NMB wamtia umaskini mstaafu

DAR ES SALAAM

Na Alex Kazenga

Uzembe unaodaiwa kufanywa na Benki ya NMB Makao Makuu umesababisha kushindwa kuondoa majonzi kwa mkunga mstaafu, Yustina Mchomvu, aliyetapeliwa fedha zake za mafao.

Fedha za mjane huyo mkazi wa Msindo, Same, mkoani Kilimanjaro, ziliibwa kitapeli Aprili mwaka huu na kuingizwa kwenye akaunti iliyofunguliwa Benki ya NMB Tawi la Mbagala, Dar es Salaam.

Akizungumza na JAMHURI, Yustina anasema awali aliyefanya utapeli huo, Said Omary Mkude, alimpigia simu akijifanya ni Meneja Mafao wa PSSSF Makao Makuu, Dodoma.

“Pamoja na kuripoti Kituo cha Polisi Same, hadi sasa NMB hawajatoa ushirikiano wa kutosha kwa mpelelezi wa kesi yangu,” anasema Yustina akimtaja jina askari anayeshughulikia suala hilo.

Kilichotokea

Awali, Watanzania walielezwa kwamba usajili wa ‘line’ za simu kwa alama za vidole ungekuwa muarobaini wa wizi wa fedha kupitia simu za mkononi, lakini, tukio alilokutana nalo Yustina linaonyesha kuwa hali bado ni tete.

Yustina ndiye mwathirika wa hivi karibuni aliyenusurika kuibiwa Sh milioni 40 za mafao yake kwa njia ya utapeli; hata hivyo, amejikuta akiibiwa Sh milioni 5.

“Nilistaafu kazi serikalini Septemba mwaka jana na kulipwa Sh milioni 40 kama mafao. Kwa kweli haikuwa halali. Nilipunjwa, kwani nilistaafu baada ya kufanya kazi kwa miaka 38.

“Nikashauriwa niandike barua ya malalamiko. Nikaandika na kuipeleka ofisi za PSSSF za Moshi mjini,” anasema mama huyo.

Kwa bahati mbaya, majibu ya malalamiko hayo aliyoyapata Aprili 7, mwaka huu, yakawa si msaada bali mwanzo wa huzuni aliyonayo hadi leo.

Yustina anasema siku hiyo alipokea simu kutoka kwa Mkude, akijitambulisha kama ofisa wa PSSSF kutoka Dodoma, akimueleza kuwa barua alizotuma zimepokewa na sasa anataka kuzifanyia kazi.

Katika malalamiko yake, Yustina aliwaeleza PSSSF kuwa kuna miaka hakuwekewa mafao yake japokuwa alichangia.

“Sasa Mkude aliponipigia, akaniuliza kama mimi ndiye Yustina na kwamba faili langu liko mezani kwake, nilimuamini. Sikuwa na wasiwasi hata kidogo. Ningehofia nini wakati anataja barua nilizoandika kiofisi?” anasema.

Mkude akamwambia kwamba maofisa wanaohusika na malalamiko ya kupunjwa mafao ya wanachama wamepitia nyaraka zote na kubaini kuwa ni ya kweli; na kwamba fedha alizopunjwa ni Sh milioni 19.5; “Kwa hiyo PSSSF tunataka kuziingiza fedha hizo kwenye akaunti yako,” Yustina anamnukuu Mkude akisema maneno hayo.

“Aliniambia ili nipate fedha hizo ni lazima niwe nimejiunga na huduma ya ‘NMB Mobile’, ambayo tayari nilishajiunga muda mrefu. Akaanza kunielekeza namba za kubonyeza kwenye simu yangu,” anasema Yustina.

Mama huyo anasema alifuata maelekezo hayo kwa umakini na kuingiza namba ya siri ili fedha aliyoahidiwa na Ofisa wa PSSSF (Mkude) iruhusiwe kuingia kwenye akaunti yake ya benki.

“Baada ya muda nikashituka. Nikaangalia salio. Nikaona fedha iliyomo kwenye akaunti ipo vilevile, haijaguswa. Nikazidi kupata imani kuwa ninayoelekezwa kufanya ni ya kweli. Nikaendelea na hatua nyingine alizokuwa ananielekeza.

“Baada ya muda mfupi, nikaangalia tena akaunti yangu. Nikashituka kuona fedha yote iliyokuwamo imeondolewa! Mungu wangu! Yaani akaunti imebaki na Sh 14,000 tu!” anasema.

Baada ya kubaini hilo, akampigia simu Mkude na kuhoji sababu ya fedha kuondolewa kwenye akaunti yake, akajibiwa kuwa ni tatizo la mtandao, na kwamba asubiri kidogo.

Hiyo ndiyo ikawa mara ya mwisho Yustina kuwasiliana na Mkude, kwa kuwa simu yake haijapatikana hadi leo; kitu kilichomtia hofu na kwenda kuripoti Kituo cha Polisi Same.

“Polisi wakanitaka niwapelekee ‘bank statement’ wajiridhishe. Nikapeleka na palepale nikabadili namba ya siri kwa sababu niliyokuwa nayo nilihisi imeshajulikana,” anasema Yustina. 

Fedha hizo, Sh 5,476,291, ziliibwa kutoka kwenye akaunti Na. 40502500019; NMB Tawi la Same, mali ya Yustina Aprili 7, mwaka huu. 

Hata hivyo, tangu Aprili 8, mwaka huu aliporipoti tukio hilo polisi, Yustina anasema hakuna ufumbuzi au msaada wowote aliopata, wala dalili za kurejeshewa fedha zake hakuna.

Kumbukumbu zinaonyesha kuwa fedha za mama huyo zilihamishiwa kwenye Akaunti Na. 20110052862; NMB Tawi la Mbagala Mtongani, Dar es Salaam, inayomilikiwa na Said Omary Mkude.

Muda mfupi baadaye fedha hizo zikatolewa kwa mikupuo mitatu; Sh 1,932,483 yenye Ref: EC 1008754570886, Sh 1,932,483 (EC 100875459614) na Sh 1,611,325 (EC 100875476081).

Polisi, PSSSF wazungumza

Wakati Yustina akiwalaumu Polisi kwa kuchelewa kumpa majibu stahiki, mpelelezi wa kesi hiyo (jina linahifadhiwa), anasema upelelezi wake unakuwa mgumu kutokana na kutopata ushirikiano wa kutosha kutoka NMB.

“Nilifika NMB Tawi la Mbagala, nikaomba kupata vielelezo na mawasiliano ya simu alivyoacha mhusika wakati anafungua akaunti. Wakanijibu kuwa wenye uwezo wa kutoa taarifa za mteja ni Makao Makuu ya NMB.

“Nikawapelekea barua kuomba taarifa hizo. Kinachosubiriwa ni majibu yao ili hatua nyingine za kisheria zifuate,” anasema.

Anasema kwa mujibu wa taratibu, taarifa hizo zitakapokuwa tayari zitatumwa NMB Mbagala ambao watazipeleka NMB Same, watakaozipeleka Kituo cha Polisi Same kwa hatua zaidi.

Kwa maana hiyo, kwa sasa Polisi wametulia wakisubiri mchakato huo.

Kwa upande wake Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kilimanjaro, Simon Maigwa, amelieleza JAMHURI kuwa kesi za wizi kwa njia ya mtandao haziwezi kuwa na majibu ya haraka kwa sababu huhusisha idara mbalimbali.

Wakati RPC Maigwa akijibu hivyo, Meneja Uhusiano wa PSSSF, James Mlowe, anasema katika siku za karibuni kumekuwa na ongezeko la kesi za wizi wa fedha za wastaafu kwa njia ya mtandao, akiwataka wastaafu kuwa makini.

Anakiri kuwapo matukio ya kitapeli ambapo matapeli hutumia majina ya idara za serikali kupiga simu kwa watu na kujitambulisha kama maofisa wanaotaka kuwasaidia.

Anataja sababu za ongezeko la kesi za aina hiyo kuwa ni wastaafu kupata fedha za kiinua mgongo na kuzitumia kwa fujo na kuishiwa mapema, hali inayowafanya kuzungumza na kila mtu wanayehisi anaweza kuwasaidia.

“Mwanzoni PSSSF kulikuwa na utaratibu wa watu wanaoingia ofisini kwetu kusaini kitabu cha wageni. Tukagundua kumbe kupitia kitabu kile kuna watu walikuwa wanachukua namba za wateja na kuanza kuwasumbua,” anasema Mlowe.

Mlowe anasema sasa wamebadili utaratibu, wageni wanaandika majina pekee bila kuweka namba za simu.

Anasema watu wasio waaminifu huenda kwenye ofisi za PSSSF na kusikiliza shida za wastaafu, kisha wanakwenda kwenye daftari la wageni kuchukua namba zao za simu kwa malengo yao.

Majibu ya NMB

JAMHURI limefika Makao Makuu ya NMB, Mtaa wa Ohio/Ally Hassan Mwinyi (Nyumba ya Sanaa) na kuelekezwa kumtafuta Meneja Uhusiano, Eunice Chiume, na kupewa anwani ya barua pepe ili atumiwe maswali.

Hata baada ya kumtumia maswali kuhusu Yustina na magumu anayopitia, na kutaka kujua hatua ambazo zimefikiwa na NMB na lini watatoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi, hadi tunakwenda mitamboni, Eunice hakuwa amejibu lolote.

JAMHURI likawasiliana na NMB kupitia huduma maalumu ya mtandao wa Whatsapp na kuwasilisha malalamiko ya Yustina.

Baada ya majadiliano ya hapa na pale, NMB wakajibu: “Tunaomba kufanya uchunguzi zaidi na tutawasiliana na wewe punde tu baada ya uchunguzi kukamilika.”