DAR ES SALAAM

Na Mwalimu Samson Sombi

Tangu kurejea kwa mfumo wa vyama vingi nchini Julai 1992 na kufanyika Uchaguzi Mkuu wa kwanza chini ya mfumo huo mwaka 1995, kumekuwa na wimbi la wanasiasa kuhama chama kimoja na kujiunga na kingine, na baadhi kurudi katika vyama vyao vya awali kufuatana na upepo wa kisiasa.

Kadiri miaka inavyosonga, idadi ya vyama vya siasa vyenye usajili rasmi inaongezeka huku mwamko wa kisiasa ukishika kasi tofauti na awali.

Wanachama na wananchi wamekuwa makini katika kufuatilia mienendo ya wanasiasa na sera za vyama vyao. Aidha, mitandao ya kijamii imekuwa na mchango mkubwa katika masuala mbalimbali ya kijamii ikiwamo ya kisiasa.

Tofauti na miaka ya nyuma ambapo masuala yahusuyo siasa na wanasiasa yalijadiliwa zaidi wakati wa kampeni za uchaguzi, wagombea walinadi sera za vyama vyao majukwaani na kutoa nafasi kwa wananchi (wapiga kura) kufanya uamuzi kupitia masanduku ya kura.

Duniani kote vyama vya siasa hushindana kwa sera zinazoelezwa na wagombea ambao hupimwa kwa namna wanavyoweza kusimamia utekelezaji wa sera hizo. 

Chama kuwa na sera ni kitu kimoja, utekelezaji wa sera hizo ni hatua ya na muhimu sana kwa mustakabali wa taifa na wananchi.

Katika mfumo wa vyama vingi vya siasa wanasiasa, hasa wenye malengo ya kuwania nafasi za uongozi ikiwamo ubunge na urais, huchunguza kwa umakini mkubwa upepo wa kisiasa. 

Wanapogundua kuwa upepo huo hauko upande wa vyama vyao, hufanya uamuzi mgumu wa kuvihama vyama vyao na kujiunga na vile ambavyo upepo kwa wakati huo huvuma kuelekea upande wao.

Na mara mambo yanapokwenda kombo, baadhi hurudi nyumbani kuendelea na harakati za kutimiza ndoto au malengo yao mengine katika uwanja wa siasa.

Kama inavyotokea katika uchaguzi mbalimbali tangu kuingia kwa mfumo huu, Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana baadhi ya wanasiasa waliamua kuvihama vyama vyao na kwenda kutafuta nafasi za uongozi katika vyama vingine, bila kujali masilahi mapana ya vyama vyao.

Tofauti na vyama vingine, wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) hawapaswi kuonyesha nia ya kugombea na kuanza harakati hizo kabla ya muda uliowekwa.

Wanaobainika kuvunja kanuni hiyo kuchukuliwa hatua kali za kinidhamu na wengine kufukuzwa uanachama pale ambapo vikao vya chama vinaporidhia mwanachama huyo kuvuliwa uanachama na zaidi huwa hakuna nafasi ya kukata rufaa.

Mmoja wa makada waliokumbwa na sekeseke hilo ni aliyewahi kuwa Waziri wa Mambo ya Nje, Bernard Membe. 

Kada huyo ni miongoni mwa wanachama waliotuhumiwa kufanya kampeni mapema kuelekea Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015.

Katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, Membe aliingia ‘tano bora’ ndani ya CCM lakini hakufanikiwa kupenya hatua ya ‘tatu bora’, hivyo ndoto zake za urais kuanza kufifia.

Katika hatua nyingine, kada huyo mkongwe alikabiliwa na makosa mbalimbali ya kimaadili yaliyosababisha kuitwa mbele ya vikao vya juu vya chama, ikiwamo Kamati ya Maadili, ikiwa ni utaratibu wa kupewa nafasi ya kujitetea inapotokea malalamiko juu ya mwenendo wa mwanachama.

Licha ya Membe kuhojiwa na kupewa nafasi ya kusikilizwa Februari 28, 2020, CCM ilimvua uanachama baada ya kutoridhishwa na mwenendo wake.

Pamoja na kuvuliwa uanachama, Membe hakukata tamaa katika harakati za kutimiza ndoto zake kisiasa. 

Badala yake aliamua ujiunga na ACT- Wazalendo, baadaye akateuliwa kupeperusha bendera ya chana hicho kuwania nafasi ya urais.

Julai 2020, Membe alijiunga na ACT-Wazalendo na kupewa nafasi ya mshauri wa chama kutokana na uzoefu wake mkubwa katika siasa za ndani na nje ya nchi. 

Mbunge huyo wa zamani wa Mtama alionekana kuwa na ushawishi mkubwa wa kisiasa ndani ya chama hicho, hivyo akapewa jukumu zito la kukipigania chama hicho kushika dola.

Akizungumza wakati wa hafla ya kukabidhiwa Ilani ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2020 ya ACT-Wazalendo jijini Dar es Salaam, Membe anasema kila mwanachama makini wa CCM anafahamu  ukweli uliomo ndani ya chama hicho kikongwe Afrika.

“Hata nyinyi mnafahamu kwamba ndani yake kuna CCM wapya na CCM ‘waliotumbuliwa’ na kukatwa. Walipotaka kuja huku ACT- Wazalendo, wakakatazwa,” anasema Membe.

Anasema ingawa amejiunga na ACT-Wazalendo Julai (2020), amekuwa akiwasiliana na Kiongozi Mkuu wa chama hicho tangu Februari, wakibadilishana mawazo na kutafuta namna sahihi ya kumkomboa Mtanzania.

Kwamba hata ndani ya Ilani ya ACT amechangia mambo kadhaa, hasa katika sekta anayoifahamuu vema; ya diplomasia ya kimataifa.

“Ni Ilani bora kuliko zote. Nimekuwa kwenye siasa kwa miaka 38 sasa. Nimesoma ilani za vyama vyote. Lakini hii inatekelezeka na itamkomboa Mtanzania,” anaeleza Membe huku akishangiliwa na wafuasi wa chama hicho.

Katika matokeo ya Uchaguzi Mkuu huo, Membe alipata kura 81,129 sawa na asilimia 0.55, akitimuliwa vumbi na mgombea wa CCM, Dk. John Magufuli, aliyepata kura 12,516,252 sawa na asilimia 84.40.

Magufuli alifuatiwa na mgombea wa Chadema, Tundu Lissu, aliyepata kura 1,933,271 sawa na asilimia 13.04.

Safari ya Membe ndani ya ACT-Wazalendo ilikamilika Januari mwaka huu alipotangaza kujitoa bila kuweka wazi chama ambacho alitarajia kujiunga.

Jumanne ya Oktoba 5, mwaka huu akiwa mkoani Lindi, Membe alisema anamuunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan na yupo tayari kumpigia kampeni katika Uchaguzi Mkuu mwaka 2025.

“Niwaombe tusahau yaliyopita, tuanze upya, tujenge taifa letu. Niko tayari kuwa kampeni meneja wa Rais katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025,” anasema.

Katika ziara hiyo ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Membe anasema wakati wote yuko tayari yeye na wananchi wa Lindi kumpa ushirikiano Rais Samia na serikali yake kwa kuwa ameonyesha dhamira ya kuirudisha nchi  kwenye misingi ya umoja, mshikamano na uhusiano wa kitaifa na kimataifa.

Samia aliapishwa kuwa Rais wa Sita wa Tanzania, Machi 19 mwaka huu, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri, inayosema: “Endapo kiti cha Rais kitakuwa wazi kutokana na Rais kufariki  dunia, kujiuzulu, kupoteza sifa za uongozi au kutomudu kazi zake kutokana na maradhi ya mwili na kushindwa kutekeleza kazi na shughuli za Rais, basi Makamu wa Rais ataapishwa na atakuwa Rais kwa muda uliobaki katika kipindi cha miaka mitano na kwa masharti yaliyoelezwa katika ibara ya 40 ya Katiba.”

Rais Samia amechukua nafasi ya mtangulizi wake, Rais Magufuli, aliyefariki dunia Machi 17, mwaka huu kutokana na maradhi ya moyo.

Siku za hivi karibuni kumekuwa na uvumi juu ya Rais Samia kugombea au kutokugombea nafasi  hiyo ya juu mwaka 2025,  hatua  ambayo ilimfanya Rais kutoa msimamo wake juu ya gumzo hilo.

Jamatano ya Septemba 15, mwaka huu jijini Dar es Salaam, Rais Samia amesema hadi sasa bado Tanzania haijafanikiwa kumpata Rais mwanamke anayetokana na Uchaguzi Mkuu kwa kuwa aliyepo madarakani amepatikana kwa kudra za Mungu na matakwa ya kikatiba.

Mbali na kauli hiyo, ametoa wito kwa wanawake na Watanzania kusukuma ajenda ya kumsaka Rais mwanamke atakayetokana na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

“Rais mwanamke tutamweka mwaka 2025. Wanawake oyee!” anasema Rais Samia na kuibua shangwe kwa wanawake waliofurika katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, Dar es Salaam.

“Ndugu zangu, mwaka 2025 tukifanya vizuri tutaweka Rais mwanamke. Tutakutana hapa tufurahi. Wameanza kutuchokoza, kuandika kwenye vigazeti kwamba Samia hana nia. Nani kawaambia? Fadhila za Mungu zikija mkononi, uzisiachie,” anasema Rais.

Mbali na Membe, aliyekuwa Waziri Mkuu katika Awamu ya Nne, Edward Lowassa, aliondoka CCM na kujiunga na Chadema Julai 28, 2015 na baadaye kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho.

Lowassa ambaye alipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.7, alirejea CCM Machi 1, 2019 na kusema amerudi nyumbani.

Machi 10 akiwa Monduli, Lowassa alisema amerudi nyumbani na asiulizwe amerudi kufanya nini, huku akiwashukuru Chadema kwa mapokezi na ushirikiano waliompa wakati wote akiwa huko.

Kuhusu uongozi wa Rais Samia, Lowassa amesema:

“Rais Samia amethibitisha pasipo shaka kwamba Tanzania imepata nyota ya jaha kwa kuwa na Kiongozi Mkuu mwanamke hodari na shupavu ambaye leo hii tuna kila sababu ya kujivunia na kumuunga mkono.”

Mwaka 2015 wanachama na viongozi wengi wa CCM walihamia upinzani na miaka mitatu  baadaye, wanachama hao na wale wa upinzani waliaanza kurejea CCM, wakidai kuvutiwa na utendaji kazi wa Rais Magufuli.  

Rais Samia amekuja na kaulimbiu ‘Kazi Iendelee’. Hamahama hiyo itaendelea? Muda utazungumza.

0755985966

284 Total Views 2 Views Today
||||| 0 I Like It! |||||
Sambaza!