*Rais Samia avunja usiri wa mikopo serikalini

*Aanika kiasi ilichokopa serikali, matumizi yake

*Wingi wa miradi kuchemsha nchi miezi 9 ijayo

*PM asema ‘kaupiga mwingi’ 2025 – 2030 mtelezo

DODOMA

Na Mwandishi Wetu

Rais Samia Suluhu Hassan ameweka mwelekeo mpya wa kiutendaji serikalini, hasa eneo la utekelezaji wa miradi, kwa kutoa maagizo mahususi yenye kukata mnyororo wa urasimu, huku serikali yake ikijenga miradi mingi na mikubwa ndani ya miezi sita ya uongozi wake.

Amesema Tanzania imekopa mkopo wa dharura wa dola bilioni 567 sawa na Sh trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF), fedha ambazo Rais Samia ameamua badala ya kuzitumia kununua chanjo, zijenge miundombinu ya sekta mtambuka, ikiwamo maji, elimu, utalii, maliasili na kuboresha sekta ya afya kwa lengo la kurahisisha matibabu kwa wananchi wa maeneo ya vijijini. Hii ndiyo njia sahihi ya kupambana na Uviko – 19 kwa mfumo endelevu.

Katika kufanikisha mipango hii mikubwa ya kihistoria, amebaini Kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko – 19 aliyoizindua jijini Dodoma juzi inayopaswa kutekelezwa kwa miezi tisa, haitakuwa na ufanisi iwapo itatekelezwa kwa utaratibu wa mazoea.

Kutokana na hilo, ameiagiza Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) kutoa vibali vya utekelezaji wa miradi chini ya utaribu wa kupata mzabuni mwenye uwezo wa kutekeleza mradi (single sourcing) badala ya kuitisha zabuni ikachukua miezi mitatu na zaidi kukamilisha mchakato.

Ametoa onyo kali kwa watendaji serikalini na wazabuni watakaojaribu kutafuna fedha hizo za utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kukabiliana na janga la ugonjwa wa corona (Covid-19).

 Miradi hiyo yenye thamani ya Sh trilioni 1.3 zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF) kama mkopo wa masharti nafuu itahusisha sekta ya elimu, afya, maji, maliasili na utalii.

“Kama mnataka kuona rangi zangu halisi, maana mnasema mama ni mweupe! Sasa watumishi au wazabuni wajaribu kudokoa fedha hizi au wabadilishe matumizi yake bila majadiliano,” amesema na kushangiliwa.

Rais Samia amesema miradi inayokwenda kujengwa ndani ya miezi tisa ijayo ni mingi na mikubwa, hivyo akasisitiza kuwa utaratibu wa kutumia mzabuni mmoja badala ya kuitisha zabuni utasaidia kukamilisha miradi hii kwa wakati, ila akawataka watendaji serikalini na wananchi washiriki kwa kina kusimamia fedha hizi.

“Kila kona inakwenda kuchemka na miradi hii. Ma-DED wasimamie vizuri. Sitakuwa na huruma na mtu kuanzia kwa mawaziri wangu, hadi kwa wanaowafuata. Kwa sababu tukivurunda hapa, tutakuwa tunajiharibia na sitaki tutie doa, kwa sababu tunatarajia kuomba tena,” anasema.

Samia anataja muda wa utekelezaji wa miradi hiyo kuwa ni miezi tisa tu, kuanzia sasa na hataki icheleweshwe kwa visingizio vyovyote, huku akisisitiza makandarasi wa ndani ndio wanaotakiwa kuitekeleza.

“Sekta binafsi ichangamke kwa kuwa itahitajika saruji, mabati na vifaa vingine kwa wingi, kwa sababu fedha za miradi hii zinatakiwa zisitoke nje ya nchi. Zinapaswa kuzunguka humu ndani na makandarasi wa ndani wenye sifa wapewe kazi,” amesema na kuongeza:

“Kwa wasimamizi, hii miradi iishe kwa miezi tisa. Sitaki tusiitekeleze kwa visingizio. Wazabuni wapatikane kwa single sourcing’, mkitaka kufanya kwa utaratibu mwingine wa kutangaza zabuni kwa miezi mitatu mtatuchelewesha. Twende na single sourcing.

“Halmashauri, idhini itolewe na PPRA pia urasimu uondolewe katika misamaha ya kodi kwa vifaa kutoka nje ya nchi vinavyokuja kutumika katika miradi hiyo na CAG nawe fuatilia kwa karibu fedha za miradi hii.”

Pia anakataa utitiri wa kamati za kusimamia miradi hiyo usiwepo, ziwe chache, zikijumuisha wataalamu wa mikoa na wilaya ili kuwe na urahisi wa kuzibana pindi zitakapokosea.

“Kwa kuwa miradi hii inahusisha fedha, ndipo watu watataka nao wawepo. Sitaki kuundwe kamati nyingi, nataka kamati ndogo za wataalamu wa mikoa… ili watakapovurunda tuwabane wao,” anasema.

Katika hatua nyingine, ametaja mafanikio ya serikali yake kwa kipindi cha miezi sita, ikiwamo kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato na uendelezaji wa ujenzi wa miradi mikubwa ya kimkakati tangu ashike hatamu ya uongozi, huku akisema viatu vya mtangulizi wake marehemu Rais Dk. John Magufuli ni vikubwa kwake.

“Yaliyotendeka kwa miezi sita ni mengi. Mpango wa kuinua uchumi na kuikabili Uviko-19 kwa kupata mkopo wa masharti nafuu wa Sh trilioni 1.3 na wahisani wengine bado tuko katika mazungumzo nao,” amesema. 

Ametaja baadhi ya wahisani wanaoendelea na mazungumzo nao ni pamoja na China na Jumuiya ya Ulaya watakaotoa mikopo ya bei nafuu.

Anasema miezi sita ya mwanzo kwa uongozi wake ilikuwa migumu, kwani alikutana na wimbi la pili ya ugonjwa wa Uviko – 19, hali iliyoathiri uchumi wa dunia na Tanzania haikuachwa salama.

Hata hivyo, kutokana na juhudi alizofanya, hali imeanza kuimarika. Amesema serikali imefuta kodi za kero na ukusanyaji wa mapato umeimarika, huku uchumi ukikua. 

“Kwa robo ya pili ya mwaka, uchumi wetu umekua kwa asilimia 4.3 ukilinganishwa na asilimia 4 katika kipindi kama hiki kwa mwaka uliopita… akiba ya fedha za kigeni imeongezeka na kufikia dola milioni 5.8 za Marekani ukilinganisha na dola milioni 4.9 kwa kipindi kama hiki kwa mwaka uliopita.”

Amesema kati ya Aprili na Septemba, 2021 serikali imekusanya Sh trilioni 11.41 na imewekeza Sh trilioni 8.24 kwenye miradi ya maendeleo, suala ambalo halijapata kutokea, huku ikiwarejeshea Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT refund) wafanyabiashara kwa wastani wa Sh bilioni 451.3. 

Kwa muda mrefu kodi hii imekuwa hairejeshwi kwa wafanyabiashara kila inapokusanywa na TRA, hali iliyokimbiza wafanyabiashara wengi wenye mitaji mikubwa.

Serikali imelipa madeni ya ndani wastani wa Sh bilioni 439, ambayo ni ya watumishi wa umma, wazabuni wadogo na wakubwa yaliyokuwa ya muda mrefu. Mazingira ya uwekezaji pia yameimarishwa, kwani upatikanaji wa vibali umetoka siku 14 na zaidi hadi siku 1 mpaka 3, kulingana na mwombaji anavyokamilisha haraka nyaraka zinazotakiwa.

Rais Samia amesema utaratibu wa electronic single window (dirisha moja la kielektroniki) umesaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha mazingira ya uwekezaji nchini, huku akisema madeni ambayo bado yanadaiwa yanaendelea kuhakikiwa na serikali na kila senti halali italipwa.

Kutokana na mazingira kuboreshwa, miradi ya uwekezaji imeongezeka na kufikia dola bilioni 3.5 kwa mwaka huu, ikilinganishwa na dola milioni 647 katika mwaka uliopita. 

Pamoja uchumi kusinyaa kwa sababu ya corona, kwa Tanzania mauzo ya nje yameongezeka kutoka dola bilioni 2.4, hadi dola bilioni 3.4 katika kipindi kama hiki kwa mwaka uliopita. Brela wametoa leseni 6,051, hali inayoonyesha kurejea kwa imani ya wafanyabiashara nchini.

Rais Samia amesema bei ya mbolea imeleta mtikisiko kidogo, lakini serikali imetafuta ufumbuzi kwa kuhakikisha kinajengwa kiwanda cha mbolea jijini Dodoma. Pia serikali imenunua mahindi ya wakulima kwa Sh 500 kwa kilo, badala ya bei aliyoiita ya kinyonyaji ya Sh 300 kwa kilo.

Kuhusu miundombinu, amesema serikali itajenga barabara za njia nne katika njia za Dodoma – Singida, kutoka Dodoma – Morogoro na Dodoma – Iringa. Serikali inajenga meli mpya 5 na imeagiza ndege mpya 5, zitakazoongezeka kwa ndege 11 zilizopo sasa. Kwa upande wa barabara, serikali yake imetoa Sh bilioni 1.5 kwa kila jimbo la uchaguzi nchini kujenga barabara kwa kuanzia.

Katika miradi ya kimkakati, ambayo ni reli ya kisasa ya SGR, kwa sasa kipande cha Dar es Salaam – Morogoro, kimekamilika kwa asilimia 93, Morogoro – Makutupora (Dodoma) kimekamilika kwa asilimia 70 na tayari serikali imetumia Sh bilioni 132 kwa kipande cha Mwanza – Isaka. Magati Na. 1 – 7 katika Bandari ya Dar es Salaam ujenzi wake umekamilika na ujenzi wa Bwawa la Umeme la Mwalimu Nyerere umekamilika kwa asilimia 56.6.

Kwa upande wa elimu, serikali imeishatoa jumla ya Sh bilioni 145.49 kulipia elimu. “Waliokuwa wanasema elimu bure imekwenda, sasa wajue,” amesema Rais Samia. Ameongeza kuwa mikopo kwa wanafunzi tayari serikali imetoa Sh bilioni 208.49, huku ikikopa mkopo wa maendeleo kwa elimu ya juu wa Sh bilioni 972.

Rais amesema serikali imejipanga kujenga masoko na maeneo maalumu kwa ajili ya wamachinga nchi nzima, kwa ajili ya kuipa sura miji ya Tanzania badala ya hali ilivyo sasa ambapo wamachinga wametapakaa kila sehemu. Ameahidi kuumalizia mradi wa maji wa Same – Mwanga aliosema umekwama.

Amesema baada ya muda si mrefu, Watanzania wataanza kuajiriwa katika mashirika ya kimataifa na hii imetokana na yeye kufanya mazungumzo ya kimkakati na mashirika hayo.

Corona ameitaja kuwa ni changamoto kubwa, ambapo pamoja na serikali kupata dozi za chanjo kutoka Marekani na China, bado wananchi wanapaswa kuitumia fursa hii kuchanjwa ili kuepuka hatari ya kupata ugonjwa na kupoteza maisha. Hadi mwishoni mwa wiki, Watanzania wapatao 860,000 walikuwa wamechanjwa tayari.

Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Dk. Philip Mpango, amesema corona imeathiri nchi yetu kwa kusababisha vifo vya ndugu na jamaa, ambapo wataalamu wengi wamefariki dunia, huku familia milioni moja zikiingia katika umaskini uliotopea na sekta ya utalii ikianguka.

Amempongeza Rais Samia kwa jitahada zake za kuhami uchumi wa nchi kwa kufanikisha mkopo huo uliopatikana na kusaidia kuokoa maisha ya watu, huku akipongeza uamuzi wa Rais kutafuta chanjo kwa ajili ya Watanzania.

Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk. Hussein Ali Mwinyi, amesema katika fedha hizo wao watapata mgawo wa dola milioni 100, sawa na Sh bilioni 230 na ameahidi kuzisimamia kwa karibu zaidi.

“Nitahahikisha kuna nidhamu ya hali ya juu katika matumizi ya fedha hizo. Tunakuunga mkono katika uongozi wa serikali yako na kuhakikisha nchi yetu inapata maendeleo,” anasema.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, anasema atafuatilia kwa karibu fedha za miradi hiyo kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana.

Pia amemhakikishia Rais Samia kuwa ‘ameupiga mwingi’, na atapita vizuri sana mwaka 2025, na ataendelea vizuri hadi mwaka 2030, kwa kuwa Watanzania wanaheshimu na kuthamini kazi zake anazozifanya tangu ashike madaraka.

“Mheshimiwa Rais, ninasema umeanza vizuri, unaendelea vizuri, na kama wanavyosema umeupiga mwingi, umeanza vizuri, unaendelea vizuri, utapita vizuri sana mwaka 2025 na utaendelea vizuri hadi mwaka 2030,” amesema Majaliwa na kuibua shangwe na nderemo kwenye Ukumbi wa Jakaya Kikwete jijini Dodoma.

Awali, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Mwigulu Nchemba, amefafanua jinsi fedha hizo zitakavyotumika katika miradi mbalimbali kuwa zitajenga madarasa 15,000 kwa mpigo kwa shule za sekondari, madarasa 3,000 kwa shule za msingi na zitanunua madawati 462,795 ili wanafunzi wasibanane madarasani.

Pia anasema watajenga vyuo vya Veta katika mikoa sita vilivyokuwa katika hatua za mwisho za umaliziaji wake na vingine 26 vilivyokwama kwa muda mrefu: “Baada ya kupata mkopo huo wa IMF Septemba 7, mwaka huu ulituagiza tuje na mapendekezo ya namna ya kutekeleza miradi mbalimbali na tukakaa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Bajeti na kuja na mapendekezo ya utekelezaji wa miradi hiyo.

“Kupitia miradi hiyo unajenga historia tangu tupate uhuru kwa kutekeleza mambo makubwa ikiwamo ujenzi wa madarasa katika vyuo 17 vya ualimu pamoja na vyumba vya mihadhara na kuchapisha vitabu 10,812 vya nukta nundu kwa wanafunzi wetu wenye ulemavu wa macho,” anasema Mwigulu.

Anasema wametenga Sh bilioni 46.2 kwa ajili ya kutekeleza miradi ya maji itakayosaidia watu kunawa maji tiririka katika maeneo ya mijini yenye misongamano na Sh bilioni 55.5 zimetengwa kutekeleza miradi katika maeneo ya vijijini ili maji yapatikane kwa wakati huku magari 25 ya kuchimbia visima yatanunuliwa kwa mpigo na kila mkoa utakuwa na gari lake katika ofisi za RUWASA.

Pia anasema kupitia fedha hizo za mkopo, wametenga Sh bilioni 466.9 kwa ajili ya kuchukua hatua mbalimbali za kuidhibiti corona, ikiwamo ujenzi wa vyumba 72 vya uangalizi maalumu kwa wagonjwa mahututi (ICU) kutoka vitano vilivyokuwapo awali katika hospitali za rufaa maalumu na watanunua vifaa vyake vyenye thamani ya Sh bilioni 54.

Anasema fedha hizo zitanunua magari 20 ya kisasa ya kusafirishia wagonjwa (ambulance), ambapo tangu uhuru yalikuwapo mawili tu na zitanunua magari ya wagonjwa ya kawaida 375 na yatapelekwa katika halmashauri zote. 

Itanunuliwa pia mitambo ya kuchunguza uwepo wa maji ili kuepuka kubahatisha. Anasema watajenga miundombinu ya kisasa ya kutolea huduma za dharura katika hospitali 105 kutoka 10 za sasa. Pia watanunua magari 14 ya hududuma za chanjo.

Fedha hizo zitanunua vitanda 2,700 na magodoro na mashuka yake hospitalini, mashine za dawa ya usingizi 60, mashine za kidijitali za X-ray 87 zitakazogawiwa katika mikoa na wilaya na CT – Scan 29 kwa mpigo.

Hospitali zote za kanda zitapewa mashine za MRI, badala ya wagonjwa kuletwa Dar es Salaam. Watajenga vituo vinne vinavyotumia TEHAMA, ambapo taarifa za kila sampuli ya ugonjwa zitasafirishwa na kusomwa kidijitali. 

Vilevile watanunua mitungi 4,640 ya hewa tiba ya oksijeni itakayosambazwa katika hospitali mbalimbali nchini. Serikali pia itanunua mitambo ya kuchonga barabara kwa ajili ya Shirika la Taifa la Hifadhi za Taifa (TANAPA) kuchonga barabara wakati wote.

Spika wa Bunge, Job Ndugai, amesema Bunge litahakikisha linafuatilia kwa karibu utekelezaji wa miradi hii, hali itakayowaletea wananchi maendeleo ya kweli katika majimbo yao.

Please follow and like us:
Pin Share