo ya kisiasa ya nchi hizi ikitofautiana ambapo Kenya ilifuata siasa ya kibepari, Tanzania ujamaa na Uganda ‘udikteta’.

Kama hiyo haitoshi, katika uchumi, Kenya ilionekana kuwa imara zaidi ikilinganishwa na Tanzania na Uganda.

Tofauti hizi za kiitikadi na kiuchumi zilianza kujitokeza na kuleta mgogoro wa kimasilahi ulioanza kudhoofisha umoja. Kenya ilianza kudai na kutaka viti zaidi kuliko Tanzania na Uganda katika kamati za uamuzi.

Pamoja na vikao vya mara kwa mara vya usuluhishi, mgogoro huo ulisababisha kuanguka kwa jumuiya mwaka 1977 na kufutwa rasmi mwaka 1983.

Baada ya hapo kukawa na jitihada za kuifufua zilizopata msukumo zaidi mwaka 1993 na hatimaye Januari 2001, EAC ilifufuliwa na marais Benjamin Mkapa (Tanzania), Daniel Moi (Kenya) na Yoweri Museveni wa Uganda.

Pamoja na mambo mengine, mwanachama wa EAC anapaswa kutimiza vigezo vya utawala bora, demokrasia ya kweli na uongozi unaofuata na kuzingatia sheria.

Mambo mengine ni usawa wa kisheria wa kijamii, haki za binadamu, kama ilivyoainishwa katika nyaraka mbalimbali.

Tangu kuanzishwa upya kwa jumuiya hiyo, wanachama wapya wamekuwa wakiongezeka kadiri miaka inavyosonga mbele.

Rwanda na Burundi zilijiunga EAC mwaka 2017; taifa changa kabisa Afrika, Sudan Kusini, ikajiunga baada ya kutuma maombi na kujadiliwa kwa kina na vikao vya juu vya uamuzi na kufanya kuwa na jumla ya wanachama sita.

Pamoja na mafanikio mbalimbali ya kiuchumi na biashara miongoni mwa nchi wanachama wa jumuiya, pia kumekuwa na changamoto za kisheria na kisiasa.

Wakati EAC ikiendelea kuongeza wanachama, kumekuwa pia na mtazamo tofauti katika maendeleo ya kiuchumi miongoni mwa nchi wanachama.

Mfano, katika uchumi, Rwanda na Kenya wamesaini makubaliano ya ushirikiano wa kiuchumi (EPA) na Umoja wa Ulaya, wakati Tanzania na Uganda walijitoa wakitaja sababu kuwa ni kuzingatia masilahi ya mataifa yao. 

Kumekuwa pia na changamoto ndogo za kibiashara kati ya Tanzania na Kenya zinazotatuliwa mara kwa mara na viongozi wa pande mbili.

Desemba 2, 2018 katika uzinduzi wa Kituo cha Pamoja cha Forodha mpakani mwa Tanzania na Kenya kilichopo Namanga, Rais John Magufuli aliwaambia wananchi wa pande zote mbili kuwa mataifa haya ni ndugu na wanapaswa kupendana na kushirikiana.

Siku za hivi karibuni kumetokea mgogoro eneo hilo baada ya wafanyabiashara wa Tanzania kuzuiwa kuingia Kenya kwa sababu mbalimbali, ikiwamo ugonjwa wa corona, kisha mgogoro ukatatuliwa baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kufanya ziara Kenya mwanzoni mwa Mei mwaka huu.

Kumekuwa pia na misimamo tofauti miongoni mwa nchi wanachama wa EAC juu ya masuala ya kimataifa katika vyombo vya utetezi wa haki, ambapo Burundi imejitoa katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai (ICC).

Rais Museveni ni mkosoaji mkubwa wa mahakama hiyo, lakini Tanzania imesema haina mpango wa kujitoa huku Rwanda ikionyesha msimamo wake wa kutokuwa kabisa sehemu ya makubaliano ya Rome yaliyounda ICC.

Miaka ya karibuni kumekuwa na mgogoro kati ya Uganda, Rwanda na DRC, kila mmoja akimtuhumu mwenzake kusababisha chokochoko za kisiasa.

Hali hiyo imesababisha ombi la DRC kutaka kujiunga na EAC kuwekewa pingamizi na baadhi ya raia wa Uganda.

Kama ilivyokuwa kwa wanachama wengine wapya, DRC ilituma maombi kujiunga na jumuiya hiyo, na kama wakikubalika EAC itakuwa na nchi saba wanachama.

Ombi la DRC limewekewa pingamizi na wakili wa Mahakama Kuu ya Uganda, Adam Kyomuhendo.

Wakili huyo maarufu anadai DRC imevunja haki za binadamu kwa kumshikilia mwanaharakati kutoka Uganda, William Mugunya na wenzake zaidi ya 35.

Inaelezwa kuwa raia hao wa Uganda wameshikiliwa DRC kwa zaidi ya miaka sita sasa kinyume cha haki za binadamu; moja ya vigezo vya nchi kuomba uanachama.

Pingamizi hilo ambalo limepelekwa Mahakama Kuu ya Afrika Mashariki, limesimamisha mchakato ambao uamuzi wake ungefanyika Juni 23 hadi Julai 3 mwaka huu.

Februari mwaka huu, wakuu wa nchi wanachama wa EAC walikutana katika mkutano uliofanyika Tanzania kutoa maelekezo kwamba kesi hiyo ipelekwe pia katika Kamati ya Sekretarieti kutolewa uamuzi Novemba.

Wakati hilo likijitokeza, hali ya kisiasa Uganda bado haijatengemaa kutokana na marekebisho ya Katiba yaliyopitishwa na Bunge Desemba 20, 2017 ya kuondoa ukomo wa umri wa Rais uliokuwa umebainishwa katika Ibara ya 102(b) ya katiba.

Pamoja na ukweli kwamba umoja huo ulilenga ushirikiano zaidi kisiasa na kiuchumi, bado kuna tofauti kubwa katika kuheshimu misingi ya demokrasia katika baadhi ya nchi wanachama.

Katika kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo, imependekezwa kuundwa Katiba ya Shirikisho la Siasa ya EAC na kupata maoni ya kada zote kutoka nchi wanachama. 

Timu ya wataalamu ya Afrika Mashariki inayokusanya maoni kuhusu kuanzishwa shirikisho la kisiasa itatembelea Tanzania mwezi ujao.

Timu hiyo ya Rasimu ya Katiba ya Fungamano la Kisiasa la Afrika Mashariki iko kwenye mchakato wa kukusanya maoni katika nchi sita wanachama.

Mambo mengine ni kuanzishwa kwa soko kwa ajili ya bidhaa, huduma, ajira na mji mkuu wa Afrika Mashariki, lengo ni kuwa na fedha moja na shirikisho kamili.

Timu hiyo iliundwa Desemba 2018 kwa makubaliano ya kuunda kamati ya kuandika katiba ya Shirikisho la Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa taarifa, kamati hiyo ilikutana Januari 14 – 18 mwaka 2020 nchini Burundi na ilitangaza kuwa Katiba ya Muungano itaandaliwa mwisho wa mwaka huu kisha shirikisho kuanzishwa mwaka 2023.

Mwaka huu, Waziri wa Mambo ya Nje, Balozi Liberata Mulamula, amesema timu hiyo itatembelea nchini kama hatua ya mpito kuelekea Shirikisho la Kisiasa la Afrika Mashariki.

Katika hatua nyingine, Balozi Mulamula ameitaka EAC kujiimarisha zaidi katika diplomasia ya uchumi ili kuyafikia masoko ya kimataifa.

Pamoja na malengo na masharti ya jumuiya hiyo kuonekana bado ni changamoto kubwa kwa baadhi ya nchi wanachama na wanachama wapya, EAC chini ya uenyekiti wa Rais Paul Kagame, bado ina safari ndefu kufikia malengo yake huku viongozi wakipaswa kutanguliza masilahi mapana ya umoja huo.

0755-985966

476 Total Views 4 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!